Dodoma. Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani nchini, Zanini Athumani, amesema wafanyakazi wa majumbani nchini bado wanakabiliwa na changamoto kubwa zinazohitaji hatua za haraka za kisheria, kisera na kijamii ili kuhakikisha wanapata haki zao kama wafanyakazi wengine.
Zanini amesema hayo leo, Juni 10, 2026, kwenye mkutano wa wadau wa sekta mbalimbali wa kazi zenye staha, uliolenga kuweka mikakati ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa kazi za majumbani 2025/26–2029/30, uliofanyika jijini Dodoma.
Amesema wafanyakazi hao hufanya kazi kwa muda mrefu bila mapumziko ya kutosha, huku baadhi yao wakilipwa mishahara midogo au kucheleweshwa malipo, jambo linaloathiri maisha yao ya kila siku.
“Baadhi ya waajiri bado hawazingatii viwango vya chini vya mshahara. Wafanyakazi hulipwa kidogo, kwa kuchelewa au bila utaratibu rasmi wa mikataba,” amesema Zanini.
Ameongeza kuwa changamoto nyingine ni mawakala wa ajira wasiosajiliwa wanaowanyonya wafanyakazi kwa kukata mishahara yao au kuwaingiza katika ajira zisizo na ulinzi wa kisheria, hali inayowafanya wengi kukosa msaada wanapokumbana na matatizo.
Mmoja wa wafanyakazi wa majumbani akiwa kwenye mkutano wa kujadili haki na maslahi yao Jijini Dodoma leo Juni 10, 2026. Picha na Rachel Chibwete
Kwa upande wake, mwakilishi mkazi wa shirika lisilo la kiserikali la kutetea maslahi ya wafanyakazi wa majumbani (CVM), Laura Vallesi, amesema mkutano huo unalenga kuthibitisha upya dhamira ya kulinda wanawake na wasichana wanaokumbwa na unyonyaji na ukatili katika sekta ya ajira za ndani.
“Tuko hapa kwa ajili ya wanawake na wasichana wanaofanyishwa kazi bila ulinzi, wale wasiokuwa na mazingira bora ya kazi, na watoto wanaosafirishwa kutoka vijijini na kuingizwa kwenye kazi ngumu bila elimu wala usalama,” amesema.
Ameongeza kuwa suluhisho la changamoto hizo linahitaji ushirikiano kati ya Serikali na wadau wote katika kujenga mfumo imara wa kazi zenye staha, sambamba na kuunga mkono utekelezaji wa Mkataba wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Na. 189.
Amesema kazi za ndani ni muhimu kwa jamii, lakini zimekuwa zikihusisha baadhi ya matukio ya unyonyaji, hususan kwa watoto wanaoahidiwa elimu kisha kulazimishwa kufanya kazi ngumu.
Amesema licha ya kuwepo kwa sheria za kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu, bado kuna haja ya kuongeza uelewa wa jamii, kuimarisha mifumo ya ulinzi na kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua.
Wadau wa wafanyakazi wa majumbani wakiwa kwenye mkutano wa kujadili haki na maslahi ya wafanyakazi hao Jijini Dodoma leo Juni 10, 2026
Meneja wa miradi wa shirika la Wote Sawa, Jackline Mujunangoma, amesema usafirishaji haramu wa binadamu bado ni tishio kubwa kwa wanawake na wasichana, ambapo wengi hupoteza haki zao za msingi, ikiwemo elimu na usalama.
Amesema kupitia miradi mbalimbali, mashirika ya kiraia yanashirikiana kuwawezesha waathirika kurejea shuleni, kupata stadi za maisha na kuanza upya maisha yao kwa heshima na usalama.
Katibu Mkuu wa Chodawu, Said Wamba, amesema juhudi za muda mrefu za wadau zimeanza kuleta matokeo chanya, lakini bado changamoto kubwa ni kuridhia Mkataba wa ILO Na. 189 kuhusu kazi zenye staha kwa wafanyakazi wa majumbani.
“Tumeendelea kuishawishi Serikali kuridhia mkataba huu kwa miaka mingi. Tunaamini utekelezaji wake utaimarisha ulinzi wa haki za wafanyakazi wa majumbani,” amesema.
Ameongeza kuwa elimu kwa wafanyakazi na ushirikiano na vyuo vya ufundi umesaidia kuboresha ujuzi na hali ya kazi kwa kundi hilo.
Wamba amehimiza ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi na mashirika ya kiraia katika kupambana na unyonyaji, ukatili na ajira za watoto, huku wakisisitiza kuwa mustakabali bora wa wafanyakazi wa majumbani unategemea hatua za pamoja na utekelezaji wa sheria zilizopo.