
Hata hivyo, kwa muda mrefu bahari imekuwa ikikabiliwa na shinikizo kubwa, na siku zijazo zinatishia kuleta changamoto zaidi ambazo zinaweza kuhatarisha si afya ya bahari pekee, bali pia mustakabali wa binadamu.
Wataalamu wapatao 550 kutoka nchi 86 wametumia karibu miaka mitano kuandaa tathmini ya kurasa 1,600 inayofafanua changamoto zinazoikabili bahari. Tathmini hiyo ya kisayansi, inayojulikana kama “Tathmini ya Dunia ya Bahari”, inalenga kutoa maarifa yanayohitajika ili kulinda na kudumisha afya ya sayari yetu.
Haya ndiyo mambo muhimu yaliyobainishwa katika tathmini hiyo.
Bahari inawahusu watu wote, popote walipo
- Bahari inaathiri maisha ya kila siku ya kila mtu, hata wale wasiokaa katika maeneo ya pwani.
- Husaidia kudhibiti hali ya hewa kwa kufyonza sehemu kubwa ya joto la ziada duniani pamoja na gesi hatari zinazochangia mabadiliko ya tabianchi. Bila mchango wake wa kupooza dunia, hali mbaya zaidi za hewa zingekuwa za kawaida, na kuhatarisha uhakika wa chakula, minyororo ya usambazaji na sekta ya bima.
- Ni chanzo muhimu cha chakula. Akiba ya samaki inapopungua au minyororo ya usambazaji inapovurugwa kutokana na athari za tabianchi au uvuvi haramu, bei hupanda si kwa dagaa pekee bali pia kwa vyakula vingi vinavyotegemea biashara ya kimataifa na uchumi wa maeneo ya pwani.
- Bahari huchangia afya ya akili na mwili, hutoa dawa mbalimbali na sehemu kubwa ya hewa ya oksijeni tunayovuta.
- Pia inasaidia biashara ya kimataifa yenye thamani ya matrilioni ya dola, utalii na ajira.
Bahari inakabiliwa na shinikizo linaloongezeka
Shughuli za binadamu zinaendelea kubadilisha mifumo ya ikolojia ya baharini. Idadi ya watu duniani ilifikia bilioni 8.2 mwaka 2024, huku asilimia 37 ya watu hao wakiishi ndani ya kilomita 100 kutoka pwani.
Hali hiyo imesababisha shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii kujikita katika maeneo ya pwani yaliyo hatarini, na kuongeza matumizi ya rasilimali za asili, ujenzi wa miundombinu, utupaji wa taka na uharibifu wa makazi ya viumbe.
Wakati huo huo, maendeleo ya shughuli za baharini mbali na pwani yanaongezeka, ikiwemo mashamba ya kuzalisha umeme wa upepo baharini, miundombinu ya mafuta kwenye kina kirefu cha bahari, pamoja na nyaya na mabomba yanayopita chini ya bahari, ambayo yote yanabadilisha mazingira ya viumbe vya baharini.
Mabadiliko ya tabianchi yanabadilisha bahari
Takwimu kuhusu ongezeko la joto la bahari na kupanda kwa kina cha bahari zinaonesha hali inayotia wasiwasi:
- Kasi ya kupanda kwa kina cha bahari kutokana na kuyeyuka kwa barafu na kuongezeka kwa ujazo wa maji kutokana na joto imeongezeka maradufu kutoka milimita 1.9 kwa mwaka kabla ya 2015 hadi milimita 4.3 kwa mwaka mwaka 2023.
- Joto katika eneo la Aktiki linaongezeka mara nne zaidi ya wastani wa dunia.
- Maeneo yenye kiwango kidogo sana cha oksijeni, yanayojulikana kama maeneo yaliyokufa sasa yanafikia kilomita za mraba milioni 4.5.
- Asilimia 16 ya ongezeko lote la joto la bahari tangu mwaka 1955 limetokea baada ya mwaka 2018.
Bioanuwai ya baharini inaendelea kupungua
Viumbe vya baharini vinakabiliwa na shinikizo kubwa. Hali hiyo inaonekana wazi kupitia kupungua kwa takriban asilimia 80 ya miamba ya matumbawe katika Bahari ya Karibea tangu miaka ya 1970.
Iwapo ongezeko la joto duniani litazidi nyuzi joto 1.5 za celsiasi juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda, asilimia 90 ya miamba ya matumbawe duniani inaweza kutoweka.
Mifumo muhimu ya ikolojia ya pwani kama mikoko na nyasi za baharini inaendelea kupungua.
Aidha, viumbe mbalimbali kuanzia planktoni hadi mamalia wa baharini vinahamia kuelekea ncha za Kaskazini na Kusini za dunia kutokana na kuongezeka kwa joto, huku viumbe wageni visivyo vya asili vikienea kwa urahisi zaidi katika mazingira yaliyobadilika.
