Dar es Salaam. Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amefichua siri ya namna mtoto wake wa miaka 18 alivyomuuliza swali lililomchochea kufanya uamuzi wa kurejea Chadema na kuachana na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mchungaji Msigwa aliyekuwa mbunge wa Iringa Mjini kupitia Chadema kwa miaka 10 (2010/20), alijiunga na CCM Juni 30, 2024 kabla ya kutangaza kurejea Chadema Mei 23, 2026 huku akitoa sababu kuu kwamba mauaji ya Oktoba 29, 2025 yalisukuma dhamira yake.
Aprili 23, 2026, Mwenyekiti wa Ripoti ya Tume ya kuchunguza matukio ya kabla na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman alipokabidhi ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan alisema kutokana na ghasia hizo, watu 518 waliuawa, wengine kujeruhiwa na uharibifu wa mali za umma na binafsi.
Kada wa Chadema, Mchungaji Peter Msigwa (kushoto) akifafanua jambo alipokuwa akifanyiwa mahojiano na waandishi waandamizi wa Mwananchi Communications Ltd, jijini Dar es Salaam leo Juni 2, 2026.
Mwananchi imefanya mahojiano maalumu na Msigwa jana Jumanne Juni 2, 2026, jijini Dar es Salaam kuhusu uamuzi wake wa kuondoka CCM alikokaa takribani miaka miwili na kurejea Chadema alikowahi kuwa mbunge na mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa.
Akizungumzia uamuzi wa kurejea Chadema, Mchungaji Msigwa amesema alitumia miezi sita kutafakari kuhusu uamuzi wake wa kuondoka CCM kutokana na mauaji ya wananchi yaliyofanyika wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Amesema mazungumzo ya kifamilia pamoja na dhamira yake iliyokuwa ikimsuta vilimgusa na kumfanya kutafakari upya msimamo wake wa kisiasa kabla ya kufikia uamuzi wa kurejea Chadema akiamini alifanya makosa kuondoka kwenye chama hicho.
Mchungaji Msigwa amesema jambo lililopigilia msumari uamuzi huo ni swali aliloulizwa na mtoto wake aliyetaka kufahamu kama yeye na kaka zake wawili wangeuawa kama vijana wengine siku ya uchaguzi, angeendelea kusimama kutetea haya.
Amesema hiyo dhamira ilianza baada ya uchaguzi wa Oktoba 29 kutokana na mauaji ambayo hayajawahi kutokea nchini, mpaka mtoto wake wa miaka 18 akamwambia kama yeye na kaka zake wawili Peter Junior na Jimmy, wangekuwa miongoni mwa waliokufa, angeendelea kutetea hayo.
“Nikichanganya na dhamira yangu ilivyonihukumu, nikaona kwamba hatuko sawa kama Taifa na mimi niliona nisifurahishe watu wa nje, nikachekesha, nikasifiwa, lakini nafsi yangu na dhamiri yangu vinanihukumu,” amesema Mchungaji Msigwa.
Amesema maneno hayo ya mtoto wake yalichanganyika na dhamira yake iliyokuwa ikimsuta mara kwa mara akiona Taifa haliko katika hali sahihi. Hivyo, aliamua kufuata kile alichoamini ni sahihi na kurejea Chadema kuendelea mapambano.
Kada wa Chadema, Mchungaji Peter Msigwa (kushoto) akifafanua jambo alipokuwa akifanyiwa mahojiano na waandishi waandamizi wa Mwananchi Communications Ltd, jijini Dar es Salaam leo Juni 2, 2026.
“Nimerejea Chadema kwa kuomba msamaha na kusamehewa kwa makosa yote niliyofanya. Wale wote niliowakwaza ndani ya Chadema wanisamehe, kwani sikutegemea uchaguzi ungefanyika kwa namna iliyosababisha mauaji ya watu. Baadhi ya maiti hazijazikwa kwa heshima,” amesema.
Mchungaji Msigwa amesema Oktoba 29 ilibadilisha mtazamo wake kuhusu CCM, falsafa yake na namna inavyowatazama watu. Kipindi hicho kilikuwa kigumu kwake kwa kuwa hakutarajia watu kupoteza maisha kwa namna hiyo.
“Nilienda kupiga kura, lakini niliyoyaona katika kituo cha kupigia kura sikuyatarajia. Nilijiuliza maswali mengi, jambo lililonifanya kutafakari.
“Ni sawa na mchezaji wa Simba, Clatous Chama, alivyokuwa Yanga alipiga chenga nyingi na bado anapiga nyingi akiwa Simba. Nimegundua sikuwa sehemu sahihi, ndiyo maana nimerudi nyumbani,” amedai.
Alichokutana nacho Chadema
Mwanasiasa huyo mkongwe amesema baada ya kurejea Chadema amekutana na makundi matatu ya watu. Kwanza, ni lile lililofurahia uamuzi wake wa kurudi Chadema na limekuwa likimpigia simu, kumpongeza, kumtumia jumbe na kumfuata kwenye mitandao ya kijamii.
“Nimebaini kuhama kwangu kutoka Chadema kwenda CCM kuliwakwaza watu wengi sana, wakiwamo watumishi wa umma na wananchi wa kawaida ambao wengi wao siwafahamu, lakini wamekuwa wakinitafuta,” amesema.
Kundi la pili, amesema ni la watu wenye shaka kuhusu kama bado anaweza kuaminika au kama ni mtu anayefuata masilahi binafsi. Kundi la tatu, ni lile ambalo hata kabla hajahama halikumkubali na bado halimtaki.
“Makundi yote hayo matatu nilikuwa nayatarajia. Kama mwanasiasa na kiongozi, nayakumbatia yote. Wanaonikosoa, wenye mashaka na wanaonikubali wote ni watu wangu. Hali hiyo hainisumbui. Ninachowaomba wenye mashaka na wasioniamini wanipatie muda. Kama muumini, naamini watu hutambulika kwa matunda yao,” amesema.
Msigwa amesema wapo wanaodai kurejea kwake Chadema kumesababishwa na kukosa cheo ndani ya CCM. Amepinga madai hayo na kusisitiza alihama baada ya dhamira kuumsuta tangu Oktoba 29, 2025.
“Kama ningekuwa natafuta vyeo, basi vipo CCM. Fedha pia zipo CCM. Ningeweza kubaki huko na kuendelea kusifia huku nikisubiri uteuzi hata kwa miaka miwili. Kwa wasifu nilionao, kuwa CCM bado kungekuwa na manufaa kwangu. Lakini nimeamua kuondoka na kuja huku ambako tunaamini katika kusimamia misingi yetu,” amesema.
Amesema anafahamu ugumu wa maisha ya kisiasa ndani ya Chadema ambako hakuna vyeo vya kutegemea. Akitolea mfano wa Musa aliyeishi katika utawala wa kifalme wa Farao nchini Misri, alipokumbuka asili yake aliamua kuwatetea Waisraeli.
“Pamoja na faida ambazo ningeweza kuzipata ndani ya CCM, nimeamua kuondoka na kurejea mahali, ninapoamini ndipo ulipo wito wangu. Furaha yangu iko hapa. Nenda mashariki, nenda magharibi, lakini njia zote hunipeleka nyumbani,” amesema.
Mafunzo aliyopata CCM
Akizungumzia maisha yake ndani ya CCM, Mchungaji Msigwa amesema amepata mafunzo na majuto. Kwa upande mmoja, amekiri kuwa CCM ina nidhamu na inazingatia utaratibu wa utekelezaji wa shughuli zake za kichama.
“Jambo linalonisikitisha kuhusu CCM ni kuwa haiwezi tena kushinda uchaguzi bila kutegemea dola. Hilo ni hatari kwa usalama wa nchi. Serikali na chama tawala vina wajibu wa kulinda usalama wa Taifa, lakini chama kinapoanza kupoteza ushawishi na kutegemea vyombo vya dola kushinda uchaguzi, hali hiyo ni ya kutia wasiwasi,” amesema.
Msigwa amesema kutegemea dola kupata ushindi kunamaanisha taasisi muhimu za kisheria haziwezi kuwa huru.
Ametaja Mahakama, Bunge, polisi na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwa miongoni mwa taasisi zinazopaswa kufanya kazi kwa uhuru.
“Wananchi wakianza kuona Mahakama inatumika kwa masilahi ya watu wachache, hupoteza imani. Wakiona Bunge haliwasemei wala kuisimamia Serikali ipasavyo, hupoteza imani. Vivyo hivyo wanapoona polisi haitendi kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Msigwa amesema imani ya wananchi inapopotea, shinikizo ndani ya jamii huongezeka. Amesema watu wanaweza kukaa kimya kwa muda, lakini hali hiyo inaweza kuzaa madhara makubwa baadaye.
“Roho ya nchi ni kuwa na Mahakama huru ambazo hazingiliwi, majaji hawapelekewi maelekezo wala kutishwa. Roho ya nchi ni kuwa na polisi wanaotekeleza sheria kwa haki, na Bunge linaloisimamia Serikali. Uhuru huo ukikosekana, watu huanza kugeuka madikteta,” amesema.
Amesema nguvu ya Taifa imo katika uimara wa taasisi zake. Akirejea historia, alisema hata Dola ya Roma ilianguka licha ya kuwa na jeshi imara kwa sababu mifumo yake ilidhoofika.
“Libya ya Muammar Gaddafi, Ufaransa katika vipindi fulani vya historia, Urusi ya zamani na Cambodia ni mifano ya tawala zilizoporomoka kwa sababu taasisi hazikuwa imara. Tanzania inaelekea huko. Ndiyo maana nasema chama tawala hakina ushawishi wa kutosha bali kinategemea dola kushinda,” amesema.
Ashindwa kuchawishi mabadiliko
Alipoulizwa kama aliwahi kujaribu kushawishi mabadiliko akiwa ndani ya CCM, Mchungaji Msigwa amesema alikuwa mwanachama wa kawaida, ingawa wakati mwingine alipata nafasi ya kutoa maoni yake.
Kada wa Chadema, Mchungaji Peter Msigwa (kushoto) akifafanua jambo alipokuwa akifanyiwa mahojiano na waandishi waandamizi wa Mwananchi Communications Ltd, jijini Dar es Salaam leo Juni 2, 2026.
“Nchi hii inapata shida kwa sababu matatizo ya kisiasa yanapaswa kutatuliwa kisiasa, na matatizo ya kiuchumi yanapaswa kutatuliwa kiuchumi. Tunahitaji Katiba bora, vyombo huru vya uchaguzi na kusikiliza wananchi wanataka nini ili kujenga mazingira ya usawa,” amesema.
Amesema matumizi ya nguvu kutatua changamoto za kisiasa hayawezi kusaidia zaidi ya kuongeza shinikizo katika jamii. Ameongeza kuwa alijitahidi kutoa ushauri, lakini haikuwa rahisi kusikilizwa kutokana na ukubwa wa chama hicho.
Itaendelea kesho