Iringa.  Mfumo mpya wa ukusanyaji taka wa Manispaa ya Iringa umefungua fursa mpya za kiuchumi, afya za wananchi, kung’arisha mji na kuchochea ajira kupitia uchakataji wake huku ikiongeza kiwango cha taka zinazokusanywa kutoka tani 131.24 hadi 148.39 kwa siku.

Mwananchi inashuhudia magari maalumu ya ukusanyaji taka yanayozunguka katika mitaa mbalimbali ya Manispaa ya Iringa ilivyokuwa alama ya mabadiliko makubwa katika usafi wa mazingira.

Mfumo huo umechangia kuondoa kwa kiasi kikubwa changamoto zilizokuwa zikihusishwa na ucheleweshaji wa ukusanyaji taka huku ukisaidia kuboresha mandhari ya mji, afya za wananchi, kuzalisha fursa mpya za kiuchumi kupitia uchakataji wa taka.

Awali, taka zilikuwa zikikusanywa kwa kuchelewa au kubaki kwa muda mrefu katika maeneo ya makazi ya watu, hali iliyosababisha malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya hofu ya magonjwa ya mlipuko.

Hata hivyo, hali hiyo imeanza kubadilika baada ya Manispaa ya Iringa kuingia katika mfumo wa ubinafsishaji wa huduma za ukusanyaji taka kupitia kampuni za Shirika la Uzalishaji la Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT) na kampuni ya ujenzi, usambazaji wa vifaa vya ujenzi na uhandisi (BEJOM).

Hatua hiyo imeonesha jinsi ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi unavyoweza kuleta matokeo chanya katika utoaji wa huduma za kijamii, hususan katika sekta ya afya ya mazingira.

Baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Miyomboni, Manispaa ya Iringa, wakipeleka taka katika gari la kubebea taka la kampuni za Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT), ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha usafi wa mazingira na afya ya jamii. Picha na Christina Thobias

Takwimu za mabadiliko

Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Taka na Usafi wa Mazingira, Manispaa ya Iringa, Samwel Subi anasema kabla ya kuanza kwa mfumo wa ubinafsishaji, manispaa ilikuwa ikikusanya wastani wa tani 131.24 za taka kwa siku.

“Baada ya kampuni za Suma JKT na BEJOM kuanza kutoa huduma, kiwango hicho kimeongezeka na kufikia tani 148.39 kwa siku,” anasema Subi.

Kwa mujibu wa Subi, ongezeko hilo linaashiria kuwa taka nyingi zaidi sasa zinakusanywa na kuondolewa kwa wakati tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Kuhusu malipo ya huduma,Subi anasema kila kaya inayopata huduma ya ukusanyaji taka huchangia Sh2,000 kwa mwezi ili kuwezesha huduma hiyo kuendelea kutolewa kwa ufanisi.

Kwa mtazamo wa wataalamu wa mazingira, ongezeko la kiwango cha taka zinazokusanywa lina maana kubwa zaidi ya takwimu na kila tani ya taka inayokusanywa kwa wakati ni hatua ya kupunguza uchafuzi wa mazingira, kuboresha afya ya jamii na kuongeza mvuto wa mji.

Usafi wa Manispaa kitaifa

Mafanikio hayo hayajaonekana tu katika ongezeko la kiwango cha taka zinazokusanywa kila siku, bali pia mwaka huu yametambuliwa katika ngazi ya kitaifa katika mashindano ya usafi wa mazingira.

Katika shindano hilo ambalo hujumuisha halmashauri zote nchini, Manispaa ya Iringa ilishika nafasi ya pili na kujinyakulia cheti cha pongezi pamoja na zawadi ya Sh 4 milioni kutoka Wizara ya afya.

Mafanikio hayo yanatokana na juhudi za kuboresha mfumo wa ukusanyaji taka, ushirikiano wa wananchi katika kutunza mazingira na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika utoaji wa huduma za usafi.

Hata hivyo, upatikanaji wa tuzo hiyo unatajwa kuongeza hadhi ya mji wa Iringa kama moja ya manispaa zinazofanya vizuri katika usimamizi wa mazingira nchini na kujali afya ya mwananchi.

Kauli za wananchi

Geofrey Mwashi, mkazi wa Kihesa, anasema mazingira ya eneo analoishi yamebadilika kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka michache iliyopita.

“Zamani taka zilikuwa zinakaa kwa muda mrefu kabla ya kubebwa na kulikuwa na harufu mbaya na nzi wengi hasa kipindi cha joto, lakini sasa magari yanapita mara kwa mara na hali imeimarika sana,” anasema Mwashi.

Agatha Mponela anasema mfumo wa sasa umeongeza uwajibikaji kwa sababu wananchi wanaweza kufuatilia huduma wanayolipia.

“Tulikuwa tunaona kama usafi ni jukumu la Halmashauri pekee na sasa tunaona matokeo ya mchango wetu kwa sababu taka zinachukuliwa kwa wakati,” anasema Agatha.

Kauli za wananchi hao zinaonesha kuwa maboresho yaliyofanyika hayaonekani tu kwenye takwimu za manispaa bali pia katika maisha ya watu wanaotumia huduma hizo kila siku.

Baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Miyomboni, Manispaa ya Iringa, wakipeleka taka katika gari la kubebea taka la kampuni za Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT), ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha usafi wa mazingira na afya ya jamii. Picha na Christina Thobias

Faida kwa afya ya Jamii

Mafanikio ya mfumo huo yanaungwa mkono na wataalamu wa afya ambao wanaamini mazingira safi ni msingi muhimu wa kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali.

Dk Fabian Mwasabwite wa Hospitali ya Sokoni Iringa, anasema mazingira safi yana mchango mkubwa katika kuzuia magonjwa yanayotokana na uchafuzi wa mazingira.

Anasema taka zinapobaki kwa muda mrefu kwenye maeneo ya makazi huongeza uwezekano wa kuenea kwa magonjwa kwa kuwa huwa mazalia ya nzi, mbu na wadudu wengine wanaosambaza maradhi.

“Usimamizi mzuri wa taka ni sehemu ya kinga ya afya ya jamii na tunapopunguza mrundikano wa taka katika maeneo ya makazi, tunapunguza hatari ya magonjwa kama kuhara na, homa ya matumbo.

“Lakini pia magonjwa mengine yanayochangiwa na uchafuzi wa mazingira, hivyo uwekezaji katika usafi wa mazingira ni uwekezaji katika afya za wananchi,” anasema Dk. Mwasabwite.

Taka zageuka fursa za ajira

Mbali na kuboresha mazingira na afya za wananchi, mfumo mpya wa usimamizi wa taka umeanza kufungua fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Iringa kwa kujipatia kipato na ajira kwa vijana na wabunifu.

Subi anasema taka nyingi zinazoweza kurejelezwa sasa zinakusanywa na kutumika kama malighafi katika shughuli mbalimbali za uzalishaji, hali iliyochochea uchumi kwa mtu mmoja mmoja.

“Kwa sasa, Manispaa ya Iringa ina vituo vitatu vya uchakataji wa taka za plastiki vinavyotoa fursa kwa wananchi kujipatia kipato kupitia biashara ya taka zinazoweza kurejelezwa,” anasema Subi.

Anaongeza kuwa wananchi wengi wamejiajiri kwa kuokota plastiki, vyuma na viloba kisha kuviuza kwa ajili ya kuchakatwa na kuzalisha bidhaa nyingine, hatua ambayo imebadilisha maisha ya wananchi.

Hata hivyo, katika maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo, vijana na wanawake wameanza kuona taka kama fursa badala ya uchafu na wengine hukusanya chupa za plastiki, mifuko ya nailoni na vyuma.

Mitaa 32 bado haijafikiwa

Pamoja na mafanikio hayo, takwimu zinaonesha kati ya mitaa 160 iliyopo katika manispaa hiyo, mitaa 32 ya pembezoni mwa mji huo bado hazijafikiwa na huduma hiyo.

Changamoto hiyo inatokana na ugumu wa miundombinu ya barabara katika maeneo hayo, jambo linalofanya magari makubwa ya taka kushindwa kufika kwa urahisi.

Baadhi ya wakazi wa maeneo ya pembezoni mwa mji wanasema bado wanatumia mbinu za kuchoma taka au kuzitupa kwenye mashimo kutokana na kukosekana kwa huduma ya magari.

“Tunafurahia kuona mji unasafishwa lakini bado tunahitaji huduma hizi zifike kwetu na hata sisi tuna haki ya kuishi katika mazingira safi,” anasema Debora Peter, mkazi wa Kihesa Mafifi Juu.

Hatua zinazohitajika

Wataalamu wa mazingira wanaeleza mafanikio ya muda mrefu yatategemea uwezo wa manispaa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya ukusanyaji taka, kuongeza elimu ya mazingira kwa wananchi.

Kadiri idadi ya watu wa Iringa inavyoendelea kuongezeka, ndivyo kiasi cha taka kinachozalishwa kinavyoongezeka hivyo, kuna haja ya kuendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji na uchakataji taka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *