
Mlipuko huo, ambao pia umeenea hadi nchini jirani ya Uganda, unasababishwa na aina adimu na hatari ya virusi vya Ebola inayojulikana kama Bundibugyo.
Mkurugenzi wa Operesheni za Tahadhari na Hatua za Dharura za Afya wa WHO, Dkt. Abdirahman Mahamud, amesema kuwa hadi tarehe 8 Juni, DRC ilikuwa imerekodi wagonjwa 550 waliothibitishwa wa Ebola na vifo 101.
“Habari njema ni kwamba hadi sasa tuna wagonjwa 19 ambao wamepona, hivyo utambuzi wa mapema na matibabu vinaokoa maisha,” amesema Dkt. Mahamud alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva kwa njia ya video.
Kuongezeka kwa vipimo kumeongeza utambuzi wa wagonjwa
Akizungumza kutoka Bunia katika Jimbo la Ituri, kitovu cha mlipuko huo ambako kunapatikana asilimia 94 ya wagonjwa wote nchini humo, Dkt. Mahamud amesema ongezeko la wagonjwa waliothibitishwa linatokana na kupanuliwa wigo kwa huduma za upimaji.
“Kuongezeka kwa wagonjwa waliothibitishwa kunatokana na kuongezwa kwa kiwango cha upimaji,” amesema.
Maabara mpya zilizogatuliwa zimeanzishwa ili kuharakisha uchunguzi wa sampuli zinazoshukiwa kuwa za Ebola, ikiwemo maabara inayofanya kazi kikamilifu mjini Mongbwalu.
WHO imesema hatua hiyo inasaidia kubaini maambukizi mapema na kuanza matibabu kwa haraka zaidi.
Uganda bado haijaripoti maambukizi katika jamii
Nchini Uganda, mamlaka za afya zimeripoti wagonjwa 19 waliothibitishwa wa Ebola, vikiwemo vifo viwili, pamoja na mgonjwa mmoja alishukiwa kuwa na Ebola ambaye sasa amefariki dunia.
WHO imesisitiza kuwa hadi sasa hakuna ushahidi wa maambukizi ya ugonjwa huo ndani ya jamii nchini Uganda.
Hadi tarehe 6 Juni, mamlaka za afya nchini DRC zilikuwa zimewatambua watu 5,040 waliokutana au kuwasiliana na wagonjwa wa Ebola katika majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
Kupitia kampeni kubwa ya ufuatiliaji, wahudumu wa afya wamefanikiwa kuwafikia asilimia 62 ya watu hao.
“Tunatarajia kufikia lengo la asilimia 90 hadi 95 katika wiki zijazo,” amesema Dkt. Mahamud.
Ameeleza kuwa maendeleo yanayopatikana ni ya “taratibu lakini thabiti”, yakijengwa juu ya kuimarisha uhusiano wa kuaminiana kati ya wahudumu wa afya na jamii.
Wahudumu wa afya wa ndani ni mhimili muhimu
WHO imesisitiza kuwa wahudumu wa afya wa ndani wana mchango mkubwa katika kubaini wagonjwa mapema na kuwapeleka kwenye vituo vya matibabu.
“Tuna mfumo unaofanya kazi vizuri na uliounganishwa kuanzia ufuatiliaji wa ugonjwa, ufuatiliaji wa waliokutana na wagonjwa, vituo vya matibabu hadi maabara,” amesema Dkt. Mahamud, akiongeza kuwa ushirikiano wa taarifa umeimarisha hatua za mlipuko huo.
Pamoja na mafanikio hayo, juhudi za kudhibiti Ebola bado zinakabiliwa na changamoto kubwa katika maeneo ya mbali yenye miundombinu duni na mawasiliano hafifu.
“Katika baadhi ya maeneo, sampuli za wagonjwa huchukua hadi saa nane kufikishwa maabara.Ituri ni kubwa kama Ufaransa,” amesema Dkt. Mahamud.
Amefafanua kuwa wagonjwa walioko Bunia wanaweza kupata majibu ya vipimo ndani ya saa moja au mbili, lakini wale walioko maeneo ya mbali zaidi wanaweza kusubiri hadi saa 24.
Katika hatua ya kuleta huduma karibu zaidi na wananchi, maabara mpya inatarajiwa kuanza kazi ifikapo Ijumaa mjini Aru, karibu na mpaka wa Uganda, ambako kwa sasa sampuli husafirishwa kwa zaidi ya saa 10 kwa njia ya barabara ili kufanyiwa uchunguzi.
WHO yaongeza msaada katika maeneo yaliyoathirika
WHO imesema imeanzisha maabara tano za muda katika maeneo yaliyoathirika ili kuwezesha upimaji kufanyika karibu na kitovu cha mlipuko.
Kwa kushirikiana na washirika wake na kuunga mkono juhudi zinazoongozwa na serikali ya DRC, shirika hilo la Umoja wa Mataifa limepeleka zaidi ya wataalamu 100 nchini humo, kusafirisha tani 40 za vifaa tiba na vifaa vya kinga, pamoja na kusaidia kuanzisha vituo vya matibabu ya Ebola.
WHO imeeleza kuwa mchanganyiko wa upimaji wa haraka, ushirikishwaji wa jamii na ufuatiliaji madhubuti ndio unaotoa matumaini makubwa ya kudhibiti mlipuko huo kabla haujasambaa zaidi katika eneo la Maziwa Makuu barani Afrika.