
Kwa karibu miaka 10, Kundi la wapiganaji wa Kiislamu Al-Shabaab, limekuwa likitishia eneo hili la kaskazini mwa Msumbiji. Likiwa na utajiri wa maliasili, Cabo Delgado inasalia kuwa jimbo maskini zaidi nchini. Utekaji wa utajiri na mamlaka na watendaji wa kigeni, vurugu za vikosi vya usalama, na ufisadi vimeunda mazingira ya kuibuka kwa kundi hilo lenye silaha.
Matangazo ya kibiashara
Mwaka 2017, mjini Namanhumbir, karibu na mji wa Montepuez katika eneo la ndani la Cabo Delgado, msimu wa mvua tayari umeanza wakati maelfu ya wachimbaji wadogo wadogo walipoona kuwasili kwa vikosi vya usalama vya Msumbiji. Walikamatwa kikatili kufuatia kile kilichosekana kuwa ni “uchimbaji haramu.”
Wengi wa hao walioitwa “garimpeiros” hawa (wachimbaji haramu) hawatoki katika eneo hilo. Baadhi hurejea katika wilaya zao za nyumbani au kusini mwa Tanzania. Wengine wanajiunga na kundi la ajabu lenye silaha linalozidi kupata umaarufu katika eneo hilo. “Kuanzia wakati huo, ikawa vita ,” mchimbaji aliliambia Shirika la Kimataifa la Utatuzi wa Migogoro katika ripoti ya 2021.
Unyakuzi wa Utajiri
“Usimamizi wa maliasili na makampuni ya kigeni ni mojawapo ya mada kuu katika hotuba zinazotolewa na Al Shebab,” Joao Feijo, ambaye ni mtafiti katika Kituo cha Kuchunguza Mazingira Vijijini anaeleza.
Miongoni mwa rasilimali hizi ni pamoja na mawe ya thamani, ambayo mlolongo wake uligunduliwa mwaka wa 2009. Cabo Delgado kwa sasa inatoa asilimia Themanini (80%) ya rubi duniani.
Mmoja wa wasimamizi wakuu ni Shirika la Montepuez Rubis Mining (MRM), ambayo ilipata mkataba wa miaka 25 mnamo mwaka wa 2012 eneo linalokadiria kilomita za mraba 10,000.
Kampuni tanzu ya kampuni kubwa ya Uingereza Gemfields Limited (ambayo pia inamiliki Fabergé), MRM pia inamilikiwa kwa 25% na Jenerali Raimundo Pachinuapa, mwanachama wa FRELIMO, chama kilicho madarakani tangu nchi hiyo kuupata uhuru wake mwaka wa 1975.
Mnamo 2019, Gemfields Limited ilikubali kulipa fidia ya yuro milioni 6.7 kwa wachimbaji wa madini badala ya kufuta kesi za kisheria zinazoituhumu kampuni hiyo kwa ukiukaji wa haki za binadamu.
Malalamiko hayo yaliwasilishwa jijini London na kampuni ya sheria ya Leigh Day kwa niaba ya wachimbaji madini haramu 273 wanaofahamika kama garimpeiros.
Kwa mujibu wa Leigh Day, ukatili wa kimwili na kingono, unyanyasaji wa kingono, na mauaji yalifanywa na huduma za usalama za MRM pamoja na vikosi vya usalama vya Msumbiji.
Gemfields walikiri vurugu huko Montepuez, lakini kampuni kubwa ya uchimbaji madini haijawahi kukubali jukumu lolote.
“Mateso, kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria, mauaji… yote yanaendelea,” analalamika Aly Caetano, mratibu wa Kituo cha Maendeleo na Haki za Binadamu (CDD) huko Cabo Delgado. “Wakati huo huo, barabara ya Montepuez-Pemba inabaki kuwa mbaya zaidi katika eneo hilo. Hisia hii ya kuibiwa inachochea usemi wa magaidi.”
Rushwa
Mashirika ya kiraia huko Cabo Delgado pia zinalaani ufisadi wa mamlaka unaoambatana na uporaji wa rasilimali za eneo hilo.
Kwa mfano, kaskazini mwa nchi, kuna Hifadhi ya Asili ya Niassa. Eneo lililolindwa, ambalo pia limekuwa kitovu cha shughuli za Biashara haramu, kama vile usafirishaji wa pembe za ndovu na mbao.
Mnamo Agosti 2020, makontena 82 yaliyopelekwa China yalikamatwa katika bandari ya Pemba na mamlaka ya Msumbiji.
Ndani kulikuwa na magogo ya miti yaliyovunwa kinyume cha sheria. Miezi minne baadaye, makontena haya yalipenya kwa njia ya ajabu kupitia njia za forodha za Msumbiji.
Sitini na sita (66) kati yao zilipatikana zikiwa njiani kuelekea China, kulingana na Shirika la Upelelezi wa Mazingira, Environmental Investigation Agency (EIA).
Ikiwa imetawaliwa sana na makampuni ya Kichina, Sekta ya mbao nchini Msumbiji pia ina uhusiano wa karibu na maslahi ya kiuchumi ya maafisa wa FRELIMO.
Miongoni mwao ni José Pacheco, gavana wa zamani wa Cabo Delgado na Waziri wa Kilimo. Katika uchunguzi kuhusu makampuni ya misitu ya Kichina, EIA ilifichua uhusiano wa kifedha kati ya José Pacheco na mfanyabiashara anayeitwa Liu.
Wanaume hao wawili walikutana mara kadhaa, hasa katika mkutano wa FRELIMO huko Pemba.
Mwaka wa 2016, kulingana na Taasisi ya Rasilimali Duniani, mbao za Msumbiji zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 400 ziliingia katika soko la China. Hata hivyo, forodha za Msumbiji zilitangaza mauzo ya nje ya dola milioni 100 pekee mwaka huo.
Utaratibu Mpya
Cabo Delgado Inayopatikana kwenye umbali wa zaidi ya kilomita 3,000 kutoka Maputo, Mji Mkuu wa Nchi hiyo, ndio eneo masikini zaidi la Msumbiji.
Kulingana na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa, wastani wa mapato kwa kila mtu ni chini ya dola moja kwa siku.
Kutojua kusoma na kuandika kunaathiri asilimia sitini na moja 61% ya idadi ya watu, na asilimia arobaini na tano, 45% ya watoto wanakabiliwa na utapiamlo sugu.
Wapiganaji wa Al Shebab wanataka kuanzisha mafunzo ya dini ya kiisilamu, anaelezea Vasco King wa shirika la haki za binadamu Kundeleya, huko Pemba. “Wanaamini utaratibu wa haki zaidi unahitajika. Wanafaidika na hali ya kijamii iliyoonyeshwa na ukosefu wa ajira na maendeleo duni.”
Shambulio la kwanza la kigaidi lilipiga mji wa pwani wa Mocimboa da Praia mnamo Oktoba 2017.
Vituo kadhaa vya polisi vilishambuliwa kwa wakati mmoja. Karibu watu kumi na watano waliuawa. “Ilikuwa mshtuko mkubwa,” anasema Omar Sufo, mkazi wa Mocimboa da Praia. “Tulijua watu walikuwa wakifanya mazoezi msituni, lakini hakuna mtu aliyefikiria kuwa lilikuwa ni shambulio.”
Katika maeneo ya vijijini, hasira ilikuwa ikiongezeka kwa muda mrefu. Viongozi wa harakati hiyo, kama Maulana Ali Cassimo, walikuwa wakiwafikia wakulima vijana na wachimbaji wa dhahabu hawa garimpeiros. Afisa huyu wa zamani kutoka Wizara ya Kilimo alisafiri vijijini kwa pikipiki yake kufanya kampeini ya kulaani kufukuzwa kwa watu, ukatili wa polisi, na udhibiti wa mamlaka ya Maputo juu ya rasilimali za Cabo Delgado.
Dola la Kiislamu
Mnamo 2019, kundi la Al Shabab nchini Msumbiji liliahidi utii kwa shirika linalofahamika kama Dola la kiisilamu, Islamic State. Katika toleo la Julai 2020, gazeti la propaganda la kundi la kigaidi, Al Naba, lilichapisha kichwa cha habari “Wapiganaji wa vita, jihadharini na uwekezaji wenu nchini Msumbiji.”
Ajenda ya ISIS iko wazi: kuwafukuza wanauchumi wa kigeni kutoka Cabo Delgado. Lengo lao: unyonyaji wa uwanja mkubwa zaidi unaozalisha gesi duniani, kwenye pwani ya Palma.
Uwanja huo una akiba ya mita za ujazo bilioni 5, ambayo Total na washirika wengine wamepewa idhini hiyo. Baada ya miaka ya kusimamishwa kwa shughuli zao, kampuni kubwa ya mafuta na gesi ya Ufaransa ilitangaza kuanza tena kwa mradi huo mwaka huu.
Leo, ni vigumu kukadiria idadi ya wapiganaji wanaounda kundi la Shebab. Mnamo 2025, Kituo cha Kitaifa cha Kupambana na Ugaidi cha Marekani kilikadiria 300.
Kundi la Kimataifa la ufuatiliaji wa Mgogoro lilihesabu 3,000 mnamo 2020. Wakati huo huo, mgogoro huo umesababisha karibu watu 800,000 kutoroka makazi yao kulingana na Umoja wa Mataifa.