Uchafuzi wa bahari unaongezeka
Uchafuzi wa bahari unaendelea kuongezeka kwa kasi.
Kila mwaka tani milioni 52 za taka za plastiki huingia baharini, na kuchangia uwepo wa takriban chembe trilioni 24 za mikroplastiki ambazo sasa zimeonekana kuathiri zaidi ya aina 4,000 za viumbe vya baharini.
Uchafuzi wa kemikali nao unaongezeka, huku zaidi ya kemikali 4,000 zinazotokana na dawa na bidhaa za matumizi binafsi zikigunduliwa katika maji ya bahari.
Habari njema ni kwamba baadhi ya vichafuzi vya zamani kama zebaki vimepungua katika maeneo fulani duniani.
Mifumo ya chakula kutoka baharini iko hatarini
Bahari ni chanzo muhimu cha lishe na kipato kwa mamilioni ya watu duniani, ikitoa asilimia 20 ya protini ya wanyama inayoliwa na binadamu.
Ufugaji wa viumbe wa majini unaendelea kukua na sasa ni sekta yenye thamani ya dola bilioni 90 duniani.
Vilevile, watu milioni 121 hushiriki katika uvuvi wa burudani baharini, jambo linalochangia uchumi wa maeneo mengi pamoja na ustawi wa jamii.
Hata hivyo, uthabiti wa mifumo hii unazidi kutishiwa:
- Asilimia 37 ya akiba ya samaki duniani ilivuliwa kupita kiasi mwaka 2021.
- Uvuvi haramu, usioripotiwa na usiodhibitiwa huondoa kati ya tani milioni 8 hadi 14 za samaki kila mwaka na kuzalisha mapato haramu ya dola bilioni 9 hadi 17.
- Milipuko ya magonjwa, uchafuzi wa mazingira na athari za tabianchi vinaendelea kuhatarisha uendelevu wa muda mrefu wa ufugaji wa viumbe wa majini na sekta ya uvuvi.
Uchumi wa bahari ni mkubwa lakini bado haujadumu
Thamani ya uchumi wa bahari inakadiriwa kufikia dola trilioni 1.5 kwa mwaka na inatarajiwa kuzidi dola trilioni 3 ifikapo mwaka 2030.
Sekta ya utalii wa pwani na baharini inasaidia ajira milioni 174 duniani.
Jitihada zinaendelea kufanyika ili kuelewa athari za muda mrefu na uendelevu wa uzalishaji wa mafuta na gesi baharini pamoja na usafirishaji wa mizigo kwa meli, ambao unasafirisha zaidi ya asilimia 80 ya biashara ya dunia na pia kuchangia uzalishaji wa gesi chafuzi.
Utawala na maarifa kuhusu bahari
Ushirikiano wa kimataifa katika usimamizi wa bahari unaongezeka, lakini uwepo wa mikataba 57 ya kimataifa inayohusiana na ulinzi wa bahari umechangia kuwepo kwa mifumo iliyogawanyika ya usimamizi.
Kufanikisha uchumi endelevu wa bahari kunahitaji usawa na ushirikishwaji mkubwa wa maarifa pamoja na desturi za jadi za jamii za Wenyeji wa asili.
Bila mchango wao, itakuwa vigumu zaidi kufanikisha afya ya bahari, ustawi wa jamii na maendeleo endelevu na yenye usawa.
Pia bado kuna mapengo makubwa ya maarifa kuhusu bahari. Kufikia mwaka 2025, ni asilimia 27 pekee ya sakafu ya bahari iliyokuwa imechorwa ramani, hali inayomaanisha kuwa mifumo ya ikolojia ya kina kirefu cha bahari, michakato ya kibaolojia na athari zinazojumlishwa bado hazieleweki vya kutosha.
Suluhu zipo, lakini hatua za haraka zinahitajika
Licha ya changamoto zinazoongezeka, suluhisho zipo. Miongoni mwao ni matumizi ya mbinu za asili za kuhifadhi mazingira, kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi na kupanua maeneo ya hifadhi za baharini.
Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa hata kurejesha kikamilifu mifumo ya ikolojia ya bahari kungechangia takriban asilimia mbili pekee ya malengo ya kimataifa ya kupunguza athari za tabianchi, jambo linaloonesha umuhimu wa mabadiliko makubwa ya kimfumo.
Muongo ujao utakuwa wa maamuzi. Bila hatua za haraka na za pamoja za kimataifa, afya ya bahari itaendelea kudorora, na kuhatarisha uthabiti wa hali ya hewa, bioanuwai, usalama wa chakula, ajira na ustawi wa mabilioni ya watu duniani.