
Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limehimiza ushirikiano wa wadau wote, ikiwamo Serikali, sekta binafsi, taasisi za umma, jamii na wananchi, katika usimamizi na uhifadhi wa mazingira ili kufanikisha maendeleo endelevu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Juni 17, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja wa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa NEMC, Martha Kawishe amesema mazingira ni suala mtambuka linalohitaji kila mdau kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sheria na miongozo iliyowekwa.
Kawishe amesema NEMC inaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria za mazingira kupitia ukaguzi wa miradi na utoaji wa elimu kwa umma kuhusu udhibiti wa kelele chafuzi, uharibifu wa vyanzo vya maji, utupaji holela wa taka, utiririshaji wa maji taka hususan wakati wa msimu wa mvua, pamoja na ukataji hovyo wa miti.
Aidha, amesema baraza hilo linaendelea kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa nchini inazingatia Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) kabla ya kuanza shughuli zake.
Kawishe pia amewataka wananchi kuwa waangalifu dhidi ya watu wanaojifanya maofisa wa NEMC kwa lengo la kufanya udanganyifu. Amesisitiza kuwa malipo yote hufanyika kwa kufuata taratibu za Serikali na kwamba, ukaguzi wote unafanywa na maofisa wenye mamlaka kisheria.
Amesema maofisa hao wanapaswa kuwa na kitambulisho cha ukaguzi, kitambulisho cha kazi pamoja na nyaraka zinazowapa mamlaka ya kufanya ukaguzi.
Ameongeza kuwa ukaguzi wa NEMC hufanyika kidijitali, ambapo mteja hupokea ujumbe wa taarifa mara baada ya ukaguzi kukamilika.
Pia, NEMC imewahimiza wananchi kutumia huduma za kituo chake cha huduma kwa wateja kuwasilisha changamoto mbalimbali za kimazingira.