
Hatimaye, baada ya kipindi cha karibu mwaka mzima cha malalamiko, hofu na sintofahamu, wakazi wa Mji Mkongwe wa Zanzibar pamoja na watu wanaofika katika eneo hilo sasa wanapumua kwa afueni.
Wengi wao wanaamini kuwa sasa ule msemo usemao baada ya dhiki huja faraja una maana halisi katika maisha yao ya kila siku.
Kwa muda mrefu, eneo hilo lilishuhudia malalamiko ya wananchi kuhusu vitendo vilivyodaiwa kufanywa na baadhi ya askari wa Mamlaka ya Mji Mkongwe waliokuwa wakivaa mavazi maalumu ya ninja.
Malalamiko hayo yalihusu watu kutandikwa mikong’oto, kuporwa fedha, simu za mkononi, baiskeli, pikipiki, funguo za magari na hata leseni za udereva.
Kwa sasa, hali imebadilika kwa kiasi kikubwa. Wafanyabiashara wadogo wadogo ambao kwa miezi kadhaa walikumbwa na hofu na kukosa uhakika wa kuendelea na shughuli zao, wameanza kurejea katika maeneo yao ya biashara.
Wachoma mihogo, wachoma mishikaki, wauza mbatata za urojo, kinamama wanaouza vitafunwa na uji, wauza dagaa, mikate pamoja na bidhaa nyingine mbalimbali sasa wanaendelea na shughuli zao za kujitafutia kipato kama ilivyokuwa hapo awali.
Katika kipindi hicho cha taharuki, Mji Mkongwe ulionekana kupoteza sifa yake ya kuwa eneo salama kwa wakazi na wageni. Malalamiko yalitawala katika vijiwe vya mazungumzo, vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na hata kufika ndani ya Baraza la Wawakilishi.
Pamoja na malalamiko hayo, viongozi wa Mamlaka ya Mji Mkongwe waliendelea kusisitiza kuwa operesheni zilizokuwa zikifanyika zilikuwa halali na zililenga kuimarisha usafi wa mazingira pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato. Viongozi hao walikanusha kuwapo kwa vitendo vya uonevu, uporaji na matumizi ya nguvu kupita kiasi, licha ya kuwapo kwa picha na video zilizosambaa zikionyesha watu wakipigwa au kunyanyaswa.
Hata hivyo, hali ya sasa inaashiria mwanzo wa ukurasa mpya. Mabadiliko ya uongozi yaliyofanyika ndani ya mamlaka hiyo yanaonekana kuwa miongoni mwa sababu zilizochangia kurejea kwa utulivu na kuondoa hofu iliyokuwa imejengeka miongoni mwa wananchi.
Aidha, wafanyabiashara wamepewa nafasi ya kuendelea na shughuli zao kwa kufuata utaratibu unaokubalika kisheria.
Leo hii, askari waliokuwa wakionekana mara kwa mara wakiwa na virungu, bakora na minyororo ya kufungia magari na pikipiki hawaonekani tena mitaani. Badala yake, hali ya kawaida na utulivu imeanza kurejea katika mitaa ya Mji Mkongwe.
Hatua za kurejesha utulivu zinastahili kupongezwa. Lakini pongezi pekee hazitoshi. Ni muhimu kuhakikisha kuwa yaliyotokea hayarudiwi tena kwa namna yoyote ile. Jamii yenye amani haiwezi kujengwa juu ya hofu, vitisho na matumizi ya nguvu yasiyozingatia misingi ya sheria na utu.
Kadhalika, mamlaka husika zinapaswa kuhakikisha kuwa madai yote yaliyotolewa dhidi ya baadhi ya askari yanachunguzwa kwa kina. Pale ushahidi wa picha, video au vielelezo vingine unapothibitisha kuwapo kwa ukiukwaji wa sheria, hatua stahiki zichukuliwe bila upendeleo ili kurejesha imani ya wananchi kwa taasisi za umma.
Si hivyo tu, wafanyabiashara waliopoteza mali zao, kuvunjiwa meza za biashara au kunyang’anywa vifaa vya kazi kama sufuria, sahani na bakuli wanapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma na haki. Wengi wao walitegemea biashara hizo kwa ajili ya kujikimu na kuhudumia familia zao.
Bila shaka, uhifadhi wa Mji Mkongwe ni jambo lisilopingika. Eneo hilo ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya utalii Zanzibar kutokana na historia yake, majengo ya kale na urithi wake wa kipekee unaotambuliwa kimataifa.
Hata hivyo, jukumu la kuulinda urithi huo halipaswi kutekelezwa kwa njia zinazoweka rehani haki, usalama na utu wa wananchi.
Kinachohitajika ni sheria na taratibu rafiki zinazowezesha usimamizi bora wa mazingira, biashara na huduma za umma bila kuleta migongano isiyo ya lazima kati ya mamlaka na wananchi.
Wageni na wenyeji wanapaswa kujisikia salama na kuheshimiwa wanapokuwa katika eneo hilo. Pia, kuna haja ya kuyatazama upya malalamiko ya muda mrefu kuhusu viwango vya faini vinavyotozwa kwa baadhi ya makosa.
Wapo wanaohoji mantiki ya adhabu za zaidi ya Sh100,000 kwa dereva wa bodaboda aliyekutwa ameegesha pikipiki mahali pasiporuhusiwa. Kwa wengi, kiwango hicho kinaonekana kuwa kikubwa ukilinganisha na hali halisi ya kipato cha wananchi wa kawaida.
Vivyo hivyo, utaratibu wa kuwatoza wafanyabiashara ada za usafi wa mazingira kila siku huku wakiwajibishwa kwa taka zinazoweza kutupwa na watu wasiojulikana karibu na maeneo yao ya biashara unahitaji kutafakariwa upya, ili kuondoa hisia za kutendewa isivyo haki.
Malalamiko mengine yanahusu ada za maegesho zinazodaiwa kutozwa hata nyakati za usiku wa manane au siku za mapumziko katika baadhi ya maeneo ya Mji Mkongwe. Hoja hizi nazo zinahitaji kusikilizwa na kufanyiwa tathmini kwa lengo la kujenga mfumo unaokubalika na wadau wote.
Kwa ujumla, mabadiliko yanayoonekana sasa yanatoa matumaini mapya kwa wananchi. Lakini matumaini hayo yataendelea kuwa na maana ikiwa yataambatana na mageuzi ya kweli katika namna mamlaka zinavyotekeleza majukumu yao.
Uongozi mpya wa Mamlaka ya Mji Mkongwe una nafasi ya kuandika historia mpya. Unaweza kujifunza kutokana na yaliyopita na kujenga mfumo wa usimamizi unaozingatia sheria, haki na utu wa wananchi. Huo ndio utakaokuwa msingi imara wa kuuhifadhi Mji Mkongwe na kuufanya uendelee kuwa fahari ya Zanzibar na kivutio kwa wageni kutoka ndani na nje ya nchi.