
Hata hivyo, hali ya ukosefu wa usalama, uharibifu wa miundombinu na kuanza kwa msimu wa mvua vinaendelea kuathiri utoaji wa msaada huo.
“Hali ni mbaya sana na inahitaji hatua za haraka ili kuokoa maisha ya watu wanaohitaji msaada kwa dharura,” amesema Mutinta Chimuka, Mkurugenzi wa WFP nchini Sudan Kusini. “Tunatumaini kuendelea kuwafikia wale wote wanaohitaji msaada. Hivyo basi, usalama wa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu pamoja na mizigo ya misaada ni muhimu ili tuweze kuongeza kiwango cha msaada na kuwafikia kwa ufanisi watu wote wenye uhitaji.”
Hali ya uhakika wa chakula Akobo
Kwa mujibu wa tathmini ya hivi karibuni ya uainishaji wa viwango vya upatikanaji wa chakula, IPC baadhi ya maeneo ya mkoa wa Akobo yako katika kiwango cha daraja la 5 la IPC ambalo ni Janga la njaa kali, moja ya kaunti nne zinazokabiliwa na hatari ya kutumbukia katika baa la njaa iwapo hali itaendelea kuzorota.
Makadirio yanaonesha kuwa hadi mwezi Julai:
- Watu takribani 97,000 watakuwa katika kiwango cha daraja la 3 la IPC (Mgogoro wa Chakula).
- Watu wapatao 85,000 watakuwa katika kiwango cha daraja la 4 la IPC (Dharura).
- Watu karibu 12,000 watakuwa katika kiwango cha daraja la 5 la IPC (Janga la Njaa Kali).
Mgogoro wa utapiamlo umeongezeka na kufikia kiwango cha daraja la 5 la IPC la Utapiamlo Mkali ambayo ni hali Mbaya Kupindukia kutokana na kuhama kwa watu, kupotea kwa vyanzo vya kujikimu, kusitishwa kwa huduma za afya na lishe, pamoja na kuongezeka kwa hatari ya magonjwa kutokana na msongamano wa watu.
Viwango vya utapiamlo mkali miongoni mwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na akina mama wanaonyonyesha vinaongezeka kwa kasi, jambo linaloongeza hofu ya kutokea kwa hali inayofanana na baa la njaa katika eneo hilo.
Mapigano yanayoendelea tayari yamesababisha watu takribani 142,000 kuhama kutoka Kaunti ya Akobo na maeneo ya jirani, huku zaidi ya 100,000 wakikimbilia nchini Ethiopia.
Aidha, kuporomoka kwa masoko ya ndani kutokana na migogoro na uporaji kumepunguza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa chakula.
Shughuli za WFP Akobo
Tangu kuanzishwa kwa hatua hizi za dharura wiki tatu zilizopita, WFP imewafikia zaidi ya watu 60,000 walio katika mazingira magumu katika Akobo, wakiwemo:
- Zaidi ya watu 15,000 waliopokea msaada wa chakula wa dharura.
- Karibu wanawake 6,000 wajawazito na wanaonyonyesha waliopokea virutubisho vya lishe.
- Zaidi ya watu 30,000 waliopokea biskuti zenye kutia nguvu HEB, ambazo ni chanzo muhimu cha lishe kwa watu walio safarini au waliokimbia makazi yao.
- Zaidi ya watoto 6,000 pamoja na wanawake wajawazito na wanaonyonyesha waliopokea vyakula maalumu vya lishe kupitia mpango wa lishe ya ziada kwa wote.
WFP na washirika wake pia wamefanya uchunguzi wa hali ya lishe kwa watoto 15,000, na kuwajumuisha watoto 3,000 wenye utapiamlo wa wastani wa kiwango cha juu katika programu za matibabu ya lishe.
Uratibu wa ugavi na usafirishaji
WFP imeendelea kuratibu na kusambaza misaada kupitia hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na:
- Kusafirisha tani metri 25 za biskuti zilizoongezwa virutubisho na vyakula maalumu vya lishe, ikiwemo tani 14.5 za nafaka zilizosafirishwa kwa ndege hadi maghala ya maeneo ya mbele.
- Kusafirisha kwa ndege tani 300 za bidhaa mbalimbali za chakula na lishe kwenda Akobo.
- Msafara wa malori 33 wa WFP na Kundi la Usafirishaji wa Misaada unaobeba zaidi ya tani metri 200 za chakula na vifaa vya lishe pamoja na tani 100 za vifaa vya msaada wa dharura.
- Zaidi ya safari 60 za ndege za WFP, ikiwemo kurusha misaada kutoka angani, kusafirisha mizigo kwa ndegeza masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa UNHAS, zilizobeba tani 430 za misaada muhimu.
- UNHAS pia imesafirisha zaidi ya wahudumu 200 wa misaada ya kibinadamu kuingia na kutoka eneo hilo.
- Kuongeza safari za ndege za UNHAS hadi mara tatu kwa wiki.
Katika msimu wa mvua, wakati usafiri wa barabara hautawezekana, WFP itaendelea kusaidia Akobo kupitia usafirishaji wa misaada kwa njia ya anga ili kuhakikisha msaada wa chakula haukatizwi.
Changamoto na mahitaji ya ufadhili
Ingawa ufikiaji wa maeneo ya Akobo umeimarika hivi karibuni, utoaji wa misaada ya kuokoa maisha bado unategemea kwa kiasi kikubwa usafiri wa gharama kubwa wa anga kutokana na hali ya ukosefu wa usalama.
Hatari ya kuzuka tena kwa mapigano bado ipo. Ni muhimu uhasama ukomeshwe na wahudumu wa misaada waendelee kupata fursa salama ya kuwafikia raia ili waweze kupokea msaada wanaouhitaji.
Utoaji endelevu na wa kuaminika wa huduma muhimu pamoja na msaada kwa jamii ni msingi wa kuimarisha hali ya maisha na kujenga upya njia za kujikimu.
WFP ina wasiwasi mkubwa kuhusu maelfu ya watu walio katika maeneo magumu kufikika, ambako njaa na utapiamlo vinatarajiwa kuongezeka zaidi wakati wa msimu wa upungufu wa chakula unaokaribia kwa kasi.