
Unguja. Migogoro ya ardhi inayojitokeza mara kwa mara Zanzibar inachangiwa na ukosefu wa mpango mkuu wa ardhi, wamesema wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano, Juni 3, 2026, wakati wa mjadala wa kuchangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Mwakilishi wa Uzini, Said Azana Msingiri amesema migogoro mingi inatokea kutokana na maeneo mengi kutopimwa.
“Kwa hiyo, wizara ifanye haraka kupima maeneo haya na kuhakikisha yanatambulika, hata vikosi vya jeshi vijue maeneo yao. Kumekuwa na mvutano mkubwa kwani wananchi wanasema ni yao, na majeshi wanasema ni yao,” amesema Msingiri.
Ameongeza kuwa wananchi wanataka kutumia ardhi kwa kilimo, wizara inapaswa kuingilia kati ili kutatua migogoro hiyo.
Mwakilishi wa nafasi za wanawake, Moza Mohamed Khamis (ACT Wazalendo), amesema kuna malalamiko mengi yahusuyo fidia kwa wananchi wanaotegemea ardhi, hivyo Serikali iwasaidie si kuwakandamiza.
Amesisitiza umuhimu wa kuwa na mpango mkakati wa ardhi utakaosaidia kulinda maeneo yasichukuliwe bila ruhusa.
Mwakilishi wa Wawi, Bakar Hamad Bakar (CCM), amesema mpango mkakati ni ufunguo wa kutatua migogoro ya ardhi Zanzibar, kwani kila eneo litajulikana matumizi yake na umiliki wake tofauti na hali ya sasa.
“Kila eneo litaoneshwa shughuli yake na kuondoa changamoto zinazojitokeza kwa sasa, pia kupunguza gharama za fidia kwa Serikali,” amesema Hamad.
Mwakilishi wa Mfenesini, Othman Machano Said (CCM), amesema licha ya jitihada za Serikali, kutopimwa ardhi bado kumesababisha changamoto kwa wananchi.
Mwakilishi wa Paje, Jaku Hashim Ayub, amesema kuna haja ya marekebisho ya Sheria ya Ardhi, huku akihimiza kuwa Shirika la Nyumba lisingeweza kuondoa wapangaji kwa nguvu, hasa wazee, na kuongeza kuwa uwekezaji wa nyumba unakabiliwa na changamoto kubwa.
Awali, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Rahma Kassim Ali alisema kwa mwaka wa fedha 2025/26, wizara ilikadiria kutumia Sh308.057 bilioni kutekeleza vipaumbele vitano.
Vipaumbele hivyo ni pamoja na kujenga nyumba mpya za makazi na biashara, kutengeneza nyumba zilizopo, kuandaa na kufanya mapitio ya mipango mikuu na mipango ya kina ya matumizi ya ardhi Unguja na Pemba, pamoja na kuandaa mifumo ya Tehama ya utoaji huduma za jamii katika sekta ya ardhi na makazi, na kufanya utambuzi wa maeneo mbalimbali.
Aidha, wizara pia imepanga kuelimisha jamii kuhusu masuala ya ardhi na makazi kupitia kliniki ya ardhi na kuandaa miongozo ya ujenzi wa nyumba za makazi.