
Dar es Salaam. Mjadala wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 unaanza leo bungeni jijini Dodoma huku wadau wakitaka hoja za wabunge zijikite kuangalia mifumo ya ukusanyaji wa mapato iliyopendekezwa na huduma za wananchi.
Wadau hao wanasema mara nyingi Bunge hupitisha makadirio makubwa ya mapato bila kujiridhisha kama mifumo iliyopo inaweza kufanikisha ukusanyaji huo bila ya kuwaongezea mzigo walipakodi na wafanyabiashara wadogo.
Wengine wanasema wabunge wanapaswa kuangalia kama ongezeko la bajeti hiyo ya Sh62.3 trilioni litaonekana moja kwa moja kwenye maisha ya wananchi wa kawaida. Bajeti ya 2025/26 ilikuwa Sh56.4 trilioni.
Hoja za wadau hao zinafanana na mijadala ya wabunge wakati wakijadili bajeti za kisekta kuanzia Aprili mosi hadi Juni 2, 2026. Kilio cha wawakilishi hao wa wananchi ni fedha kutotolewa kama zilivyopitishwa, hususan za miradi ya maendeleo.
Wabunge walilalamika na kuitaka Serikali kuhakikisha inatoa fedha kama zinavyopitishwa ili kuhakikisha mipango ambayo wizara zimepanga kutekeleza kwa wananchi inafanyika kuendana na ahadi za Ilani ya CCM ya mwaka 2025/2030 waliyoahidi.
Wakati huohuo, Kampuni ya Ernst & Young (EY Tanzania) imeichambua bajeti hiyo, ikipongeza baadhi ya maeneo na kuonya kuwa mageuzi ya kodi pekee hayatoshi ikiwa changamoto za gharama za maisha, mafuta na usafiri zitaendelea kuongezeka.
Mjadala wa bajeti hiyo iliyowasilishwa bungeni Juni 11, 2026, na Waziri wa Fedha, Dk Khamis Mussa Omar, utakuwa wa siku saba za kazi kuanza leo, Jumatatu, Juni 15 hadi Juni 23, mwaka huu.
Pia, watajadili taarifa ya hali ya uchumi iliyowasilishwa siku hiyohiyo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.
Hatua hiyo itafuatiwa na wabunge kuipigia kura bajeti hiyo kwa ajili ya kuiidhinisha. Bajeti hiyo ndiyo ya kwanza ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Wabunge wajikite humu…
Akizungumzia maeneo ambayo wabunge wanapaswa kujadili kuhusiana na bajeti hiyo, Mchambuzi wa Uchumi, Dk Baraka Mshana, anasema ni vema waangalie uwezo wa Serikali kukusanya mapato yaliyopangwa.
Mara nyingi, anasema, Bunge hupitisha makadirio makubwa ya mapato bila kujiridhisha kama mifumo iliyopo inaweza kufanikisha ukusanyaji huo bila kuwaongezea mzigo walipakodi na wafanyabiashara wadogo.
Anaeleza wabunge wanapaswa kuhoji kwa kina mkakati wa kupanua wigo wa kodi badala ya kuongeza shinikizo kwa walipa kodi walewale waliopo kwenye mfumo rasmi.
Kwa mtazamo wa Dk Mshana, uchumi wa Tanzania bado una kundi kubwa la shughuli zisizo rasmi zinazoweza kuingizwa kwenye mfumo bila kuathiri ukuaji wa biashara.
“Wabunge wasikubali kuishia kushangilia ukubwa wa bajeti. Waulize fedha hizi zitatoka wapi, kwa gharama gani na kwa athari gani kwa sekta binafsi. Bajeti nzuri si wingi wa fedha tu, bali iwe na vyanzo vya mapato vinavyotekelezeka,” anasema.
Anashauri mjadala uguse kwa undani deni la Taifa, malimbikizo ya madai ya wakandarasi na wazabuni, pamoja na namna Serikali itakavyodhibiti matumizi yasiyo ya lazima ili fedha nyingi zaidi ziende kwenye miradi ya maendeleo.
Maisha ya wananchi yaguswe
Mshauri wa Maendeleo ya Jamii, Profesa Rehema Mwangoka, anasema wabunge wanapaswa kuangalia kama ongezeko la bajeti linaonekana moja kwa moja kwenye maisha ya wananchi wa kawaida.
Anaeleza mara nyingi mijadala mingi huzungumzia reli, barabara na viwanja vya ndege huku huduma za msingi zikisahaulika.
Anasema ni muhimu wabunge kuhoji ubora wa huduma za afya vijijini, upatikanaji wa dawa, upungufu wa watumishi na hali ya miundombinu ya shule, hasa katika maeneo yanayokua kwa kasi kutokana na ongezeko la watu.
“Mjadala wa bajeti usiwe wa majengo na takwimu pekee. Mbunge akisimama aeleze mwananchi wa kijijini atanufaika vipi na Sh62.3 trilioni zinazojadiliwa Dodoma,” anasema.
Anasema wabunge pia wanapaswa kufuatilia kama fedha za maendeleo zinazotengwa kwa halmashauri zinafika kwa wakati, kwa kuwa kuchelewa kwa fedha hizo kumeendelea kuathiri utekelezaji wa miradi mingi inayogusa wananchi moja kwa moja.
Sekta binafsi iangaliwe
Mchambuzi wa masuala ya biashara na uwekezaji, Hamisi Mvungi, anasema mjadala wa bajeti unapaswa kuipa nafasi kubwa sekta binafsi kwa sababu ndiyo msingi wa uzalishaji ajira na mapato ya kodi.
Anasema wabunge wanapaswa kuhoji kwa kina mazingira ya biashara, gharama za mitaji, upatikanaji wa fedha kwa vijana na wanawake, pamoja na changamoto za soko kwa wazalishaji wa ndani.
Mvungi anasema Tanzania imewekeza fedha nyingi katika miundombinu mikubwa, lakini mafanikio ya uwekezaji huo yatategemea uwezo wa wafanyabiashara na viwanda vya ndani kutumia fursa hizo kuzalisha bidhaa na huduma kwa ushindani.
“Ningependa kuona wabunge wakijadili zaidi namna ya kutengeneza ajira kuliko namna ya kuongeza matumizi ya Serikali. Uchumi imara hujengwa na sekta binafsi yenye nguvu, si matumizi ya Serikali pekee,” anasema.
Anasema wabunge wanapaswa kuhoji utekelezaji wa vivutio vipya vya kodi na sera zilizotangazwa kwenye bajeti ili kuhakikisha vinawanufaisha wawekezaji wa ndani sambamba na wawekezaji wa kimataifa.
Uwajibikaji katika usimamizi wa fedha
Mchambuzi wa Siasa na Utawala, Dk Amina Kalinga, anasema hoja kubwa inayostahili kujitokeza katika mjadala huo ni suala la uwajibikaji wa matumizi ya fedha za umma.
Anaeleza kila mwaka Serikali huidhinishiwa mabilioni ya shilingi kwa ajili ya miradi mbalimbali, lakini baadhi yake huchelewa kukamilika au kugharimu zaidi ya ilivyopangwa.
Anasema wabunge wanapaswa kuwataka mawaziri kueleza matokeo ya fedha zilizotengwa katika mwaka unaomalizika kabla ya kuidhinisha fedha mpya.
Anasema mjadala wa bajeti unapaswa kujengwa zaidi kwenye matokeo kuliko ahadi.
“Mbunge anayewatumikia wananchi vizuri si yule anayesoma takwimu, bali anayewauliza watendaji kwa nini fedha zilizotolewa mwaka jana hazikuleta matokeo yaliyotarajiwa,” anasema.
Anasema Bunge linapaswa kuhoji kwa kina mifumo ya ufuatiliaji wa miradi, matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji wa mapato na hatua zinazochukuliwa dhidi ya ubadhirifu ili kila shilingi ya bajeti ionekane kwenye maendeleo halisi ya wananchi.
Uchambuzi wa bajeti yenyewe
Akichambua bajeti hiyo kwa ujumla, Mkurugenzi wa Huduma za Kimataifa za Kodi na Miamala wa Kampuni ya Ernst & Young (EY Tanzania), Chialu Masonobo, anapongeza msamaha wa mwaka mmoja wa kodi ya mapato kwa wafanyabiashara wapya.
Anasema biashara nyingi biashara changa hukabiliwa na changamoto ya kupata mapato ya kutosha katika hatua za mwanzo.
Pia, anasema pendekezo la kupunguza kodi ya faida inayobakizwa kwenye biashara kutoka asilimia 30 hadi asilimia 15 litaziwezesha kampuni kuwekeza zaidi na kuzalisha ajira.
Hata hivyo, anaonya kuwa mageuzi ya kodi pekee hayatoshi ikiwa changamoto za gharama za maisha, mafuta na usafiri zitaendelea kuongezeka.
Kwa upande wa usimamizi wa kodi, Meneja wa Kodi wa EY Tanzania, Happiness Gharabaster, anasema pendekezo la kulipa marejesho ya VAT ndani ya siku 30 litasaidia biashara nyingi zilizokuwa zikikwama kutokana na ucheleweshaji wa fedha hizo.
Anasema bajeti hiyo pia imeweka vivutio kwa sekta za nishati safi, viwanda na usafiri wa anga, ikiwemo nafuu za VAT kwa wasambazaji wa gesi ya kupikia (LPG), misamaha kwa vifaa vya kuchajia magari ya umeme na kuendelea kwa nafuu za ushuru kwenye mitambo ya uzalishaji.
Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Kodi wa EY Tanzania, Fredy Rugangila, anasema pendekezo la kuongeza kiwango cha mapato kinachotozwa kodi kutoka Sh100 milioni hadi Sh200 milioni kwa baadhi ya biashara litahamasisha biashara nyingi kuingia rasmi katika mfumo wa kodi.
Hata hivyo, anabainisha kuwa Serikali pia inalenga kuongeza mapato kupitia hatua mbalimbali, ikiwemo kuongeza kodi ya huduma za kidijitali kwa watoa huduma wasiokuwa wakazi wa Tanzania kutoka asilimia mbili hadi tatu.
Vipaumbele
Kuongeza ukusanyaji wa mapato: Serikali imepanga kuhakikisha inaongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuibua vyanzo vipya, kuimarisha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na hatua za kiutawala.
Kukamilisha miradi ya maendeleo: Serikali imepanga kuendelea na utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo zinazoendelea, ikiwemo uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
Kuimarisha uzalishaji: Serikali imelenga kuendelea kuimarisha sekta za uzalishaji kwa kupendekeza msamaha wa kodi na ushuru kwa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nchini, huku zinazotoka nje ya nchi zikiongezewa kodi.
Kuimarisha huduma za jamii: Serikali imelenga kuimarisha huduma za jamii ili kuwarahisishia wananchi. Pia, hatua hiyo itaambatana na kuboreshwa kwa huduma hizo.
Mazingira ya biashara: Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27, Serikali imepanga kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini. Katika hilo, Serikali imefanya maboresho katika sheria 55 na hivyo ada na tozo 374 zimepunguzwa au kufutwa.
Imeandikwa na Juma Issihaka, Rosemary Mirondo na Gadiosa Lamtey.