Harakati ya muqawama ya Hizbullah ya Lebanon imesema imetoa kipigo kikubwa kwa wanajeshi wa Israel katika mji wa al-Bayyada, kusini mwa Lebanon, huku jeshi la Israel likiendelea kushindwa na wanajeshi wake wakikabiliwa na mbinu za kisasa zaidi.

Hizbullah imetangaza leo Jumatano kwamba imetekeleza mfululizo wa mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Israel huko al-Bayyada kusini mwa Lebanon, ikisema wapiganaji wake wamelenga kituo cha amri cha jeshi la Israel kwa maroketi kadhaa.

Harakati hiyo pia imeripoti kushambulia kitengo cha kijeshi cha Israel kilichokuwa kimesimama katika mji huo kwa makombora na kusema kitengo hicho hicho kililengwa tena katika operesheni tofauti.

Katika mashambulizi ya ziada, Hizbullah imesema imeharibu vifaru viwili vya Merkava vya Israel huko al-Bayyada kwa kutumia makombora yanayoongozwa kutoka mbali.

Haya yanajiri huko uchambuzi uliofanywa na The New York Times siku ya Jumanne ukieleza uvamizi wa Israel nchini Lebanon kwamba umekwama licha ya miezi kadhaa ya mapigano.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, utumiaji mkubwa wa Hizbullah wa ndege zisizo na rubani umewashangaza wanajeshi wa Israel na kudhoofisha vibaya mkakati wao wa nchi kavu.

Ripoti hiyo imesema ndege hizo zisizo na rubani, zinazoongozwa kupitia nyaya ambazo haziwezi kuvurugwa na mifumo ya kawaida ya kielektroniki, zimewafanya wanajeshi wa Israel kuwa shabaha dhaifu na kufichua udhaifu mkubwa katika maandalizi na mbinu za jeshi la Israel.

Ingawa vyanzo vya kijeshi vya Israel vilisema kwamba mashambulizi ya ndege zisizo na rubani ya Hizbullah siku ya Jumatatu yaliwaua wanajeshi wawili na kuwajeruhi wengine kumi, lakini Hizbullah imetoa mkanda wa video unaoonyesha ndege zake zisizo na rubani zikiwaandama na kuwashambulia wanajeshi na makamanda wa Israel katika maeneo ya Lebanon na Palestina yanayokaliwa kwa mabavu.

Uchambuzi huo umesisitiza kwamba tishio la hivi karibuni la Benjamin Netanyahu la kushambulia vitongoji vya kusini mwa Beirut na baadaye kufuta vitisho hivyo ni ishara ya kushindwa kunakoongezeka katika uwanja wa vita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *