Dar es Salaam. Katika kipindi ambacho mashirika mengi yasiyo ya kiserikali (NGOs) duniani yanakabiliwa na changamoto ya kupungua kwa misaada kutoka kwa wahisani wa kimataifa, Tanzania imeanza kuchukua hatua za kutafakari mustakabali wa sekta hiyo kwa kuhamasisha matumizi ya rasilimali za ndani kama msingi wa uendelevu wake.

Mjadala huo unatarajiwa kuwa kiini cha Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) 2026 litakalofanyika Oktoba 20 hadi 22, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Jukwaa hilo linaandaliwa na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, likibeba kaulimbiu isemayo, “Fikra Mpya kuhusu Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali: Ubunifu, Ubia na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha kupitia Vyanzo vya Ndani.”

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Ijumaa, Juni 12, 2026, kuhusu maandalizi ya jukwaa hilo, Mwenyekiti wa NaCoNGO, Jasper Makala, amesema kaulimbiu ya mwaka huu imechaguliwa kwa kuzingatia mabadiliko yanayoendelea kushuhudiwa katika sekta ya maendeleo duniani.

“Kwa muda mrefu mashirika mengi yamekuwa yakitegemea kwa kiwango kikubwa fedha kutoka kwa wahisani wa nje. Hata hivyo, mazingira hayo yanabadilika kwa kasi, hivyo ni muhimu sasa kujenga uwezo wa mashirika kuibua na kusimamia rasilimali kutoka ndani ya nchi ili kuhakikisha huduma kwa wananchi zinaendelea bila kuyumba,” amesema Makala.

Kwa mujibu wa wadau wa sekta ya maendeleo, kupungua kwa misaada katika baadhi ya maeneo duniani kumechangiwa na mabadiliko ya vipaumbele vya nchi wahisani, changamoto za kiuchumi pamoja na migogoro ya kimataifa inayozifanya nchi nyingi kuelekeza fedha katika mahitaji yao ya ndani.

Kutokana na hali hiyo, mashirika yasiyo ya kiserikali nchini yanaanza kuangalia kwa karibu fursa zilizopo ndani ya Tanzania, ikiwemo ushirikiano na sekta binafsi, matumizi ya teknolojia katika uchangishaji wa fedha, pamoja na kuanzisha miradi ya kijamii yenye uwezo wa kuzalisha mapato.

Makala amesema moja ya malengo makuu ya jukwaa hilo ni kujenga mjadala wa kitaifa kuhusu namna ya kuifanya sekta ya NGOs kuwa imara zaidi na isiyoyumbishwa na mabadiliko ya ufadhili wa nje.

“Tunataka kuona mashirika yanakuwa na fikra mpya za uendelevu. Hii ni pamoja na ubunifu katika kupata rasilimali, kujenga ubia wa kimkakati na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji ambayo itaongeza imani kwa wadau wa ndani na nje,” amesisitiza.

Jukwaa hilo linatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya washiriki 3,000 kutoka Tanzania na nchi mbalimbali za Afrika Mashariki, wakiwemo viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, wawakilishi wa Serikali, sekta binafsi, taasisi za utafiti, washirika wa maendeleo na vyombo vya habari.

Mbali na kujadili changamoto za ufadhili, washiriki watajadili mchango wa mashirika katika maendeleo ya Taifa na namna ya kuimarisha ushiriki wao katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kama ilivyo utaratibu, Jukwaa la Taifa litatanguliwa na majukwaa ya ngazi ya wilaya yatakayofanyika Juni na Julai 2026 pamoja na majukwaa ya mikoa yatakayofanyika Agosti na Septemba 2026. Majukwaa hayo yatakusanya maoni, changamoto na mapendekezo yatakayowasilishwa katika jukwaa kuu la kitaifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *