Mbeya. Wasomi mkoani Mbeya wamehimizwa kuwa mstari wa mbele kueleza na kutangaza maendeleo yaliyofikiwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, badala ya kuzingatia wanaobeza juhudi za Serikali ya awamu ya sita.

Wito huo umetolewa leo Juni 10, 2026, katika kongamano la Shirikisho la Wasomi Mkoa wa Mbeya lililowakutanisha wataalamu kutoka sekta mbalimbali ikiwamo afya, elimu, miundombinu na huduma za jamii.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Ndele Mwaselela, amesema Rais Samia ameleta maboresho makubwa katika sekta za afya, elimu na miundombinu, hivyo mafanikio hayo yanapaswa kutangazwa.

“Tunashuhudia ujenzi wa vituo vya afya, zahanati, hospitali, shule na barabara. Haya ni maendeleo yanayoonekana, hivyo wasomi wanapaswa kuyaeleza kwa wananchi,” amesema.

Washiriki wa kongamano la shirikisho la wasomi mkoani Mbeya.

Mwaselela pia amewataka wasomi kuendelea kulinda amani ya nchi akisema ndiyo msingi wa maendeleo na ustawi wa jamii.

Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Mbeya, Ally Simba, amesema uwekezaji wa Serikali umechangia kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi hadi zaidi ya asilimia 90 katika madarasa ya mitihani. Amesema mkoa huo hupokea zaidi ya Sh1.7 bilioni kila mwezi kwa shughuli za elimu na unaendelea kutekeleza mikakati ya kuboresha ufundishaji na mazingira ya kujifunzia.

Kwa upande wa miundombinu, Katibu Tawala Msaidizi wa Miundombinu, Mhandisi Rashid Mtamila, amesema huduma ya maji imeongezeka kutoka asilimia 51 hadi 90 kutokana na kuimarika kwa uzalishaji wa maji. Ametaja mradi wa maji wa Mto Kiwira na mradi wa maji wa miji 28 kuwa miongoni mwa miradi inayotarajiwa kuondoa changamoto ya maji kwa wananchi.

Amesema pia ujenzi wa barabara ya njia nne unaendelea na utasaidia kupunguza msongamano wa magari pamoja na kuchochea shughuli za maendeleo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amesema mkoa huo umepokea fedha nyingi za miradi ya maendeleo, jambo linalostahili kuthaminiwa.

Meya wa Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa, amesema jiji limevuka malengo ya ukusanyaji mapato na linaendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya barabara na huduma za wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *