Katika taarifa iliyotolewa mjini Nairobi Kenya Mkurugenzi wa Kanda wa UNICEF kwa Afrika Mashariki na Kusini, Etleva Kadilli, amesisitiza kuwa elimu lazima ibaki kuwa haki inayopatikana kwa watoto wote, wakiwemo wale wanaoishi katika maeneo ya migogoro, kambi za wakimbizi wa ndani, na nchi zinazowahifadhi wakimbizi wa Sudan.

“Watoto kote Sudan wana haki ya msingi ya kupata elimu na wanapaswa kuwa na uwezo wa kufanya mitihani ya taifa kwa usalama na kwa haki bila kujali walipo,” amesisitiza Kadilli.

Miaka ya kuvurugika kwa elimu

Wito huo unakuja wakati mzozo unaoendelea nchini Sudan ukiendelea kuvuruga elimu ya mamilioni ya watoto.

Kwa mujibu wa UNICEF, mamia ya maelfu ya wanafunzi wameshindwa kukamilisha mitihani yao katika miaka ya hivi karibuni kutokana na ukosefu wa usalama na kufurushwa katika makazi yao.

Kadilli amesema kuwa kwa wanafunzi wengi, kupata nafasi ya kufanya mtihani mmoja wa taifa ni hatua muhimu ya kurejesha safari yao ya elimu.

Ameongeza kuwa “Katika mazingira ya sasa, wanafunzi wengi wamepitia miaka ya kuvurugika kwa masomo, huku mamia ya maelfu wakishindwa kukamilisha mitihani yao kutokana na mzozo. Kwa wanafunzi hawa, kufanya mtihani mmoja wa taifa ni fursa iliyosubiriwa kwa muda mrefu ya kusonga mbele kwa usawa na wenzao.”

Mitihani ya pamoja ni muhimu kwa haki na usawa

UNICEF imesisitiza kuwa mfumo mmoja wa mitihani unaotambuliwa kitaifa ni muhimu katika kuhakikisha usawa na kulinda thamani ya vyeti vya wanafunzi.

“Ni muhimu watoto wote iwe wako katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro, maeneo ya watu waliokimbia makazi yao, au maeneo yenye utulivu zaidi wapate mitihani ile ile inayotambuliwa kitaifa,” amesema Kadilli.

Ameonya kuwa mifumo iliyogawanyika ya utoaji vyeti inaweza kuunda vikwazo vya muda mrefu kwa vijana wanaotafuta elimu ya juu na ajira.

“Kwa kizazi cha vijana ambao elimu yao tayari imeathiriwa vibaya na mzozo, vyeti vinavyotambuliwa ni msingi wa kuendelea na masomo, kupata ajira, na kuchangia katika ujenzi wa Sudan,” amesema akiongeza kuwa “Mifumo iliyogawanyika ya vyeti inaweza kuunda vikwazo vitakavyodumu hata baada ya mzozo kumalizika.”

Wito wa uendeshaji salama na sawia wa mitihani

UNICEF imezitaka serikali ya Sudan na pande zote katika mzozo kukubaliana juu ya hatua za vitendo zitakazowezesha mitihani kusimamiwa kwa usalama na kwa namna inayofanana kote nchini pamoja na katika nchi zinazowahifadhi wakimbizi wa Sudan.

“Kwa msimu huu wa mitihani na hata baada yake, ni muhimu kuhakikisha mitihani ile ile inayotambuliwa kitaifa inapatikana kote Sudan na katika nchi zinazowahifadhi wakimbizi wa Sudan,” amesema Kadilli. “UNICEF iko tayari kusaidia juhudi hizi.”

Shirika hilo pia limesisitiza kuwa elimu inapaswa kubaki eneo lisiloegemea upande wowote na lisilotumiwa kugawanya jamii.

“Elimu lazima ibaki kuwa eneo lisilo na upendeleo. Inapaswa kulindwa dhidi ya migawanyiko na kuongozwa na maslahi bora ya watoto.” 

Amemalizia kwa kusisitiza kuwa kuhakikisha wanafunzi wote wa Sudan wanafanya mtihani mmoja wa taifa, popote walipo, ni jambo muhimu katika kulinda haki zao na mustakabali wao.

“Kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wa Sudan wanaweza kufanya mtihani ule ule, bila kujali walipo, ni muhimu katika kulinda haki zao leo na fursa zao za baadaye.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *