Dodoma. Kila mwanadamu ana mapito yake hapa duniani. Wapo walioamini katika mafanikio lakini hawakufikia ndoto zao, na wengine walikutana na mafanikio bila kutarajia.

Katika safari hiyo, wapo waliotarajia na huenda walijipa matumaini ya ushindi, lakini wakaishia njiani bila kujua upande wa kuelekea. Hata hivyo, jambo muhimu ni kuendelea kuamini katika ushindi bila kukata tamaa.

Mifano mingi ipo kwa wanasiasa ambao kila mmoja huota ndoto ya kufikia nafasi za juu za uongozi, iwe kwa ajili ya kulitumikia taifa, kutafuta kipato au kupata cheo. Kwenye siasa, milima na mabonde ndiyo sehemu ya safari yenyewe.

Ndivyo ilivyokuwa safari ya Kiza Mayeye katika msako wa kutafuta ubunge, ndoto iliyodumu kwa miaka 30 kabla ya kutimia na hatimaye kufuta machozi ya baba yake.

Kiza alianza safari ya siasa za upinzani kupitia Chama cha Wananchi (CUF) akiwa mbunge wa Viti Maalumu na baadaye, baada ya msukosuko wa kisiasa ndani ya chama hicho, yeye pamoja na viongozi na wanachama wengine walihamia ACT Wazalendo.

“”Wazo la kutaka ubunge lilinijia mwaka 1995 nikiwa darasa la pili, siku hiyo baba (yangu Hussein Mayeye) alitoka kwenye mkutano wa kura za maoni ndani ya CCM halafu akarudi amepoa baada ya kushika nafasi ya pili, nikamwambia kwa sauti, ‘kama wamekushinda, ipo siku nitawashinda.

“Nilimwambia baba usihuzunike, kama wamekushinda ipo siku mimi nitawashinda, ipo siku jina lako litatajwa bungeni wakati mimi nikiwa mbunge na leo jina lake linatajwa mimi nikiwa bungeni,” anasema.

Katika mahojiano maalumu yaliyofanyika katika Ofisi za Mwananchi, mtaa wa Uhindini jijini Dodoma, akiangazia masuala mbalimbali, mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini anasema tangu wakati huo hakuwahi kuifuta ndoto hiyo hadi ilipotimia Oktoba 29, 2025, na akamfuta machozi baba yake aliyeshuhudia uapisho wake bungeni.

Anasema tangu mwaka 1990 baba yake alikuwa na ndoto za kuwatumikia wananchi, lakini ndoto hiyo iliishia njiani ndipo yeye akaamua kuitimiza, akiunganisha na ndoto ya baba yake.

Kwa nini aliwaza ubunge?

“Nilimuona baba akiwa kama aliyechanganyikiwa, hakuwa akiamini kilichomtokea maana alikuwa mshindi wa pili kwa mara ya pili mfululizo lakini tofauti ya kura chache mno, ilimuumiza baba ambaye kwa wakati huo alimini angekuwa mbunge,” anasema.

Kwa mujibu wa Kiza, mara ya kwanza baba yake kugombea ubunge ilikuwa mwaka 1990, lakini wakati huo yeye alikuwa mdogo sana kiasi cha kutoelewa kilichoendelea isipokuwa kupitia simulizi alizopewa baadaye.

Tukio lililobaki akilini mwake ni la mwaka 1995, alipokuwa amejiandaa kuwa mtoto wa mbunge, lakini matokeo ya jumla yalimtoa nje Mwalimu Mayeye, baba yake, ambaye kama ilivyokuwa mwaka 1990, alishika nafasi ya pili katika kura za maoni za CCM.

Tukio asilolisahau

Kama ilivyokuwa kwa baba yake, Kiza naye aligombea mara mbili katika jimbo hilo. Mara ya kwanza alipoteza mwaka 2020 katika uchaguzi anaosema ulikuwa mgumu, hasa katika hatua ya kutangaza matokeo. Anaamini kura alizopata zilimtosha kuwa mbunge, lakini mtihani ulikuwa kwenye utangazaji wa matokeo.

Wakati huo alikuwa CUF, na Mkurugenzi wa Uchaguzi alimtangaza kuwa amepata kura 16,000 huku mshindi akitangazwa kuwa na zaidi ya kura 22,000.

Hii ndiyo kusema kuwa mfupa mgumu uliomshinda baba yake, mwana ameutafuna baada ya kuuwekea malengo na kugundua siri ya ushindi ilikuwa kupitia ACT Wazalendo, akiamini ndiyo njia ambayo ingemfikisha Kanaani, na ndivyo ilivyokuwa.

Anasema siku alipotangazwa kuwa mshindi wa ubunge, sura ya baba yake ilikuwa tofauti na alivyoizoea, akieleza kuwa alikuwa na furaha iliyopitiliza.

“Kumbuka baba ni mwana-CCM hadi leo tunavyozungumza na huwa tunabishana sana kwa hoja. Lakini mwana ni mwana, hivyo kwenye ubunge wangu kuna mchango wake. Siku hiyo alinikumbatia, akatazama pembeni, sina uhakika, lakini alitoa machozi,” anasema Kiza.

Anataja kuwa mabishano yao yalihusu kila mmoja kumshawishi mwenzake kujiunga na chama anachokiamini, ingawa kwa sasa hubishana kwa hoja na hata kufurahia pamoja mechi za Simba, timu ambayo wote ni mashabiki.

Akutana na ugumu

Kabla ya yote, Kiza alikumbana na ugumu kutoka kwa baba yake mzazi kwani wakati anaanza harakati za siasa, baba yake alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, hivyo haikuwa rahisi kuona ndani ya familia yao kukiwa na mwanasiasa wa upinzani.

Hata hivyo, anamtaja baba yake kuwa mtu mwenye maono ya mbali anayependa kutoa uhuru wa mawazo bila kujali kama mtoto ni wa kike au wa kiume.

Anasema mzazi wake alimsikiliza na kumwelewa, ingawa mara kadhaa walikuwa wakibishana kwa hoja wanapokuwa nyumbani, lakini mbele ya majukwaa kila mmoja alinadi sera za chama chake.

Alitakiwa kujitoa mwaka 2025

Moja ya mambo anayoyakumbuka ni wingi wa simu na watu waliomfuata wakimtaka ajitoe kwenye kinyang’anyiro baada ya kutangazwa kwa jina la Peter Serukamba, ambaye wakati huo alikuwa ameacha nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

“Simu zilinichanganya hasa, watu walikuja kwa wingi wakisema nakwenda kupoteza pesa zangu kwa sababu Serukamba nisingemuweza. Jambo hilo lilinichanganya kidogo, lakini nikasema nakwenda kumshinda kwani huyu ndiye saizi yangu,” anasema.

Kwake, anaona kama angekabiliana na mtu ambaye hajawahi kuwa mbunge, huenda ingekuwa vigumu kumpata kwa hoja, lakini aliposikia ni Serukamba, akaamini tayari alikuwa na rekodi ya kisiasa ambayo angeweza kuijadili mbele ya wananchi.

Pia anasema wakati CCM walipokuwa wakielekea kwenye kura za maoni, alifunga kwa maombi kwa siku tatu akimuomba Mungu Serukamba ndiye ashinde, licha ya wengi kuamini angekuwa mgombea mgumu kumshinda.

Serukamba aliwahi kuwa mbunge wa Kigoma Mjini (2010–2015), kisha Kigoma Kaskazini (2015–2020). Wakati akiwa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alikuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chadema, na walibadilishana majimbo mwaka 2015 baada ya Zitto kuhamia ACT Wazalendo.

Kilichotokea mwaka 2025 kinafanana kwa kiasi fulani na mwaka 2015, ambapo Kiza alikusudia kugombea Kigoma Kaskazini kupitia CUF, lakini jimbo hilo liliachiwa Chadema chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Hata hivyo, Julai 2017, baada ya kupita miaka miwili, Kiza alipendekezwa na CUF na baadaye akateuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa mbunge wa Viti Maalumu miongoni mwa wabunge wanane waliojazia nafasi zilizoachwa wazi kutokana na migogoro ndani ya chama hicho.

Kuhusu upinzani

Mbunge huyo anasema upinzani unapitia milima na miiba, lakini jambo la msingi ni kuwa na ujasiri na kuamini katika matokeo chanya.

Anaamini chama tawala kimefika mwisho wa hoja mpya za kuwashawishi Watanzania, hivyo anaona ni wakati wa upinzani kuwasemea wananchi na kushughulikia changamoto zao.

Ndani ya Bunge anaamini kuwa licha ya uchache wao, wataendelea kujenga hoja zenye mashiko, huku akisisitiza kuwa upinzani si kupinga kila jambo wala kutukana, bali ni kuchambua na kuunga mkono au kupinga kwa masilahi ya wananchi.

Anasema matamanio yake ni kuona mambo yanakwenda vizuri bila kujali nani anasimamia au anatoka wapi, ilimradi maendeleo ya Watanzania yapatikane.

Kuhusu jimbo lake

Kiza anasema changamoto za jimbo lake zinamnyima usingizi, hasa mahangaiko ya akina mama katika vituo vya afya, wafanyabiashara wadogo, ukosefu wa madawati na vyoo shuleni, pamoja na changamoto za miundombinu ya barabara kwa ajili ya kufungua fursa za uchumi.

“Nina miezi sita tangu nianze rasmi kufanya kazi, lakini kuna mambo sitaki kuyasema yote. Nimefanya makubwa ukilinganisha na watangulizi wangu.

“Nimeanza maboresho na ukamilishaji wa maboma ya zahanati na vituo vya afya, kujenga vyoo vya wanafunzi, kuboresha masoko, na kufuta kero ya wanawake wanaojifungua wanaotakiwa kwenda na vifaa. Napambana kwa fedha zangu, natumia mfuko wa jimbo na pia nina marafiki wanaonisaidia,” anasema.

Anasema hakutafuta ubunge kwa ajili ya mafanikio binafsi, bali kuwa sauti ya wananchi wa Kigoma Kaskazini na kuacha alama zitakazowafanya wasijute kumchagua.

Anasisitiza wabunge wajenge imani kwa waliowachagua na wakumbuke ahadi walizozitoa wakati wa kampeni, kwa kuwa wapiga kura hawasahau waliyoahidiwa.

Ushauri wake kwa wanasiasa wanawake ni kupendana, kujiamini na kutosubiri kuwezeshwa, bali kujenga hoja na kufuatilia ndoto zao. Anasema hata yeye alibebwa zaidi na wanawake hadi akatangazwa mshindi.

Kiza Mayeye ni nani?

Ni mwanamke mwanasiasa aliyezaliwa Kijiji cha Mwandiga mkoani Kigoma, katika mtaa ambao pia wamezaliwa wanasiasa wawili waliowahi kuliongoza jimbo hilo kwa nyakati tofauti.

Miongoni mwao ni Peter Serukamba, aliyeshindana naye katika uchaguzi wa mwaka 2025, na Zitto Kabwe. Kwa historia, watatu hao walisoma shule moja na walifundishwa na Mwalimu Mayeye, baba mzazi wa Kiza.

Ni miongoni mwa wabunge wanane walioingia bungeni mwaka 2017 baada ya mgogoro kati ya aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, uliosababisha baadhi ya wabunge kuondolewa na nafasi hizo kuwa wazi.

Kiza ni msomi wa Chuo Kikuu cha St. Augustine cha Mwanza, alikosomea Mawasiliano na Utangazaji. Aliwahi kufanya kazi kama ofisa habari katika moja ya benki kabla ya kuacha kazi kwa hiari na kuingia rasmi kwenye siasa mwaka 2014.

Itaendelea kesho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *