Gazeti la Kiebrania huko Israel limekiri kwamba nguvu ya Iran imethibitishwa katika majibu yake ya hivi karibuni ya makombora dhidi ya utawala wa Israel.

Gazeti la Kiebrania la Yedioth Ahronoth limekiri kwamba Iran ilikuwa na uamuzi wa mwisho na kuonyesha nguvu yake katika kuunda mlinganyo mpya wa nguvu kikanda.

Gazeti hilo linaashiria majibu ya makombora ya Iran kwa ukiukaji wa usitishaji mapigano uliofanywa na utawala wa Israel na uchokozi wake dhidi ya vitongoji vya kusini mwa Beirut huko Lebanon.

Wakati huo huo, kituo cha runinga cha kanali ya 15 cha utawala wa Israel kimeongeza katika ripoti hiyo kwamba duru ya sasa ya mapigano na Iran imemalizika kwa pigo chungu kwa sera ya kujikinga ya Israel.

Katika ripoti yake, kituo cha televisheni cha Kanali ya 12 ya Israel kimeashiria mashambulizi ya makombora ya Iran katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina kujibu uchokozi wa Israel katika vitongoji vya kusini mwa Beirut, na kukiri kwamba Iran imeweza kuunganisha tena pande zote za Muqawama katika medani za vita.

Gazeti la Kizayuni la Israel Hum pia limesisitiza katika ripoti yake kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeanzisha mlingano unaotia wasiwasi kwa kutangaza kwamba shambulio lolote dhidi ya Beirut litajibiwa kwa kipigo cha makombora dhidi ya Israel.

Chanzo cha kijeshi kilichonukuliwa na shirika la habari la Tasnim, kimesema Iran ilitumia mseto wa makombora ya Emad, Qadr F na kizazi kipya cha Kheibar Shekan katika mashambulizi yake ya Jumapili na Jumatatu dhidi ya Israel. Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesema operesheni zote dhidi ya Israel zimetekelezwa kwa mafanikio makubwa.

IRGC imeonya kuwa iwapo Israel itaanzisha mashambulizi mengine, wigo wa kijiografia na kijeshi wa operesheni za kujibu za Iran utapanuliwa kwa kiasi kikubwa, na kwamba malengo yote ya Marekani na Israel katika eneo la Magharibi mwa Asia yanaweza kulengwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *