
Huku nikitumai kuwa hujambo mpenzi msikilizaji popote pale ulipo, nakukaribisha kuwa nami katika Makala ya Wiki ya juma hili itakayoangazia jinsi mamlaka za Marekani, ambayo ni moja ya wenyeji wa mashindano ya Dunia ya soka yaliyoanza siku ya Alkhamisi, zilivyozitendea timu za nchi washiriki wa mashindano hayo zilipowasili nchini humo.
Wakati mashindano ya soka ya Kombe la Dunia la FIFA kwa mwaka 2026, yanayoandaliwa kwa pamoja na Marekani, Canada na Mexico, yakiwa yameanza rasmi siku ya Alkhamisi, mlolongo wa matukio yanayohusiana na masuala ya uhamiaji na utoaji viza kwa misafara ya timu, waamuzi na mashabiki kutoka nchi za Asia na Afrika, umeibua masuali mazito kuhusu uwezo wa Marekani kuwa mwenyeji asiyependelea upande wowote na anayewakaribisha kiusawa wageni wote wa mashindano hayo.
Ndani ya muda wa masaa 48 tu kilishuhudiwa kile kilichoonekana kama mwenendo wa ucheleweshaji viza, ukataaji maombi ya kuingia Marekani, pamoja na ukaguzi mkali wa kiusalama, hali ambayo imeziathiri kwa kiwango kikubwa zaidi misafara ya timu zilizotoka nchi za Kiislamu, za Asia na Afrika pamoja na mataifa mengine yaliyo nje ya ushirika wa Magharibi.
Matukio yote hayo yanaashiria kuwepo kwa matatizo ya kimfumo, na sera zinazobagua kwa misingi ya uraia, rangi na mwelekeo wa kisiasa, jambo linalokinzana na dhati halisi ya michuano ya Kombe la Dunia la FIFA.
Katika tukio la karibuni zaidi wakati wa hekaheka za kukaribia kuanza michuano hiyo, viza ya mshambuliaji wa timu ya taifa ya Uswisi, Breel Embolo, iliwekwa chini ya uchunguzi wa kiidara mara baada ya yeye na timu yake kuwasili nchini Marekani.
Mchakato huo ulimzuia Embolo kujiunga na wachezaji wenzake katika mazoezi kwa siku kadhaa, jambo lililoathiri maandalizi na utayari wake kiuchezaji, wakati ukiwa umesalia muda wa chini ya wiki moja kabla ya kuanza mashindano hayo.
Japokuwa hatimaye aliruhusiwa rasmi kuingia Marekani, lakini ucheleweshaji aliofanyiwa Breel Embolo mwanasoka maarufu barani Ulaya ambaye hana rekodi yoyote ya makosa ya jinai au masuala ya kiusalama, umeibua masuali kuhusu namna utaratibu wa kuingia Marekani usivyoweza kutabirika na jinsi unavyokinzana na uungwana wa kimichezo.
Huo ukiwa ndio msukosuko uliompata mwanasoka huyo wa timu ya taifa ya Uswisi, timu ya taifa ya soka ya Iran ilifikwa na makubwa zaidi ya hayo. Ni baada ya msafara wa timu hiyo kulazimika kupitisha kwanza siku kadhaa nchini Uturuki kwa ajili ya kukamilisha taratibu za viza katika Ubalozi Mdogo wa Marekani nchini humo.
Japokuwa timu hiyo ilifanikiwa hatimaye kupata viza za kuingia Marekani lakini watu 15 waliokuwemo kwenye msafara huo, wakiwemo makocha, maafisa wa usaidizi na meneja wa timu Mohammad Nabi, walikataliwa moja kwa moja kupatiwa viza, hali iliyoifanya timu ya soka ya Iran ifanye maandalizi yake ikiwa na idadi pungufu ya wahusika wa benchi lake la kiufundi.
Lakini kilichozua mjadala mkubwa zaidi ni kwamba wachezaji wa Iran wameruhusiwa kuingia Marekani siku za mechi tu, jambo linalowakosesha kutekeleza ratiba ya kawaida ya mazoezi, ya muda wa kabla ya mechi.
Siku ya Jumanne, zikiwa zimesalia siku tatu tu kabla ya ufunguzi rasmi wa mashindano ya soka ya Kombe la Dunia, mamlaka za Marekani zilizuia pia kuwepo kwa mashabiki wa Iran katika viwanja ambavyo timu ya taifa ya nchi hiyo itacheza mechi zake tatu za hatua ya makundi.
Shirikisho la soka la Iran lililaani vikali uamuzi huo wa ghafla uliochukuliwa na mamlaka za Marekani wa kufuta mgao wake wa tiketi. Kwa mujibu wa kanuni za FIFA, asilimia 8 ya tiketi za kila mechi inapasa itengwe kwa ajili ya mashirikisho ya soka ya timu zinazoshiriki.
Hayo yakiwa ndiyo iliyotendewa timu ya taifa ya soka ya Iran, nyota wa timu ya Iraq, Aymen Hussein, ambaye ni mfungaji bora wa timu hiyo, alizuiliwa na kuhojiwa kwa muda wa karibu masaa saba mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Chicago O’Hare. Hakukuwa na mashtaka rasmi wala maelezo ya wazi yaliyotolewa kuhalalisha au kutaja sababu za kuzuiliwa kwake kwa muda mrefu kama huo.
Lakini wakati yeye Hussein aliruhusiwa baadaye, mpiga picha rasmi wa timu ya soka ya Iraq Talal Salah alishikiliwa kwa muda wa masaa 10 katika uwanja huo wa ndege na mwishowe akakataliwa kuingia Marekani na kulazimishwa arejee Iraq.
Omar Abdulkadir Artan, ambaye alitangazwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuwa Mwamuzi Bora wa Afrika wa mwaka 2025 alizuiwa kuingia Marekani licha ya kusafiri akiwa na pasipoti ya kidiplomasia.
Baada ya kuzuiwa katika Uwanja wa Ndege wa Miami, FIFA ilitangaza rasmi, lakini bila kutoa maelezo ya kuridhisha, kuwa Artan hataruhusiwa kuchezesha mechi za mashindano hayo.
Hatua ya kumzuia mwamuzi mwenye hadhi hiyo, aliyechaguliwa na FIFA kuwa mmoja wa waamuzi bora duniani, imeibua masuali ya kama sera za Marekani za kudhibiti uingiaji wa nchini humo ndizo zenye kipaumbele kuliko mamlaka na maamuzi ya shirikisho hilo la kimataifa la soka.
MUZIKI
Timu ya taifa ya soka ya Afrika Kusini iliwasili Marekani kwa kuchelewa kuliko ilivyokuwa imepangwa, baada ya baadhi ya watu waliokuwemo kwenye msafara wake kushindwa kupata viza kwa wakati.
Ucheleweshaji huo usio na lazima ulivuruga maandalizi ya timu hiyo pamoja na mipango yake ya safari.
Kwa upande mwingine, baadhi ya wafanyakazi wa timu ya taifa ya Senegal walitakiwa kuvua nguo na viatu na kufanyiwa upekuzi wa kiusalama uliochukua muda mrefu wakati walipowasili Marekani.
Wahusika waliofanyiwa vitendo hivyo na wadadisi wa mambo walizielezea hatua hizo kuwa ni za kufurutu mpaka na zenye viashiria vya ubaguzi, hasa kwa kuwa taratibu kama hizo hazikuonekana kutumika kwa misafara ya timu za Ulaya au Amerika Kaskazini.
Mfano wa hatua hizo za kibaguzi ni ile iliyochukuliwa dhidi ya timu ya taifa ya Uzbekistan ambayo ilifanyiwa upekuzi mkali uliohusisha hata utumiaji mbwa wa kunusa mabomu mara baada ya kuwasili Marekani.
Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha upekuzi huo, na kuibua ukosoaji mkali kuhusu namna msafara wa timu ya taifa ya nchi hiyo ya Asia ya Kati ulivyotendewa licha ya kutokuwa na historia yoyote ya uadui na Marekani.
Wakosoaji wanasema matumizi ya mbwa wa kugundua viripuzi dhidi ya wanamichezo wa kimataifa na maafisa wa timu zao, bila kuwepo tishio lolote lenye uzito, ni kielelezo cha kuwachukulia watu kuwa ni washukiwa na watuhumiwa kwa sababu tu ya asili ya wanakotoka, jambo linalokinzana na uungwana unaotakiwa kuonyeshwa katika kombe la dunia.
Katika upande mwingine, mashabiki kadhaa wa Scotland waliokuwa na haki ya kuingia Marekani bila ya viza kupitia mfumo wa ESTA walifutiwa vibali vyao vya usafiri siku chache kabla ya kuondoka kuelekea huko.
Hatua hiyo ilichukuliwa na mamlaka za Marekani wakati mashabiki hao walikuwa tayari wamenunua tiketi za mechi na kuwekesha nafasi za malazi, jambo ambalo liliwatia hasara kubwa kifedha.
Hakuna maelezo rasmi yaliyotolewa kuhusu kufutwa kwa vibali hivyo.
Katika nchi mbalimbali duniani, mashabiki waliokuwa tayari wamenunua tiketi za Kombe la Soka la Dunia na kupanga safari zao walijulishwa kuwa maombi yao ya viza za kuingia Marekani yamekataliwa.
Akthari ya mashabiki wa soka kutoka Morocco waliokuwa tayari wamenunua tiketi za bei ya juu kwa ajili ya kuishangiria timu yao walinyimwa viza, hali iliyowasababishia hasara kubwa kifedha.
Katika kesi nyingi, maombi hayo yalikataliwa baada ya mashabiki hao kuwa tayari wameshatumia fedha za tiketi na huduma za malazi ambazo haziwezi kurejeshwa.
Kutokuwepo mfumo wenye uwazi na wa haraka wa kukata rufaa kwa matukio ya michezo ya kimataifa kumewafanya maelfu ya mashabiki washindwe kwenda kuona mubashara mashindano ambayo walikuwa tayari wameshayalipia.
Mlolongo wa matukio yaliyoshuhudiwa katika muda wa masaa 48 ya hekaheka za kuelekea kwenye michuano ya soka ya kombe la dunia umewakasirisha mashabiki wa soka na kuhoji kuhusu uwezo wa Marekani kuwa mwenyeji mkuu wa mchezo huo unaopendwa zaidi duniani.
Kwanza ni kwamba, sera za viza na udhibiti wa mipaka za Marekani zinaonekana kutotofautisha kwa kiwango cha kutosha kati ya wasafiri wa kawaida na washiriki waliothibitishwa rasmi katika mashindano makubwa ya kimataifa.
Pili, kuna tofauti zinazoonekana wazi katika namna timu kutoka maeneo mbalimbali ya dunia zinavyotendewa na mamlaka za Marekani. Misafara ya timu za Ulaya haijaripoti kucheleweshewa mambo yao, kuzuiliwa au kupekuliwa kiudhalilishaji. Lakini mkabala wake, timu za nchi za Kiislamu kama Iran na Iraq, mataifa ya Afrika kama Senegal na Afrika Kusini, pamoja na Uzbekistan inayotoka Asia ya Kati, zimefanyiwa maudhi na udhalilishaji.
Lakini tatu, kunyimwa kuingia Marekani mwamuzi kama Omar Abdulkadir Artan, aliyeteuliwa rasmi na FIFA na anayesafiri kwa kutumia pasipoti ya kidiplomasia, kunadhihirisha jinsi mamlaka za Marekani zinavyopuuza kanuni na maamuzi ya FIFA yenyewe, jambo linaloweza kuathiri hadhi ya mashindano hayo.
Na mwisho ni kuwa, hasara za kifedha walizopata mashabiki ambao viza zao zimekataliwa, baada ya kuwa wameshanunua tiketi na kujiandaa kwa safari, zinaonyesha kutokuwepo uratibu kati ya mamlaka za uhamiaji za Marekani na mifumo ya tiketi na lojistiki ya FIFA.
Kwa maelezo hayo mpenzi msikilizaji, tunatamatisha makala yetu ya wiki kwa juma hili. Nakushukuru kwa kunisikiliza, na nakuombea kila lenye kheri, fanaka na baraka maishani…/