
Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameeleza haja ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na kutumia mifumo ya kisasa ya teknolojia ili kuhakikisha utekelezaji wa bajeti unafanyika bila kutegemea wafadhili.
Pia wamesisitiza kuwa ukuaji wa uchumi lazima uendane na uhalisia wa maisha ya wananchi, huku wakisema ongezeko la pato la Taifa linapaswa kuonekana moja kwa moja katika maisha ya watu wa kawaida.
Wakichangia mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/27 leo Jumatatu Juni 15, 2026 katika kikao cha Baraza la Wawakilishi Chukwani, Unguja, wajumbe hao wamesema kuna umuhimu wa kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi yanawanufaisha wananchi wote.
Kwa mwaka wa fedha 2026/27, SMZ inatarajia kutumia jumla ya Sh8.5 trilioni.
Mwakilishi wa Viti Maalum, Mariam Said Khamis (CCM), amesema licha ya mafanikio yanayoonekana katika ukuaji wa uchumi, bado kuna haja ya kuongeza kasi ili maendeleo hayo yaonekane katika maisha ya wananchi wa kawaida.
Amesema uchumi unakua lakini bado kuna pengo kati ya ukuaji huo na hali halisi ya maisha ya wananchi, hivyo Serikali inapaswa kuongeza juhudi zaidi.
Mariam amesema ili kufikia malengo ya kuongeza mapato, kunahitajika matumizi ya teknolojia ya kisasa itakayosaidia kupunguza mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali.
Akizungumzia deni la taifa, Mariam amesema licha ya kuonekana kuwa bado ni himilivu, serikali inapaswa kuhakikisha mikopo inayopatikana inatumika kwa miradi iliyokusudiwa na si kunufaisha watu wachache.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Malindi, Abdughani Ismail Zuberi (CCM), amesema Serikali inapaswa kutafuta vyanzo vipya vya mapato, ikiwemo kutoza kodi kwa majukwaa ya kidijitali.
Ameishauri Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) kuanzisha programu tumizi itakayowezesha wafanyabiashara kuwasilisha ritani zao kupitia simu badala ya kompyuta, ili kurahisisha ulipaji kodi na kupanua wigo wa mapato.
Zuberi amesema Zanzibar bado ipo nyuma katika sekta ya teknolojia na inahitaji uwekezaji zaidi ili kufikia malengo ya maendeleo ya kisasa.
Mwakilishi wa Paje, Jaku Hashim Ayubu (CCM), amesema bado kuna utitiri wa kodi unaowaumiza wananchi hususan wafanyabiashara wadogo.
Amesema iwapo Serikali imeondoa baadhi ya kodi katika sekta ya usafiri wa anga, inapaswa pia kuangalia uwezekano wa kupunguza kodi katika usafiri wa baharini unaotegemewa zaidi na wananchi wa kipato cha chini.
Mwakilishi wa Viti Maalum, Zainab Khamis Shomar (CCM), amesema ingawa bajeti inaeleza kuongeza kodi kwa baadhi ya bidhaa, ni muhimu kufafanua kiwango cha ongezeko kwa kila bidhaa kutokana na utofauti wake.
Hata hivyo ameunga mkono hatua ya kuondoa kodi viwanja vya ndege, akipendekeza pia kupunguzwa kwa baadhi ya kodi katika usafiri wa baharini ili kupunguza gharama kwa wananchi.
Aza Januari Joseph (Viti Maalum – CCM) ameshauri Serikali kupunguza gharama za upimaji wa afya kwa mama lishe ili kuwawezesha kufanya biashara zao kwa usalama, na kupunguza mzigo wa gharama za uendeshaji.
Akitoa maoni ya kamati, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Ali Suleiman Ameir amesema pamoja na hatua ya kuongeza kodi kwa baadhi ya bidhaa za nje ili kulinda uzalishaji wa ndani, Serikali inapaswa kuhakikisha hatua hizo zinaenda sambamba na kuimarisha uzalishaji wa ndani.
Kamati pia imeitaka Serikali kufanya tathimini ya kina kubaini kama hatua hizo zimefanikiwa kupunguza uingizaji wa bidhaa na kuongeza uzalishaji wa ndani.
Hadi Machi 2026, deni la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar limefikia Sh3 trilioni, likijumuisha deni la ndani la Sh2.987 trilioni na deni la nje la Sh1.4 trilioni, huku uwiano wake kwa Pato la Taifa ukiwa asilimia 40.63.
Kamati imeishauri Serikali kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi wa mikopo na misaada ya nje, pamoja na kuboresha usimamizi wa mapato ya serikali.
Pia imeitaka kuhakikisha mikopo inalipwa kwa wakati ili kuepuka ongezeko la gharama za riba na kulinda uhimilivu wa taasisi za kifedha.
Aidha kamati imeeleza kuwa kasi ya ongezeko la deni inapaswa kuendana na uwezo wa Serikali kulihudumia kwa kuimarisha mapato na matumizi pamoja na kudhibiti uwiano wa deni kwa Pato la Taifa chini ya kikomo cha asilimia 55 kinachokubalika kwa uhimilivu wa deni.
Kuhusu dhamana za Serikali zenye thamani ya Sh300 bilioni kwa taasisi za umma, kamati imeitaka Serikali kuweka bayana masharti na vigezo kabla ya kutoa dhamana hizo ili kuhakikisha mikopo inalipwa kwa wakati na fedha zinatumika kwa tija.