Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika laUmoja wa Mataifa la Kazi Duniani (ILO), Gilbert F. Houngbo, ambaye ametoa wito wa hatua za haraka na za pamoja ili kutokomeza tatizo hilo.

“Hali hii haikubaliki lazima tuongeze kasi ya hatua za kukomesha ajira za watoto,” amesema Houngbo katika ujumbe wake wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ajira za watoto ambayo kila mwaka huadhimishwa Juni 12.

Dira mpya ya dunia ya kukomesha ajira za watoto

Houngbo amesema kuwa dunia sasa ina mwongozo madhubuti kupitia Mfumo wa Kimataifa wa Marrakech wa Hatua Dhidi ya Ajira za Watoto, ambao unaweka mkazo katika ajira zenye staha kwa wazazi, elimu bora kwa wote, mifumo ya ulinzi wa hifadhi ya jamii na sheria pamoja na taasisi imara.

Kwa mujibu wake, mfumo huo unaweka kwa mara ya kwanza viashiria vya wazi vya kupima maendeleo pamoja na utaratibu wa uwajibikaji utakaosaidia kufuatilia utekelezaji wa ahadi zilizowekwa.

“Mfumo wa Marrakech unatupatia ramani ya njia inayojengwa juu ya ajira zenye staha kwa wazazi, elimu bora kwa wote, ulinzi wa kijamii na sheria pamoja na taasisi imara,” amesema.

Kadi nyekundu kwa ajira za watoto

Kaulimbiu ya mwaka huu,ya Siku ya Kupinga Ajira kwa Watoto ni “Kadi Nyekundu kwa Ajira za Watoto: Mchezo wa Haki kwa Watoto, Kazi zenye Staha kwa watu Wazima,” inalenga kuhamasisha serikali, waajiri, wafanyakazi na jamii kwa ujumla kuongeza juhudi za kulinda haki za watoto.

Houngbo amesema kaulimbiu hiyo ni ukumbusho kwamba kila mtoto anastahili kupata elimu, kucheza na kukua katika mazingira salama na yenye ulinzi.

“Kila mtoto ana haki ya kujifunza, kucheza na kukua akiwa amelindwa na salama,” amesisitiza.

Wito wa hatua za pamoja na za dharura

Licha ya maendeleo yaliyopatikana katika baadhi ya maeneo ya dunia, ILO imeonya kuwa kasi ya sasa haitoshi kufikia lengo la kutokomeza ajira za watoto katika miaka ijayo bila juhudi mpya na uwekezaji mkubwa zaidi.

Houngbo ametoa wito kwa serikali, sekta binafsi, mashirika ya wafanyakazi na wadau wengine kuunganisha nguvu katika kutekeleza hatua zilizokubaliwa kimataifa.

“Kwa pamoja, tuchukue hatua kwa dharura na kwa azma thabiti ili kukomesha ajira za watoto,” amesema.

ILO inaeleza kuwa kukomesha ajira za watoto si tu suala la kulinda haki za watoto, bali pia ni uwekezaji muhimu kwa maendeleo endelevu, ustawi wa jamii na mustakabali wa uchumi wa dunia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *