Shinyanga. Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro ametoa maagizo kwa wenyeviti wa vijiji na watendaji wa kata wawe wamesoma taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi hadi kufikia Juni 30, 2026 na liwe limekamilika kwa maeneo yote katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Akizungumza leo Juni 18, 2026 katika ziara yake iliyofanyika katika kata ya Didia, Tarafa ya Itwangi Mtatiro ameeleza kuwa, kuna fedha ambazo wananchi wamekuwa wakichanga kwa ujenzi ukiwamo wa miundombinu, wanahitaji kujua namna pesa hizo zilivyotumika pamoja na risiti za matumizi yake ziwepo ili kujenga uaminifu kwa wananchi,
“Kufikia Juni 30, 2026 wenyeviti na watendaji wote nataka muwe mmesoma taarifa ya mapato na matumizi kwa wananchi, kuna pesa ambazo wananchi huchanga kwa ujenzi wa madarasa, zahanati na vyoo tunataka kujua zimetumikaje na risiti za malipo ziwepo,” amesema Mtatiro.
Baadhi ya wananchi wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro wakati akizungumza katika Tarafa ya Itwangi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Shule ya msingi Didia iliyopo kata ya Didia, Halmashuri ya Wilaya ya Shinyanga. Picha na Hellen Mdinda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Seth Antony ameeleza kuwa kumekuwa na changamoto ya barabara katika halmashauri hiyo inayotokana na ufinyu wa bajeti katika ujenzi wa barabara hizo, sambamba na ugawaji nguzo za umeme.
“Sera ya ugawaji nguzo imekuwa ni changamoto kwa sababu vijiji havilingani, tunaomba ugawaji wa nguzo za umeme uangalie na ukubwa wa kijiji, vijiji vyenye watu wengi tunaomba viongezewe nguzo ili basi kila mwanakijiji aweze kunufaika,” amesema Antony.
Baadhi ya wananchi wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro wakati akizungumza katika Tarafa ya Itwangi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Shule ya msingi Didia iliyopo kata ya Didia, Halmashuri ya Wilaya ya Shinyanga. