
Nahodha wa Argentina, Lionel Messi amesema kwamba amejikuta akibubujikwa na machozi baada ya mechi yao dhidi ya Algeria kumalizika, usiku wa kuamkia leo, Jumatano, Juni 17, 2026 kwa vile kabla ya hapo amepitia katika kipindi kigumu.
Katika mechi hiyo, Argentina imeibuka na ushindi wa mabao 3-0, yote yakiwekwa kimiani na Messi.
Na mshambuliaji huyo amefichua kwamba mabao hayo matatu yamemtumia mzigo wa magumu ambayo ameyapitia, wakati akijiandaa na fainali hizo.
“Zilikuwa siku ngumu na hisia zangu ni kutokana na hilo. Nawashukuru wachezaji wenzangu, benchi la ufundi na kundi. Nina furaha sana na shukrani kwa hili kundi la kipekee. Nalifurahia sana.
“Mechi za ufunguzi mara nyingi zinakuwa ngumu na tumeona kwamba hakuna yeyote anaweza kutoa chochoye. Ni Kombe la Dunia lenye ushindani na timu zimejiandaa vizuri,” amesema Messi.
Katika mchezo huo dhidi ya Algeria, Messi ameifikia rekodi ya Miroslav Klose wa Ujerumani ya kuwa Mfungaji Bora wa muda wote wa Fainali za Kombe la Dunia akifunga mabao 16.
Messi pia ameweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kufunga mabao matatu (hat trick) katika mchezo mmoja wa Kombe la Dunia akifanya hivyo katika umri wa miaka 38 na siku 357.
Awali rekodi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Roger Milla wa Cameroon ambaye mwaka 1990 alifunga mabao matatu katika mechi moja ya Kombe la Dunia akiwa na umri wa miaka 38 na siku 34.
Pia Messi ameweka rekodi ya kufunga bao katika mechi tano mfululizo za Kombe la Dunia.