Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa (UNHCR) imetangaza kwamba idadi ya watu waliolazimika kuhama makwao duniani kote ilipungua mwaka wa 2025, ikiwa ni mara ya kwanza kurekodiwa punguo kama hilo katika muongo mmoja, licha ya viwango vya juu vya wakimbizi wa muda mrefu.

Ripoti ya UNHCR iliyotolewa jana Alhamisi, ilisema kwamba takriban watu milioni 5.4 walilazimika kukimbia makwao katika mwaka uliopita, na kufanya jumla ya wakimbizi na watu walio katika hali kama za wakimbizi kufikia milioni 41.6 duniani kote, wakiwemo takriban wakimbizi milioni 6 wa Kipalestina.

Kinyume chake, viwango vya kurudi nyumbani vimeongezeka pakubwa, huku takriban wakimbizi milioni 14.7 na watu waliokimbia makazi yao wakirejea katika nchi zao; hilo likiwa ni ongezeko la 50% ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake.

Operesheni kubwa zaidi za wakimbizi kurejea makwao zimeshuhudiwa katika nchi sita: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sudan, Syria, Afghanistan, Ukraine na Myanmar.

Hata hivyo, UNHCR imeonya kwamba kurejea idadi kubwa ya wakimbizi kumefanyika katika hali tete na ngumu, huku huduma za msingi zikiwa chache, katika hali ya uharibifu mkubwa wa miundombinu na ukosefu wa usalama ukiendelea, jambo linaloibua wasiwasi mkubwa kuhusu uendelevu wa kurejea na usalama wa waliorejea.

Afghanistan imeshuhudia mojawapo na kasi kubwa za wakimbizi kurejea nyumbani, na takriban watu milioni 2.9 walirejea nchini humo mwaka uliopita wa 2025 hasa kutoka nchi za Iran na Pakistan, ongezeko mara tano zaidi ya mwaka wa kabla yake.

Hii imechangia kupunguza idadi ya wakimbizi wa Afghanistan duniani kote kutoka milioni 5.8 mwaka 2024 hadi milioni 3.7 mwaka 2025.

Taarifa zinasema UNHCR, kama sehemu ya mpango wake wa muda mrefu, inataka kupunguza nusu ya idadi ya wakimbizi wanaoteseka kutokana na kuhamishwa kwa muda mrefu ifikapo mwaka 2035, kwa kuunga mkono fursa za elimu na ajira, hasa katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati ambazo zinahifadhi idadi kubwa zaidi ya wakimbizi, pamoja na kuwahimiza wakimbizi kurudi nyumbani kwa hiari na kuimarisha hali ya kujitegemea kwa wakimbizi hao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *