
DODOMA: Wataalamu wa tiba asili hapa nchini wameiomba serikali kuendelea kuchukua hatua za makusudi za kuhamasisha utunzaji wa mazingira ili kuendelea kulinda maliasili na uoto wa asili.
Wamesema kuendelea kwa vitendo vya uharibifu wa mazingira kunachangia kupotea kwa baadhi ya tamaduni za Watanzania pamoja na mimea inayotumika kutengeneza dawa za asili.
Wakizungumza wilayani Kongwa mkoani Dodoma walipokutana kujadili changamoto zinazoikabili sekta hiyo, viongozi wa Chama cha Tiba Asili na Tiba Mbadala Tanzania (TAMESO-T) wamesema uhifadhi wa mazingira ni nguzo muhimu katika kulinda urithi wa tiba asili ambao umeendelea kusaidia huduma za afya kwa jamii kwa miaka mingi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TAMESO-T, Lucas Mlipu, amesema kuna haja ya kuongeza juhudi za upandaji miti na uhifadhi wa maeneo ya asili ili kuhakikisha mimea tiba haiendelei kutoweka kutokana na shughuli za kibinadamu zinazoharibu mazingira.
Naye, Mwenyekiti wa TAMESO-T, Bujukano Mahungu, amesema elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira inapaswa kupewa kipaumbele ili kizazi cha sasa na kijacho kiweze kunufaika na rasilimali hizo muhimu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mayeka Simon, amesema serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha mazingira yanatunzwa na maliasili zinahifadhiwa kwa manufaa ya maendeleo endelevu ya taifa.
Wadau hao wameeleza kuwa ushirikiano kati ya serikali, taasisi na wananchi ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira na kulinda urithi wa tiba asili nchini.