
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov amekosoa utendaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, akisisitiza haja ya kutekelezwa kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa “bila kubagua”.
Lavrov amesema kwamba Katibu Mkuu wa sasa wa UN hafuati mbinu hii na anashirikiana waziwazi na nchi za Magharibi, hasa kuhusu suala la Ukraine.
Kuhusu suala la Russia na Marekani, Lavrov amesema kwamba Marekani haionyeshi nia yoyote ya kurudi kwenye makubaliano yaliyofikiwa Anchorage, akimaanisha mazungumzo yaliyowakutanisha maafisa kutoka nchi hizo mbili kwa lengo la kushughulikia masuala yenye utata na kufungua tena njia za mawasiliano kati ya Moscow na Washington.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameongeza kuwa biashara ya kimataifa iko chini ya mashinikizo “haramu” ya Magharibi kupitia vikwazo na hatua za kiuchumi za upande mmoja, akisema kwamba hali hii inadhihirisha zaidi haja ya kujenga mifumo ya kifedha na kibiashara inayotegemewa zaidi ambayo haitegemei ushawishi wa nchi za Magharibi.
Matamshi ya Lavrov yanakuja huku kukiwa na mvutano unaoendelea kati ya Russia na Magharibi kuhusu vita nchini Ukraine, upanuzi wa vikwazo vya Magharibi dhidi ya Moscow, na juhudi za kundi la nchi kadhaa za kukuza mifumo mbadala ya kifedha na kibiashara ambayo itapunguza utegemezi kwa mifumo inayotawaliwa na Marekani na washirika wake.