Chunya. Kufuatia uwekezaji mkubwa wa Serikali katika sekta ya madini umeiwezesha Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, kuongeza uzalishaji wa madini ya dhahabu kutoka kilo 300 hadi 400 kwa mwezi.

Hatua hiyo imeelezwa kuchochea ongezeko la mapato ya Serikali kutoka Sh6 bilioni hadi Sh7 bilioni kwa mwezi, huku makadirio kwa mwaka yakiongezeka kutoka Sh72 bilioni hadi Sh80 bilioni.

Takwimu hizo zimetolewa leo Jumatano, Juni 3, 2026 na Ofisa Madini Mkazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Laurence Mayala baada ya kutembelea mabanda ya maonyesho ya matumizi ya teknolojia za kisasa za uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya dhahabu.

Maonyesho hayo yameandaliwa na Kampuni ya Green Mining Awareness yenye lengo la kuwapa mbinu wachimbaji ya matumizi ya teknolojia za kisasa katika uzalishaji na uchenjuaji yaliyofanyika eneo la Sinjilili.

“Wastani uzalishaji wa dhahabu umeongezeka kutoka kilo 300 hadi 400 kwa mwezi, huku mapato ya Serikali yakiongezeka kutoka Sh6 bilioni hadi Sh7 bilioni,” amesema.

Amesema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji wa Serikali, kuimarika kwa mazingira ya biashara ya masoko ya madini ikiwepo mchango wa wachimbaji wa kati na wakubwa.

Mayala amesema kwa asilimia kubwa shughuli za uchimbaji wa madini ndiyo tegemeo kuu la uchumi wa Wilaya ya Chunya, huku zaidi ya leseni 2,000 za uchimbaji zimetolewa zikihusisha zaidi ya watu 100,000.

Akizungumzia kuhusu utoroshaji wa madini, amesema ofisi yake kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama inaendelea kufanya doria za mara kwa mara ili kudhibiti vitendo hivyo.

“Tumekuwa wakali kusimamia kuhakikisha madini yote yanayozalishwa yanauzwa katika masoko rasmi ya ndani yaliyowekezwa na Serikali.

“Mtu atakayebainika kujihusisha na utoroshaji wa madini atachukuliwa hatua za kisheria na kufikishwa mahakamani,” amesema.

Aidha, amewahimiza wachimbaji na wadau wa sekta ya madini kushiriki maonyesho hayo ya siku saba ili kujifunza teknolojia mpya zitakazoongeza tija, usalama na utunzaji wa mazingira.

Amesema Serikali imepongeza jitihada za waandaaji wa maonyesho hayo kukutanisha zaidi ya kampuni 15 za ndani na nje ya nchi kwa lengo la kutoa elimu ya matumizi ya teknolojia za kisasa za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

“Maonyesho yatasaidia kuwaondoa wachimbaji katika matumizi ya mbinu za kizamani, kuwajengea uwezo wa kutumia teknolojia bora ili kuwa mabalozi wa kutunza mazingira,” amesema.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Itewe, Focas Andrew ameiomba Serikali na taasisi za kifedha kuangalia upya masharti ya mikopo kwa wachimbaji wadogo ili kuwawezesha kupata mitaji na vifaa vya kisasa.

“Masharti ya mikopo ni magumu kwa wachimbaji wengi wadogo tukipata ufadhili wenye masharti nafuu tutaondokana na uchimbaji wa kubahatisha na kuongeza uzalishaji,” amesema.

Naye mchimbaji mdogo wa madini, Philipo Haule amesema maonyesho hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa kuwapa wachimbaji elimu kuhusu teknolojia mpya licha ya changamoto ya mitaji.

Ameshauri waandaji wa maonyesho hayo kufikisha elimu hiyo katika maeneo ya vijijini ambako bado kuna matumizi ya mbinu duni za uchimbaji zinazochangia uharibifu wa mazingira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *