Video iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO inaanzia Gisakura wilayani Nyamasheke nchini Rwanda. Taswira kutoka angani inaonesha kijani kibichi… maana haya ni mashamba makubwa ya chai yaliyotanda katika vilima vya kijani kibichi huku wakulima wakionekana wakichuma majani ya chai kwa ustadi mkubwa.

Takribani kilomita kadhaa kutoka hapo, katika wilaya ya Nyaruguru kusini mwa Rwanda, mkulima Bertride Nyiranzigiye mwenye umri wa miaka 65 anaonekana akichuma majani ya chai na kuyaweka kwenye kikapu mgongoni. Bertride ambaye hapo awali alikuwa mkulima wa kujikimu kwa kulima mihogo na mahindi, sasa ni mfanyabiashara wa chai anayewaajiri wafanyakazi saba katika shamba lake la chai.

FAO Rwanda inatayarisha mkakati mpya wa sekta yake ya chai, unaoungwa mkono na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO). Mkakati huo unaweka kipaumbele katika uzalishaji wa chai yenye ubora wa juu, kwa lengo la kuongeza pato na kuboresha maisha ya wakulima wadogo wanaokabiliwa na changamoto zinazoongezeka kutokana na mzozo wa hali ya hewa, kupanda kwa gharama za mbolea, na ushindani kutoka kwa masoko ya kikanda

Kupitia mafunzo anayopata kutoka kwa wataalamu wa kilimo wanaosaidiwa na serikali na FAO, sasa anaelewa namna ya kuvuna majani bora zaidi ya chai ili kuongeza ubora wa mazao yake.

“Kinachofanya chai ya Rwanda kuwa bora ni namna tunavyotunza mashamba yetu. Tunavuna majani yenye ubora wa hali ya juu pekee. Tumefundishwa na wataalamu wa kilimo mbinu bora za kilimo cha chai, hivyo sasa tunajua namna ya kuchagua majani bora wakati wa mavuno.”

Video ya FAO inatuleta eneo jingine, hapa ni kiwandani, wafanyakazi wanaonekana wakichakata majani yaliyovunwa shambani huku magunia yakipangwa tayari kwa usafirishaji kwenda masoko ya nje ya nchi.

Bodi ya Taifa ya Maendeleo ya Mauzo ya Mazao ya Kilimo Rwanda, NAEB, inaeleza kuwa ubora wa chai ya Rwanda unatokana na mchakato mzima wa uzalishaji kuanzia shambani hadi kiwandani.

Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa NAEB, Sandrine Urujeni anasema uzalishaji nchini humo unazingatia viwango vya kimataifa.

“Majani ya chai ya Rwanda huzalishwa kwa kiwango kikubwa lakini lazima ichumwe kwa mikono kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha wakulima wanachagua majani bora. Pia tunahakikisha usindikaji wake viwandani unafuata viwango maalum. Mchanganyiko wa hatua hizi zote ndio unaoifanya chai ya Rwanda kuwa bora.”

Kwa mujibu wa FAO, chai ni zao la pili kwa mauzo ya nje nchini Rwanda baada ya kahawa. Zaidi ya watu laki moja wanahusika katika mnyororo wa thamani wa zao hilo kuanzia uzalishaji hadi usindikaji na biashara.

Hata hivyo, sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo gharama kubwa za usafirishaji kutokana na Rwanda kutokuwa na bandari, pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mwakilishi wa FAO nchini Rwanda Mohamed Aw-Dahir anasema kutokana na mazingira hayo, Rwanda imeamua kuwekeza zaidi katika uzalishaji wa chai ya ubora wa juu badala ya kuzingatia wingi wa uzalishaji pekee.

“Rwanda inalenga zaidi ubora, viwango na upatikanaji wa masoko bora. Hiyo ndiyo nafasi yake ya kipekee kutokana na hali ya uzalishaji, jiografia ya nchi yenye milima mingi, idadi ya wakulima wanaohusika na pia ukweli kwamba nchi haina bandari ya bahari. Kutokana na sababu hizo zote, serikali pamoja na FAO tunaamini kuwa kuwekeza katika ubora ndio mwelekeo sahihi kwa taifa.”

World Bank/A’Melody Lee Wafanyakazi katika bustani ya chai, nchini Rwanda, wanachuma majani ambayo yatasindikwa kuwa kinywaji hicho kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi. Kituo hicho, kilichoenea zaidi ya mamia ya hekta kinaajiri baadhi ya watu 200 wakati wa msimu wa kilele na 70 kwa mwaka mzima.

Kupitia mpango wa FAO wa MAFAP unaosaidia nchi kuchambua na kuboresha sera za kilimo na biashara ya mazao, Rwanda sasa inaandaa mkakati wake wa kwanza maalum wa sekta ya chai. Mkakati huo unalenga kuongeza uzalishaji, kuimarisha ubora wa chai na kuongeza thamani ya bidhaa zinazotokana na zao hilo.

Tukirejea shambani, kwa wakulima kama Bertride Nyiranzigiye, kilimo cha chai kimeleta mabadiliko makubwa ya maisha. Leo hii ana uwezo wa kulipia bima ya afya, ada za shule za watoto wake na hata kununua ng’ombe kwa ajili ya familia yake.

“Baada ya kuanza kulima chai, maisha yangu yalibadilika. Sasa ninaweza kulipa bima ya afya kwa wakati, kulipa ada za watoto wangu na kuboresha maisha ya familia yangu. Nimenunua ng’ombe na sasa tunapata maziwa nyumbani. Maisha yangu yameimarika sana tangu nianze kilimo cha majani ya chai.”

Meneja Mkuu wa kampuni ya SCON inayowasaidia wakulima wa chai katika wilaya ya Nyaruguru, Vincent Hategekimana, anasema majani ya chai ni zao la muda mrefu ambalo linaweza kunufaisha vizazi kadhaa vya familia moja.

“Majani ya chai ni zao la kudumu. Mara nyingi wazazi ndio wanaolima, lakini wanaonufaika zaidi ni watoto wao na hata wajukuu zao. Ni uwekezaji wa muda mrefu unaoendelea kutoka kizazi hadi kizazi.”

Katika video hii ya FAO, wakulima wanaonekana wakiendelea kuvuna chai katika mandhari ya vilima vya Rwanda vinavyojulikana kama “Nchi ya Vilima Elfu.” Licha ya changamoto zilizopo, matumaini yanaongezeka kwamba mkakati mpya wa chai utasaidia kuongeza kipato cha wakulima wadogo na kuimarisha nafasi ya Rwanda katika soko la kimataifa la majani ya chai.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *