
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imeitaja safari ya rais wa jimbo lililotangaza kujitenga na Somalia la Somaliland huko Israel kuwa ni “dhambi ya kisiasa, ukiukaji wa kanuni na sheria zote za kimataifa, na kupuuza msimamo wa Waarabu na Waislamu kuhusu suala la Quds tukufu.”
Taarifa ya Hamas imelaani ziara hiyo, ambayo imemkutanisha Abdirahman Mohamed Abdullahi na viongozi wa utawala ghasibu wa Isarel wanaojulikana kwa rekodi yao ya uhalifu dhidi ya watu wa Palestina, na kutoa wito kwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) “kuchukua hatua za kuzuia eneo la Somaliland lililojitenga kuvunja msimamo wa Kiarabu kuhusu Palestina na kuanzisha uhusiano na utawala wa kifashisti.”
Mwezi mmoja uliopita, mnamo Mei 19, eneo lililojitenga na Somalia la Somaliland lililipua bomu baada ya kutangaza kwamba litafungua ubalozi huko Israel na kwamba rais wake atafanya ziara katika utawala huo hivi karibuni.
Inatazamiwa kuwa Abdirahman Mohamed Abdullahi atafungua rasmi ubalozi wa Somaliland huko Quds inayokaliwa kwa mabavu (Jerusalem) na kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na eneo hilo lililojitenga na Jamhuri ya Somalia ambalo halikutambuliwa na nchi yoyote kwa kipindi cha miaka 35.
Awali, Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud alipinga jaribio lolot la kuanzisha uhusiano kati ya nchi hiyo na utawala haramu wa Israel na kusisitiza msimamo thabiti wa Mogadishu kuhusu mapambano ya uhuru wa Palestina na uungaji mkono wake kwa haki za watu wa Palestina.
Sheikh Mohamud pia alisisitiza kwamba serikali yake inapinga hatua zozote zinazokiuka mamlaka na umoja wa ardhi ya Somalia, na kusema kile kinachosambazwa kuhusu kuanzishwa uhusiano au kufunguliwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Israel na eneo la Somaliland hakiwakilishi Jamhuri ya Shirikisho ya Somalia na hakina uhalali wowote wa kisheria au kisiasa.
Zaidi ya 99% Wasomali wanafuata dini ya Uislamu, na idadi yao mwanzoni mwa mwaka huu wa 2026 ilikadiriwa kuwa takriban watu milioni ishirini.