Unguja. Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, inakusudia kufanya sensa ya uvuvi kupata takwimu sahihi za watu waliopo katika mnyororo wa thamani.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa inalenga kuongeza maendeleo katika sekta hiyo.

Sensa hiyo inayotarajiwa kuanza kufanyika mwezi huu, itawahusisha wavuvi, vyombo vya uvuvi, waanika dagaa pamoja na wakulima wa mwani. Kwa sasa Zanzibar inakadiriwa kuwa na wavuvi 32,000.

Akizungumza wakati wa mafunzo kwa watendaji wanaohusika na ukusanyaji wa takwimu hizo jana Jumanne, Juni 16, 2026, Katibu Mkuu mwenye dhamana na wizara hiyo, Hamad Bakari Hamad amesema sensa hiyo inalenga kuhakikisha upatikanaji wa taarifa sahihi zitakazoisaidia Serikali katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo.

“Sensa hii ni muhimu kwa sababu tunapata takwimu za wavuvi, vyombo vya uvuvi, waanika dagaa na wakulima wa mwani na wote waliopo katika mnyororo huo, kuhakikisha tunapanga mipango ya maendeleo kwa kufuata takwimu,” amesema.

Amesema kupitia uwezeshaji uliotolewa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, sensa hiyo itaimarisha uvuvi endelevu pamoja na ufugaji wa mazao ya bahari kupitia mradi wa Tasafram unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).

Kwa upande wake mjumbe wa Kamati ya sensa ya uvuvi, Dk Narriman Jidawi amesema program hiyo inatarajiwa kutoa data sahihi kwa mipango na uamuzi katika mipango ya maendeleo ya sekta ya uvuvi nchini.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, bila takwimu sahihi, wawekezaji hawajui wapi pa kuweka mitambo ya uvuvi wa bahari kuu, viwanda vya usindikaji, au kilimo cha samaki.

Akizungumza kuhusu mafunzo hayo, mmoja wa wanufaika, Nassor Abdallah Nassor amesema yatawajengea uwezo watendaji ili kukusanya taarifa sahihi katika maeneo ya madiko (mialo).

Pia kupitia sensa hiyo inasaidia kutatua migogoro kwa sababu wavuvi wengi Zanzibar wanategemea bahari kwa maisha yao, hivyo itasaida kupunguza migogoro ya mipaka ya bahari, na matumizi ya rasilimali baina ya jamii za Pwani.

Uzalishaji wa samaki nchini umeongezeka kutoka tani 78,943 zenye thamani ya Sh618.18 bilioni mwaka 2024 hadi kufikia tani 79,431 zenye thamani ya Sh624.9 bilioni mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia1.4.

Ongezeko hilo ambalo limechochea upatikanaji wa malighafi kwa shughuli za biashara, kuimarisha masoko ya mazao ya baharini na kuongeza kipato kwa wavuvi na wadau wengi, lilibainishwa na Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Masoud Ali Mohamed wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27 barazan hivi karibuni.

“Wizara imefanikiwa kuongeza uzalishaji wa mwani mkavu kutoka tani 19,716 mwaka 2024 hadi kufikia tani 20,075 zenye thamani ya Sh27.3 bilioni  zimesafirishwa nje ya nchi,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *