Kituo cha Nguvu za Nyuklia cha Bushehr nchini Iran kimezalisha jumla ya kilowati-saa bilioni 80 za umeme, hatua inayochukuliwa kuwa mafanikio muhimu katika mpango wa nishati ya nyuklia kwa matumizi ya kiraia nchini.

Mohammad Eslami, mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI), amesema rekodi hiyo imefikiwa licha ya miaka ya mashinikizo ya maadui, vitisho na mazingira magumu ya kikanda.

Kwa mujibu wa Eslami, uzalishaji wa kilowati-saa bilioni 80 za umeme wa nyuklia umeokoa kiwango cha nishati kinacholingana na mapipa milioni 131 ya mafuta ghafi au mita za ujazo bilioni 21.3 za gesi asilia.

Amesema kuwa kituo hicho, ambacho ndicho pekee cha nyuklia kinachozalisha umeme nchini Iran, kimeendelea kufanya kazi kwa usalama na utulivu katika kipindi chote cha uendeshaji wake.

Eslami ameongeza kuwa shughuli za kituo cha Bushehr zimezuia utolewaji wa takribani tani milioni 86.3 za uchafuzi wa mazingira kwa miaka yote ya uendeshaji wake.

Amesema mafanikio hayo ni hatua nyingine muhimu kwa sekta ya nyuklia ya Iran na ishara ya kujitegemea, uwezo wa kiteknolojia na ustahimilivu wa taifa la Iran.

Kituo cha Nyuklia cha Bushehrkiliunganishwa na gridi ya taifa ya umeme Septemba 2011 na ndicho kituo pekee cha nyuklia kinachofanya kazi nchini Iran. Kituo hiki kina mchango muhimu katika uzalishaji wa umeme wa taifa hilo.

Marekani na Israel zililenga maeneo yaliyo karibu na kituo hicho mara kadhaa wakati wa mashambulizi yao dhidi ya Iran mwezi Machi, jambo lililozua wasiwasi kuhusu usalama wa miundombinu ya nyuklia kwa matumizi ya kiraia.

Licha ya mashambulizi hayo, kituo hicho kiliendelea kufanya kazi huku kikizingatia viwango vya juu vya kimataifa vya usalama na kudumisha uzalishaji wa umeme bila kukatizwa.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *