Washiriki wanajadili namna ya kutokomeza ukandamizaji, ukatili na manyanyaso dhidi ya watu wenye ulemavu, kuimarisha mifumo ya huduma na msaada, pamoja na kuongeza ushiriki na uwakilishi wao katika maisha ya kisiasa na umma.

Mafanikio ya kihistoria katika haki za watu wenye ulemavu yamepatikana kupitia juhudi kubwa na za muda mrefu, lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanywa ili kutimiza ahadi zilizotolewa miongo miwili iliyopita. 

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, wakati wa ufunguzi wa mkutano huo leo 

“Dunia inanufaika pale ambapo kila mtu anapata nafasi ya kutumia ujuzi wake kwa manufaa ya binadamu na kufuatilia ndoto zake,” amesema Katibu Mkuu katika kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa “Majadiliano yenu leo ni hatua muhimu kuelekea dunia ambayo kila mmoja wetu anaheshimiwa na kujumuishwa.”

COSP19 yakutanisha wadau kutoka duniani kote

Mkutano huo unaojulikana kama COSP19 ni Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu CRPD na unafanyika kuanzia leo tarehe 9 hadi 11 Juni chini ya kaulimbiu: “Kuadhimisha na kuimarisha mafanikio yaliyopatikana na kuunda awamu mpya ya utekelezaji katika dunia inayobadilika.”

Mkutano huo unajumuisha majadiliano ya meza ya duara, uchaguzi, maamuzi kuhusu hatua za baadaye pamoja na ushuhuda wa moja kwa moja kuhusu changamoto, suluhu bunifu na hadithi za mafanikio kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Maendeleo yapo, lakini kasi yake haikubaliki

Hatua zote za mkutano huu zinajengwa juu ya Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu (CRPD), ambao ni makubaliano ya kisheria yanayozitaka nchi wanachama kuheshimu, kukuza na kulinda haki za watu wenye ulemavu. Mkataba huo ulipitishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2006 na sasa umeridhiwa na nchi 192.

Miaka ishirini baadaye, mafanikio makubwa yamepatikana, ikiwemo zaidi ya asilimia 90 ya nchi kuwa na sheria zinazolinda haki za watu wenye ulemavu. Hata hivyo, ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Ulemavu na Maendeleo inaonesha kuwa karibu viashiria vyote vya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) vinavyohusu watu wenye ulemavu haviko katika mkondo unaotarajiwa.

“Ingawa maendeleo yapo, kasi yake ni ndogo mno na haikubaliki,” amesema Katibu Mkuu.

Dunia inaweza kubuniwa upya kwa ajili ya wote

Akizungumzia changamoto zinazoikabili dunia, zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, migogoro na ongezeko la gharama za maisha, Bwana. Guterres amesema kuwa mara nyingi watu wenye ulemavu hujikuta wakiishi katika mazingira yaliyoundwa na watu wengine na kwa ajili ya watu wengine.

“Mara nyingi sana, kuishi na ulemavu kunamaanisha kuishi katika dunia iliyobuniwa na wengine na kwa ajili ya wengine. Kwa bahati nzuri, inawezekana kuibuni upya dunia hiyo,” amesema.

Ameongeza kuwa Mkakati wa Umoja wa Mataifa wa Kujumuisha Watu wenye Ulemavu unalenga kuhakikisha mabadiliko yanayozingatia uzoefu na maarifa ya watu wenye ulemavu wenyewe.

“Kwa pamoja, tuhakikishe haki za kila mtu mwenye ulemavu zinatimizwa na tujenge mustakabali wenye usawa na ustawi kwa wote,” amesisitiza.

Asasi za kiraia zapaza sauti zao

Kabla ya kuanza rasmi kwa COSP19, jamii na mashirika kutoka kote duniani yalikutana Jumatatu katika Kongamano la Asasi za Kiraia lililofanyika chini ya mwavuli wa mkutano huo.

Washiriki walijadili masuala mbalimbali muhimu, ikiwemo namna ya kujenga jamii zenyemnepo, kuimarisha ushiriki wa kiraia unaofikika kwa wote, pamoja na kukuza uongozi na utetezi katika maisha ya kisiasa na ya umma.

Miongoni mwa mada zilizojadiliwa ni mafanikio, changamoto na mustakabali wa mageuzi ndani ya Umoja wa Mataifa, pamoja na juhudi za kujenga dunia isiyo na unyonyaji, vurugu na unyanyasaji dhidi ya watu wenye ulemavu.

COSP19 kwa ufupi

  • Mikutano ya COSP imekuwa ikifanyika kila mwaka katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York tangu mwaka 2008. 
  • Mikutano hiyo hujadili masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa haki za watu wenye ulemavu. 
  • Washiriki wanaweza kufuatilia mijadala yote mubashara au kwa kurejea kupitia UN Web TV, ikijumuisha tafsiri ya lugha ya alama na maandishi yanayoonekana kwenye skrini. 
  • Mjadala wa mwaka huu unalenga kutathmini mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 20 tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu na kuweka mwelekeo wa hatua za baadaye.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *