DODOMA: Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, amewataka Watanzania kuendelea kulinda amani, umoja na mshikamano wa taifa, akidai wana taarifa za kuaminika kuhusu mipango ya kuhamasisha vurugu kupitia maandamano yanayoratibiwa na baadhi ya makundi ya kisiasa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kihongosi amesema CCM imepokea taarifa zinazoonesha kuwa baadhi ya viongozi wa kisiasa na wanaharakati wanapanga kuhamasisha maandamano ambayo yanaweza kusababisha taharuki na kuvuruga utulivu wa nchi.

Amesema kuwa Watanzania wanapaswa kutambua kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo na uhuru wa taifa, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha analinda utulivu uliopo na kutokubali kushawishiwa kushiriki vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa nchi.
Kihongosi ameeleza kuwa kauli na ajenda zinazohamasisha maandamano zinaweza kuwa chanzo cha migogoro na kuvuruga mshikamano wa kitaifa, jambo ambalo halina maslahi kwa maendeleo ya wananchi.
Amesisitiza kuwa bila amani hakuna maendeleo, biashara, kilimo wala uhuru wa wananchi kutekeleza shughuli zao mbalimbali, hivyo akatoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kushiriki katika shughuli za uzalishaji, huku wakidumisha mshikamano na kulinda tunu ya amani.