
Katika Kituo cha Afya cha Moungali mjini Brazzaville, wazazi huleta watoto wao kupata chanjo muhimu huku wakipatiwa elimu kuhusu afya ya mama na mtoto.
Mohamed, aliyemleta mtoto wake wa siku kumi aitwaye Petito kupata chanjo za polio na kifua kikuu, amesema, “Tunataka apate chanjo zake zote kwa wakati.”
Muuguzi Gisèle Manguitoukoulou alisema: “Jukumu letu haliishii kutoa chanjo. Tunawasikiliza wazazi, tunawahakikishia usalama wa watoto wao na kuwasaidia kuelewa umuhimu wa kila miadi ya chanjo.”
Kiwango cha chanjo kimeongezeka
Kwa mujibu wa WHO, kati ya Januari na Aprili 2026, kiwango cha chanjo ya kwanza ya surua na rubela kiliongezeka kutoka asilimia 85 hadi 94.4, huku dozi ya tatu ya chanjo ya polio ya kunywa ikiongezeka kutoka asilimia 82.4 hadi 92.3.
Mshauri wa Chanjo wa WHO nchini humo, Dkt. Angelie Serge Patrick Dzabatou-Babeaux, amesema, “Chanjo hulinda watu katika kila hatua ya maisha.” Naye Mkurugenzi wa EPI, Profesa Jile Florient Mimiesse, alisisitiza kuwa kila dozi inayotolewa huchangia kuimarisha kinga ya jamii.
Miongoni mwa wanufaika ni Love, aliyepokea dozi yake ya mwisho ya chanjo dhidi ya dondakoo au diphtheria na pepopunda. Ameongeza kuwa“Chanjo si kwa watoto pekee. Katika kila umri ni muhimu kujilinda na kuhakikisha chanjo zako ziko sahihi.”