Waendesha mashtaka wa Italia wameanzisha uchunguzi dhidi ya Waziri wa Usalama wa Israel mwenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia, Itamar Ben-Gvir kuhusu mateso, unyanyasaji na utekaji nyara wa wanaharakati walioshiriki katika msafara wa Global Sumud Flotilla wa kupeleka misaada ya kibinadamu kwa watu wa Gaza, mwezi uliopita.

Ripoti zinasema, iwapo waendesha mashtaka watahitimisha kuwa kuna sababu za kutosha za kumfungulia mashtaka, watatoa ombi rasmi la kuanzishwa kesi dhidi yake.

Ben-Gvir, ambaye alichapisha video za kuaibisha za wanaharakati hao wakilazimishwa kupiga magoti huku wakipeperushiwa bendera ya Israel mbele yao, pamoja na picha zinazomuonyesha Ben-Gvir akimsukuma mwanaharakati mwanamke na kuumpiga chini kwa nguvu.

Serikali ya Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni ilikosoa jinsi wanaharakati wa Global Sumud Flotilla walivyotendewa akisema “hakukubaliki” na kumwita balozi wa “Israel” kwa ajili ya kutoa maelezo. Roma pia imeuhimiza Umoja wa Ulaya kuzingatia suala la kuweka vikwazo dhidi ya Ben-Gvir.

Vilevile, Ufaransa imeripotiwa kuchukua hatua ya kumzuia Ben-Gvir kuingia katika ardhi yake, na kuzidisha mzozo wa kidiplomasia kote Ulaya. Poland pia imempiga marufuku Ben-Gvir kuingia nchini humo kwa muda wa miaka mitano.

Awali, kundi la Al-Samoud Global Flotilla, limechapisha ushuhuda kutoka kwa wanaharakati wake walioachiliwa huru, likishutumu jeshi la Israel kuwa limewanyanyasa kimwili na kingono washiriki wa msafara huo.

Al-Samoud Global Flotilla imetangaza kwamba askari wa Israel waliwabaka na kuwadhalilidha kingono” wanaharakati kadhaa waliokuwepo kwenye msafara huo uliokuwa na misaada ya kibinadamu kwa watu wa Gaza baada ya kukamata meli zao katika maji ya kimataifa karibu ya pwani ya Ugiriki.

Kwa uchache wanaharakati wanne waliripotiwa kufanyiwa ukatili wa kingono na wanajeshi wa Israel.

Meli za msafara huo zilikuwa sehemu ya msafara wa pili wa Global Sumud ambao katika miezi ya karibuni umekuwa ukijaribu kuvunja mzingiro wa Israel kwa kusafirisha misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina huko Gaza. Msafara huo uliondoka katika bandari ya Barcelona, Hispania, tarehe 12 Aprili.

Meli hizo zilikamatwa karibu na rasi ya Peloponnese nchini Ugiriki, mamia ya maili kutoka Gaza.

Katika taarifa yake, msafara wa Sumud umesema wanaharakati 31 walijeruhiwa wakati wa shambulio la vikosi vya Israel.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *