Dar es Salaam. Huzuni, simanzi na kumbukumbu za mchango mkubwa katika sanaa ndivyo vilivyotawala eneo la Kawe jijini Dar es Salaam wakati mamia ya waombolezaji walipokusanyika kumuaga muigizaji mkongwe wa filamu nchini, Issa Joseph Mohamed ‘Mzee Onyango’, aliyefariki dunia Juni 11, 2026.

Miongoni mwa viongozi waliojitokeza kutoa heshima za mwisho kwa mkongwe huyo wa sanaa alikuwa Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi, ambaye aliwasili pamoja na mkewe Mariam Mwinyi.

Uwepo wa Rais Mwinyi ulionyesha namna marehemu alivyokuwa na heshima kubwa katika jamii.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi akiwa na mkewe Mariam Mwinyi katika msiba wa Issa Joseph Mohamed.

Baada ya shughuli ya kuaga mwili wake, Rais Mwinyi aliungana na ndugu, jamaa, marafiki na wasanii katika safari ya kuelekea Makaburi ya Kondo yaliyopo Ununio, Dar es Salaam, ambako marehemu alizikwa.

Mzee Onyango ameacha watoto 10, wajukuu 12 na vitukuu 12.

Akizungumza wakati wa shughuli ya kuaga mwili wa marehemu, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, amesema Tanzania imepoteza mmoja wa wasanii walioweka msingi imara wa tasnia ya maigizo.

Amesema licha ya kusimama mbele ya waombolezaji kuzungumza, moyoni alikuwa amejawa na huzuni kubwa kutokana na mchango wa marehemu katika maendeleo ya sanaa nchini.

“Mzee Onyango alikuwa mpendwa wa watu wengi. Leo tunaona umati mkubwa wa waombolezaji uliokusanyika hapa kwa sababu aligusa maisha ya watu wengi kupitia kazi zake za sanaa,” amesema.

Anaongeza kuwa marehemu alikuwa miongoni mwa waanzilishi waliotoa maigizo kutoka redioni na kuyapeleka kwenye televisheni, hatua iliyochangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa tasnia ya filamu nchini.

“Mara nyingi watu walidhani ni raia wa nchi jirani kutokana na lafudhi na namna alivyocheza baadhi ya nafasi zake. Lakini ukweli ni kwamba alikuwa Mtanzania halisi na mcheshi hadi siku zake za mwisho,” amesema.

Mwakilishi wa familia Devotha Helman aliwashukuru Watanzania wote waliokuwa pamoja na marehemu katika kipindi chake cha ugonjwa na wale waliojitokeza kwenye msiba huo.

Amesema familia imeguswa na upendo mkubwa ulioonyeshwa na wananchi, viongozi, wasanii pamoja na madaktari wa Hospitali ya Jeshi ya Lugalo waliomhudumia marehemu katika siku zake za mwisho.

Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma (MwanaFA) akiweka shada kwenye kaburi la mwigizaji mkokwe Mzee Issa Joseph  maarufu Mzee Onyango leo Juni 13, 2026 kwenye makuburi ya Kondo yaliyopo Ununio jijini Dar es Salaam

“Kutoweka kwake kumeacha pengo kubwa sana katika familia na jamii kwa ujumla. Tunamuomba Mungu amlaze mahali pema peponi mzee wetu Onyango,” amesema.

Wasanii wamkumbuka kwa mchango wake

Muigizaji Jay B amesema amejifunza mengi kutoka kwa marehemu na kwamba alikuwa mmoja wa watu waliomsaidia kufanya mabadiliko kutoka maigizo ya redioni kwenda kwenye televisheni.

“Nitamkumbuka kwa mambo mengi.

Tumefanya kazi pamoja katika filamu mbalimbali na alikuwa mtu aliyependa kuona wasanii vijana wanapiga hatua,” amesema.

Amesema kifo hicho kimekatisha baadhi ya mipango yao ya kazi ikiwamo filamu mpya ambayo walikuwa wameanza kuijadili kabla ya umauti kumfika.

Mchekeshaji Joti akiwakilisha wasanii wengine kuweka shada katika kaburi la Mzee Onyango leo Juni 13, 2026 kwenye makuburi ya Kondo yaliyopo Ununio jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake, muigizaji Steve Nyerere amesema marehemu ameacha funzo kubwa kwa wasanii kutokana na bidii na mapenzi yake kwa sanaa hadi mwisho wa maisha yake.

“Alikuwa mtu wa kazi. Hata alipokuwa amezeeka bado alikuwa tayari kushiriki shughuli za sanaa. Hilo ni somo kubwa kwa kizazi cha sasa,” amesema.

Umati wafurika kumuaga

Kuanzia nyumbani kwa marehemu Kawe hadi makaburini Ununio, waombolezaji walionekana kwa wingi wakishiriki shughuli za mazishi.

Wasanii wa maigizo walikuwa miongoni mwa makundi yaliyojitokeza kwa idadi kubwa zaidi, jambo lililoonyesha heshima aliyokuwa nayo marehemu katika tasnia hiyo.

Ibada ya kuaga mwili wake ilichukua muda mrefu kutokana na idadi kubwa ya watu waliotaka kutoa heshima za mwisho.

Historia ya mwisho ya Mzee Onyango

Mzee Onyango alifariki dunia usiku wa kuamkia Juni 12, 2026 akiwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa mtoto wake, Joseph Issa, marehemu alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu (presha) kwa muda mrefu, huku hali yake ikibadilika mara kwa mara kabla ya kufariki dunia.

Kifo chake kimehitimisha safari ya mmoja wa waigizaji waliotoa mchango mkubwa katika historia ya maigizo ya Tanzania, huku wengi wakimkumbuka kama msanii aliyebeba tabasamu la Watanzania kwa miongo kadhaa na kusaidia kufungua njia kwa kizazi kipya cha waigizaji nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *