
Rais wa Colombia, Gustavo Petro, ameikosoa Marekani kuhusu “ufashisti ulioenea katika Ikulu ya White House” huku mvutano ukiongezeka kati ya Bogota na Washington.
“Ufashisti katika Ikulu ya White House unapofusha akili na kuchochea ongezeko la watu wasio na akili duniani kote,” Petro ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Rais wa Colombia pia ameikosoa serikali ya Marekani kwa kutuma silaha kwa tawala zinazopigana, na kutoa “fedha na makombora kwa ukatili na ushenzi kama njia ya kudhibiti wengine.”
Matamshi hayo yamekuja baada ya Petro kuwekwa kwenye orodha ya vikwazo vya Ofisi ya Marekani ya Kudhibiti Mali za Kigeni (OFAC).
“Kuingizwa jina langu na wanafamilia wangu kwenye orodha ya OFAC ni jaribio la kunishinikiza na kunilazimisha nikubali matakwa (ya Marekani),” ameandika Rais Petro kwenye mtandao wa X na kuongeza: “Colombia ni nchi huru na si koloni la nchi yoyote.”
Rais huyo wa Colombia amepinga mashinikizo ya Marekani, akisema Washington inajaribu kumnyamazisha.
“Nimewekwa kwenye orodha ya OFAC kwa sababu ya nilichokisema New York,” aliwaambia waandishi wa habari huko Washington mnamo Februari 2026. “Kama kungekuwa na ushahidi wa kisheria, nisingezungumza hapa.”
“Hizi ni jitihada za kujaribu kuninyamazisha na kunilazimisha kumtii Rais wa Marekani Donald Trump,” alisema na kuongeza: “Colombia haitambui wafalme wala magavana na haitanyamazishwa. Uhuru wa kujieleza ndio kiini cha uhuru, na ukimya ni aina ya utumwa.”
Amesema: “Watu wa Colombia wana roho ya ujasiri wa mtu binafsi na upendo mkubwa wa uhuru”.
Kuhusu mauaji ya kimbari yanayofanywa na wanajeshi wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi katika Ukanda wa Gaza, Rais Gustavo Petro ameilaani tena Marekani na nchi za Ulaya kwa kuunga mkono vita vya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.