Wizara ya Intelijensia ya Iran imesema imefanikiwa kutekeleza operesheni za kupambana na ugaidi, ujasusi na hujuma nchini wakati wa uvamizi wa siku 39 wa Marekani na Israel ambao ulisitishwa mapema Aprili.

Wizara hiyo imesema katika taarifa ya Jumapili kwamba imekamata magaidi wanne, jasusi mmoja na wanachama kadhaa wa genge la hujuma za mitandao waliokuwa na nia ya kuchochea ghasia mitaani wakati wa uvamizi dhidi ya Iran.

Imesema operesheni hizo zimefanyika katika majimbo matatu, ikiwa ni pamoja na katika jimbo la Tehran.

Taarifa hiyo imesema, jasusi aliyekuwa akiripoti moja kwa moja kwa wakala wa idara ya ujasusi ya Israel iliyopo London alikamatwa katika jimbo la Ilam, lililo kwenye mpaka wa magharibi wa Iran na Iraq.

Jasusi huyo alikuwa akipanga kupenya kwenye taasisi muhimu za serikali na kudukua taarifa nyeti kuhusu mahali walipo maafisa wakuu wa nchi.

Wizara hiyo imesema kwamba wanachama wanne wa kundi la kigaidi linalofanya kazi katika jimbo la kusini-mashariki la Sistan na Baluchestan, karibu na mpaka na Pakistan, pia walikamatwa kabla ya kutekeleza operesheni dhidi ya taasisi za kiraia.

Wizara ya Intelijensia ya Iran imesema operesheni nyingine kubwa iliyofanywa wakati wa uvamizi wa Marekani na Israel nchini ilipelekea kukamatwa wahujumu 126, wakiwemo viongozi mashuhuri wa magenge ya uhalifu katika mji mkuu Tehran ambao walikuwa na nia ya kuchochea ghasia wakati wa uvamizi huo.

Operesheni hizo zilizofanikiwa zimekuja huku kukiwa na ripoti kwamba Marekani na utawala wa Israel zilitaka kutumia ghasia za ndani kudhoofisha serikali ya Iran na vikosi vya usalama wakati wa uvamizi huo.

Rais wa Marekani, Donald Trump, na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu wamekuwa wakitangaza mara kwa mara kwamba lengo kuu la uchokozi wao dhidi ya Iran ni kuwasaidia wapinzani kuangusha utawala wa Kiislamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *