
KUNA uwezekano mkubwa msimu ujao Simba ikawa na kipa mpya baada ya mabosi wa klabu hiyo kuanza hesabu za kuisaka saini ya kipa Mzimbabwe Nelson Chadya wa Scottland FC ya nchini humo.
Uamuzi wa mabosi hao Simba kuisaka saini ya kipa huyo Mzimbabwe ni kutokana na kutoridhishwa na kiwango cha kipa Tanji Kassali raia wa Niger, pia majeruhi ya muda mrefu ya kipa Yakub Suleiman na Moussa Pinpin Camara, na wekundu hao kusalia na Hussein Abel pekee.
Hata hivyo, mabosi wa Simba wameonyesha wazi hawataki kuendelea na Camara licha ya kupona na kuanza mazoezi, wakati ambao kipa huyo mkataba wake ukifikia mwisho mara baada ya msimu huu kumalizika.
Ili kujiweka katika mazingira salama kwa msimu ujao, uongozi wa Simba umeona kipa bora zaidi katika Ligi Kuu Zimbabwe, Chadya anaweza kuwa jibu sahihi la matatizo yao.
Kipa Chadya katika michezo 20 aliyocheza amekusanya cleansheet 14 katika michezo 20 na kuisaidia Scottland kuendelea kukaa kileleni mwa ligi ya Zimbabwe hadi sasa.
Mbali na Chadya, Simba pia ilikuwa inafuatilia uwezo wa kipa mwingine Futuere Sibanda, anayeichezea ZPC Kariba ya hapo hapo Zimbabwe, ikipima wapi iongeze nguvu katika kutafuta mrithi wa Kassali na Camara.
“Tunaendelea na mchakato wa kutafuta kipa mwingine, tumetafakari sana lazima tutafute kipa mwingine, hawa tulionao sasa hawatoshi, umewataja hao wawili wa Zimbabwe (Chadya na Sibanda) ni kweli, lakini bado tunazungumza nao hakuna aliyesajiliwa tayari,” alisema bosi huyo.
“Tunataka kuwa na kipa ambaye atatupa imani kwamba lango letu lipo salama hata hao makipa wa ndani bado pia tunawatafakari lolote linawezaza kutokea eneo hilo mwisho wa msimu huu.”
Camara msimu uliopita alikuwa imara akiongoza kwa cleansheet 19, na kuisaidia Simba kumaliza nafasi ya pili katika ligi pamoja na kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini kuumia kwake kumefanya aondolewe kikosini kwa mujibu wa kanuni za ligi.
Kassali mpaka sasa amepata cleansheet 13 wakati Simba ikibakiza mechi tatu kumaliza msimu akiendelea kufukuzana na Djigui Diarra mwenye cleansheet 14, hakuna shaka makipa hao wawili wameonyesha kiwango bora.