
Jeshi la Nigeria limetangaza Jumapili, Juni 7, kuachiliwa kwa mateka mia kadhaa waliokuwa wakishikiliwa na Boko Haram katika Jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria, tangu mwanzoni mwa mwezi Machi. Watoto wawili wachanga walifariki wakati wa operesheni ya ukombozi, iliyofanyika siku ya Jumamosi.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu huko Lagos, Harmony Pondy Nyaga
Ilichukua wiki kadhaa za maandalizi ya kina ya kijasusi ili kufikia eneo lenye ngome kubwa ambapo mamia ya mateka walikuwa wakishikiliwa na Boko Haram katika Milima ya Mandara kwenye mpaka na Cameroon.
Watoto wawili wachanga walifariki wakati wa zoezi la kuwahamisha.
Kulingana na Haruna Sani, msemaji wa jeshi la Nigeria, waathiriwa, hasa wanawake na watoto, walikuwa wametekwa nyara katika eneo la Ngoshe kusini mwa Jimbo la Borno.
Ni katika eneo hili ndipo utekaji nyara mkubwa uliofanywa na Boko Haram mwezi Machi, mwanzoni mwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Kaskazini mwa Nigeria mara kwa mara hukabiliwa na mashambulizi na utekaji nyara unaofanywa na wanajihadi pamoja na makundi yenye silaha yanayojulikana kama majambazi.
Kwa siku kadhaa, maandamano katika mitaa ya Nigeria yamekuwa yakidai kuachiliwa kwa wanafunzi arobaini na walimu wao saba waliotekwa nyara katikati ya mwezi Mei katika Jimbo la Oyo, utekaji nyara mkubwa ambao haujawahi kutokea kusini mashariki mwa nchi.