
Katika kipindi hiki ambacho Tanzania inapitia mijadala mikubwa ya kisiasa na kijamii, jambo moja ambalo hatupaswi kulisahau ni kuendelea kutunza umoja wa taifa letu.
Tunaweza kutofautiana kwa mawazo, lakini bado tukabaki Watanzania wenye lengo moja la kuijenga nchi yetu.
Hili liliwekwa msisitizo na hayati Mwalimu Julis Nyerere akiwa nchini Ghana Machi 1997 akisema umoja hautatufanya kuwa matajiri, lakini unaweza kutufanya isiwe rahisi kwa watu wa nje kutudharau, kutugawa au kutunyanyasa.
Kwa miaka mingi, Tanzania imebaki kuwa mfano wa amani na mshikamano katika Afrika. Watu wa dini makabila na mitazamo tofauti wameishi kwa heshima na utulivu mkubwa. Huo ndio msingi uliotujenga kama taifa.
Msingi huo haupaswi kuchukuliwa kama jambo la kawaida, amani na umoja haviji venyewe, vinalindwa kwa busara, uvumilivu na namna tunavyotendeana kila siku kama wananchi wa nchi moja.
Leo Tanzania tunashuhudia mijadala ya siasa ambayo kidogo kidogo inaendelea kumega nyufa za taifa letu, kuondoa utu wa Watanzania hadi kufikia kiwango watu kufurahia vifo vya viongozi na wakati mwingine kuzusha matukio ya kusikitisha.
Mambo haya yalianza kidogo na yanaendelea kuweka misingi ya kuchukiana kwa hali zote, kubaguana kwa udini jambo ambalo ni hatari kwa Tanzania tuliyoijenga.
Siku zote watu wanaopanga kubomoa hata nyumba hawahitaji ramani lakini wanaojenga huitaji ramani na muda mrefu wa kufikiri namna anachokitaka kinapaswa kiwe.
Tanzania ni kama nyumba unaweza kuijenga kwa miaka zaidi ya 50 ukaibomoa ndani ya dakika 20, hii inaonyesha kwamba kubomoa ni kazi rahisi kuliko kujenga.
Swali ambalo sote tunapaswa kujiuliza je kwa tunayoyashuhudia hapa nchini kwetu hatuwezi kutumia busara kujadili, kukosoana na kukaa meza moja kuzungumza kuliko kupanga kuitawanya Tanzania yetu.
Katika taifa lenye watu milioni 60 na zaidi sote hatuwezi kukubaliana jambo moja, nakubali kwamba tunamawazo tofauti lakini kwanini mawazo hayo yajikite katika kutugawa.
Tunashuhudia mijadala mingi yenye hisia kali kupitia siasa mitandaoni na hata kwenye maisha ya kawaida, wakati mwingine watu wanabishana kwa hasira kuliko wanavyosikilizana kwa utulivu.
Tatizo si kutofautiana, kutofautiana ni sehemu ya maisha ya jamii yoyote, tatizo linaanza pale tofauti za mawazo zinapogeuka kuwa chuki au sababu ya kuumizana kwa maneno.
Jamii inapojengeka juu ya chuki, uhasama watu huanza kupotezana imani. Wanaanza kuangaliana kwa shaka badala ya kushirikiana. Na hali hiyo ikikua, huathiri hata maendeleo ya taifa.
Hakuna taifa linaloweza kusonga mbele ikiwa wananchi wake hawana utulivu wa moyo kwa wenzao. Umoja wa watu ndiyo nguvu ya kwanza ya maendeleo ya nchi yoyote.
Tanzania inahitaji mazungumzo zaidi kuliko mivutano. Inahitaji watu kusikilizana zaidi kuliko kushindana kwa sauti. Tunahitaji kujenga mazingira ya kuzungumza kwa utulivu hata tunapotofautiana.
Katika kipindi hiki, viongozi wetu wana nafasi kubwa sana ya kuleta watu pamoja, kuepukana na matendo yanayoonekana kama sehemu ya kuchochea hasira kwa kundi fulani au kubeza upande bali kwa nyakati hizi kuzungumza lugha ya kuunganisha.
Uongozi bora si wa kutoa majibu pekee ya changamoto zinazolalamikiwa bali wakati mwingine ni kusikiliza, kutafakari na kuunganisha watu hata pale wanapokuwa na maoni tofauti.
Lakini jukumu la kuilinda Tanzania si la viongozi peke yao, ni jukumu la kila Mtanzania. Tunachosema, tunachoandika na namna tunavyowachukulia wengine vina mchango mkubwa kwa ustawi wa taifa.
Ni wakati pia wa kila upande kujitazama, katika mjadala wa taifa, si rahisi upande mmoja kuwa sahihi kwa kila jambo, wakati mwingine tunahitaji kukubali pale tulipokosea.
Kukubali makosa si kushindwa ni ishara ya hekima, Taifa lenye watu wanaoweza kujikosoa lina nafasi kubwa ya kusonga mbele kuliko taifa ambalo kila kundi linaamini halikosei kamwe.
Tunapaswa kuepuka tabia ya kila upande kujiona uko sahihi kila wakati. Mtazamo huo hufunga milango ya mazungumzo na kufanya maridhiano kuwa magumu kupatikana.
Tukikosa kusikilizana leo, tunahatarisha kesho ya taifa letu, migawanyiko ya ndani inaweza kuacha majeraha ambayo huchukua miaka mingi kupona.
Zaidi ya hapo, taifa lenye migogoro ya ndani huwa dhaifu, udhaifu huo unaweza kutumiwa na watu wa nje wasiolitakia mema taifa.
Hivyo kama Watanzania, tuna wajibu wa kufikiria kizazi kijacho. Tanzania ya leo ni urithi kwa watoto wetu sasa na hata baadaye.
Mchambuzi ni mwandishi wa Gazeti la Mwananchi