ILIPOISHIA

“Hizo taarifa tayari zimesambazwa katika vituo vyote vya polisi. Alama yetu ilikuwa ni namba ya usajili ya hilo gari kwani alipofika hapo gesti, watu waliona namba ya gari alilokuwa nalo. Kwa hiyo ilipotokea hii ajali, polisi walipofika wakaona namba ya usajili ya gari hilo ndiyo namba ya gari ya huyo mtu aliyefanya mauaji”

“Haiwezekani. Dereva wangu si jambazi. Inawezekana mmekosea kusoma namba”

“Kuna kachero aliyekwenda katika hiyo gesti kufanya uchunguzi na kupata ukweli. Kwa hiyo hadi kesho asubuhi ukweli utakuwa umefahamika””

SASA ENDELEA…

“Sasa itakuwaje?”

“Wewe unaruhusiwa kuondoka, uje kesho saa mbili asubuhi. Kijana wako tutabaki naye.”

Ilibidi Wakwetu amweleze James maneno ya matumaini ili aridhike kuwekwa ndani hadi kesho yake kwa vile alikuwa na imani kwamba polisi wamejichanganya.

James akawekwa ndani na Wakwetu akarudi nyumbani. Alimweleza mke wake habari waliyoipata huko polisi na wote waliamini kwamba polisi walikuwa wamejichanganya.

“Naamini hadi kesho ukweli utafahamika na James anaweza kuachiwa,” Wakwetu alimwambia mke wake.

Usiku ule Majaliwa hakurudi nyumbani. Wakwetu na mke wake walilala kwa wasiwasi mkubwa.

Hawakujua Majaliwa alikuwa amekwenda wapi na alilala wapi. Kulipokucha asubuhi Wakwetu alijaribu kumpigia simu Majaliwa lakini simu yake ilikuwa bado haipatikani.

“Simu yake haipatikani hadi sasa,” Wakwetu alimwambia mke wake wakiwa chumbani.

Sharifa akatikisa kichwa kwa kusikitika.

“Upuuzi wake mwingine ni huo wa kuzima simu, hatuwezi kujua yuko wapi,” Sharifa alisema.

“Anajua akija hapa anaweza kukamatwa na polisi kutokana na mambo aliyoyafanya.”

“Angekuja tu kutueleza nini kimetokea au angeacha simu yake ikiwa wazi. Anapozima simu anazidi kututia wasiwasi.”

“Akili za kitoto. Anadhani kwa kufanya hivyo ndiyo atasalimika. Lengo lake ni kunitia mimi kwenye matatizo.”

“Nyote mtanusurika, Inshaallah.”

Wakwetu baada ya kuoga na kuvaa alimuaga mke wake na kutoka. Saa mbili kamili akawa kwenye kituo cha polisi.

Muda huo polisi wa kituo hicho walikuwa na taarifa kamili ya tukio lililotokea Mabawa usiku uliopita.

Inspekta Amour aliyekuwa amekabidhiwa jalada la uchunguzi wa tukio hilo alikuwa amefika katika gesti ya Mabawa dakika chache baada ya tukio hilo.

Alipofika alikuta mtu aliyepigwa risasi ameshakimbizwa hospitalini.

“Tukio limetokeaje?” Inspekta Amour alimuuliza mtumishi mmoja wa gesti hiyo aliyekuwa akihusika na utoaji wa vyumba.

“Jana majira ya saa mbili usiku alifika kijana mmoja akamuulizia mteja wetu mmoja tuliyekuwa tumempa chumba namba saba,” mtumishi huyo alimweleza Inspekta Amour.

“Alimuulizaje?”

“Alitutajia jina lake akatuambia anamuhitaji.”

“Huyo mteja wenu aliandikisha jina gani?”

“Masumbuko Abdallah.”

“Kwa hiyo huyo mtu alikuja kumuulizia Masumbuko Abdallah?”

“Ndiyo.”

“Wewe ulimjibu nini?”

“Nilimwambia yuko chumba namba saba. Nilidhani kuwa ni watu wanaojuana.”

“Huyo mtu alikutajia jina lake?”

“Sikumuuliza jina lake.”

“Enhe, ulipomwambia Masumbuko yuko chumba namba saba, alikwenda?”

“Ndiyo alikwenda. Akabisha mlango na kuingia ndani. Sisi tulikuwa tunaendelea na shughuli zetu.”

“Nini kilitokea baada ya hapo?”

“Baada ya muda kidogo tulisikia mlio wa risasi ukitokea mle chumbani. Hapo hapo tukamwona yule kijana anatoka…”

“Subiri. Wakati anatoka alikuwa ameshika nini?”

“Hakuwa ameshika kitu chochote.”

“Hakuwa ameshika bastola au kitu kingine?”

“Hakuwa ameshika kitu.”

“Alipotoka mlimuuliza chochote?”

“Hatukuwahi kumuuliza chochote. Alitoka haraka haraka, akajipakia kwenye gari lake na kuondoka kwa kasi ili asije akakamatwa.”

“Mlikariri namba ya usajili ya hilo gari pamoja na kujua aina yake?”

“Ndiyo.”

Mtumishi huyo alitaja aina ya gari la Wakwetu pamoja na namba yake ya usajili.

“Sawa. Mlikwenda kuangalia katika hicho chumba?”

“Ndiyo tulikwenda.”

“Mlikuta nini?”

“Tulikuta yule mteja wetu amelala chini, damu ikimtoka tumboni. Tukamuuliza nini kimetokea lakini alikuwa kimya. Tukapiga simu polisi. Polisi wakafika, tukawaeleza kilichotokea, wakamchukua yule mtu na kumpeleka hospitalini.”

“Mteja wenu huyo alifika lini katika gesti hii?”

“Mpaka jana alikuwa na siku tatu.”

“Nataka unionyeshe jina lake katika kitabu chenu cha wageni.”

Mtumishi huyo alifanya hivyo.

“Jina lake hili hapa.”

Amour aliliona kwenye kitabu.

“Sawa. Huyo mtu aliyekuja hapa kumuulizia Masumbuko ukimkadiria ana umri gani?”

“Bado ni kijana sana. Hafikishi hata miaka thelathini.”

Inspekta Amour akashusha pumzi ndefu.

“Nataka kukiona hicho chumba namba saba,” akamwambia mtumishi huyo wa gesti.

Amour alipelekwa katika chumba hicho. Alikuta damu iliyoganda kwenye sakafu. Chumba kilikuwa hakijasafishwa.

“Masumbuko aliangukia wapi?” Amour akamuuliza.

“Hapo kwenye damu.”

“Kichwa chake kilikuwa upande gani?”

“Kilikuwa upande huu wa mlango.”

“Alikuwa amelala vipi?”

“Tulimkuta amelala chali.”

“Sawa. Nataka kukuuliza, baada ya tukio hili mligundua kama mteja wenu ameporwa pesa au kitu chochote?”

“Hatujui.”

“Asante sana. Ningependa kujua jina lako. Unaitwa nani?”

“Naitwa Hashim.”

“Hashim nani?”

“Hashim Seki.”

Inspekta Amour hakuishia hapo. Alikwenda katika Hospitali ya Bombo alikopelekwa Masumbuko Abdallah aliyekuwa amepigwa risasi.

Alimkuta katika chumba cha mahututi.

Daktari aliyempeleka katika chumba hicho alimwambia kuwa Masumbuko alikuwa ametolewa risasi tumboni lakini hali yake ilikuwa mbaya.

“Tuliambiwa kuwa ameshakufa,” Inspekta Amour akasema.

“Amepoteza fahamu lakini bado anapumua. Labda ujaribu kuja kesho uone hali yake inaendeleaje.”

“Ninahitaji ile risasi mliyoitoa tumboni mwake.”

“Ni risasi ndogo ya bastola ambayo imemchana utumbo. Ngoja nikupatie.”

“Sawa.”

Inspekta Amour alipopatiwa risasi hiyo, ambayo iliwekwa ndani ya pakiti ya nailoni, aliaga na kuondoka nayo.

Asubuhi ile Wakwetu alipowasili kwenye kituo hicho cha polisi alielezwa mkasa mzima uliotokea.

“Kijana wako hatutamwachia. Upelelezi wetu ukikamilika tutamfikisha mahakamani,” mkuu wa kituo hicho cha polisi alimwambia Wakwetu na kuongeza:

“Hivi sasa madaktari wanafanya jitihada za kuokoa maisha ya yule kijana aliyepigwa risasi na kama atakufa kijana wako atafunguliwa mashtaka ya mauaji.”

“Kwani huyo kijana aliyepigwa risasi yuko hai?” Wakwetu akauliza. Alichokuwa akikifahamu yeye ni kuwa kijana huyo alikuwa amekufa.

“Yuko hai lakini hasemi wala hatikisiki, yuko chumba cha mahututi.”

“Nitahakikisha ninamsaidia kwa gharama yoyote ili apone.”

“Ni sawa. Lakini bado kijana wako tutamfungulia mashtaka. Kama si ya mauaji, ni ya jaribio la kuua na kujeruhi kwa risasi.”

Akiwa hapo kwenye kituo Wakwetu alimshuhudia James akitolewa akiwa ametiwa pingu akipelekwa nyumbani kwake kupekuliwa. Polisi walikuwa wanaitafuta bastola ambayo waliamini alikuwa nayo nyumbani.

“Baba, nimepatwa na kesi nyingine ya mauaji,” James akamwambia Wakwetu.

“Nitapambana kwa nguvu zote kuhakikisha ninakusaidia,” Wakwetu akamwambia James mbele ya polisi.

James alitolewa nje ya kituo. Uso wake ulikuwa umefadhaika. Alipakiwa kwenye gari la polisi. Gari hilo likaondoka.

Wakwetu aliomba apelekwe Hospitali ya Bombo ili akamwone kijana aliyedaiwa kushambuliwa kwa risasi.

Wakati huo Inspekta Amour alikuwa pale kituoni. Alikuwa akijiandaa kwenda hospitalini kumjulia hali Masumbuko.

Akatakiwa aende na Wakwetu ili aweze kumwona kijana huyo.

Wakwetu akapakiwa kwenye gari. Yeye na Amour wakaelekea hospitalini.

“Jana usiku nilikwenda kumwona. Kusema kweli hali yake ilikuwa mbaya,” Amour alimwambia Wakwetu aliyeketi kwenye siti iliyokuwa kando yake.

“Tuombee tumkute mzima. Mimi niko tayari kugharamia matibabu yake hata kama atapelekwa nje ya nchi.”

“Unadhani ni kwa nini dereva wako alimshambulia yule kijana?”

“Sijui. Na mpaka sasa sina hakika kwamba ni yeye aliyefanya kitendo hicho.”

“Watumishi wa gesti walimwona na gari alilotumia walilikariri namba zake.”

“Mlipomhoji dereva wangu alisema nini?”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *