Dar es Salaam. Mbio za Absa Dar City Marathon 2026 zimeendelea kuonyesha kuwa zaidi ya mashindano ya riadha baada ya matokeo yake kusaidia kuimarisha huduma za afya katika Hospitali ya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kupitia utoaji wa vifaa tiba muhimu na kampeni ya uchangiaji damu inayolenga kuokoa maisha ya wagonjwa.
Kupitia ushirikiano kati ya Absa Bank Tanzania na The Runners Club, hospitali hiyo imekabidhiwa mashine ya kufuatilia hali za wagonjwa (patient monitor) pamoja na vifaa mbalimbali vya huduma za afya ya uzazi, hatua inayotarajiwa kuongeza uwezo wa wataalamu wa afya kutoa huduma bora kwa wajawazito na akina mama waliojifungua.
Msaada huo umetokana na mafanikio ya toleo la sita la Absa Dar City Marathon 2026 lililowakutanisha zaidi ya wakimbiaji 5,000 walioshiriki mbio za kilomita 21.1, kilomita 10 na kilomita 5, huku waandaaji wakisisitiza kuwa lengo la mbio hizo ni kuunganisha michezo na maendeleo ya kijamii.
Mashine iliyotolewa imeelezwa kuwa miongoni mwa vifaa vilivyokuwa vinahitajika katika wodi ya wazazi ya Hospitali ya Mnazi Mmoja kutokana na umuhimu wake katika kufuatilia viashiria muhimu vya afya za wagonjwa. Uwepo wake unatarajiwa kusaidia utoaji wa huduma za haraka na kuongeza usalama wa mama na mtoto wakati wa matibabu.
Mbali na mashine hiyo, taasisi hizo pia zimetoa vifaa tiba vinavyotumika katika huduma za kila siku za afya ya uzazi, ikiwemo glovu, mifuko ya mkojo, sindano, barakoa za upasuaji, bandeji pamoja na pamba maalumu za matibabu. Vifaa hivyo vinatarajiwa kupunguza changamoto za upatikanaji wa mahitaji muhimu hospitalini na kuboresha utoaji wa huduma kwa wagonjwa.
Sambamba na msaada huo, Absa Bank Tanzania na The Runners Club waliendesha kampeni ya uchangiaji damu katika Hospitali ya Mnazi Mmoja na Makao Makuu ya Absa Bank Tanzania kwa lengo la kuongeza akiba ya damu inayohitajika kwa wagonjwa mbalimbali wanaohitaji huduma za dharura.
Muuguzi Kiongozi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Shufaa Kaniki, akizungumza baada ya kupokea msaada wa vifaa vya hospitali kutoka kwa Meneja Huduma za Jamii na Matukio wa Benki ya Absa Tanzania, Abigail Lukuvi (kushoto), katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Meneja wa Huduma za Jamii na Matukio wa Absa Bank Tanzania, Abigail Lukuvi, amesema mbio za Absa Dar City Marathon zimeendelea kuwa chombo muhimu cha kuleta mabadiliko chanya katika jamii zaidi ya uwanja wa michezo.
Amesema kupitia utoaji wa vifaa tiba na uchangiaji damu, taasisi hiyo inalenga kusaidia sekta ya afya kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi na kuchangia ustawi wa jamii kwa ujumla.
“Kwa Absa Bank Tanzania, mbio hizi ni zaidi ya mashindano ya riadha. Ni jukwaa la kubadilisha maisha ya watu na kuimarisha jamii. Kupitia utoaji wa vifaa muhimu vya huduma za afya ya uzazi, vifaa tiba na damu inayookoa maisha, tunasaidia wataalamu wa afya kutoa huduma bora zaidi huku tukiwasaidia wagonjwa na familia zao katika nyakati wanazohitaji msaada zaidi,” amesema.
Kwa upande wake, Dk Mingole Said aliyepokea msaada huo kwa niaba ya Hospitali ya Mnazi Mmoja alisema mchango huo utasaidia kuongeza uwezo wa hospitali katika utoaji wa huduma za afya ya uzazi na matibabu kwa ujumla.
Amesema hospitali hiyo imeendelea kunufaika na mpango wa kijamii wa Absa Dar City Marathon kwa miaka mitatu mfululizo, jambo ambalo limekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya utoaji huduma kwa wagonjwa.
“Tunaishukuru timu ya Absa Dar City Marathon kwa kuendelea kutuchagua kuwa wanufaika wa mpango huu. Mashine ya kufuatilia wagonjwa pamoja na vifaa tiba vilivyotolewa leo vitaimarisha uwezo wetu wa kutoa huduma bora za afya ya uzazi. Pia tunapongeza kampeni ya uchangiaji damu kwa sababu upatikanaji wa damu ya kutosha bado ni moja ya changamoto kubwa zinazotukabili,” amesema.
Akizungumza kwa niaba ya The Runners Club, Godphrey Mwangungulu amesema mafanikio ya mbio hizo hayaishii katika siku ya mashindano pekee, bali yanaonekana kupitia manufaa yanayorejea kwa jamii.
Amesema ushiriki wa maelfu ya wakimbiaji katika mbio za mwaka huu umeonyesha jinsi michezo inavyoweza kuwa nguvu ya pamoja inayowezesha utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa wananchi.
“Absa Dar City Marathon siyo mbio pekee, bali ni jukwaa la kuwaunganisha watu kwa lengo la kuleta mabadiliko yenye maana katika jamii. Tunajivunia kuona nguvu ya ushiriki wa wananchi ikigeuzwa kuwa msaada halisi unaoimarisha huduma za afya na kuokoa maisha,” amesema.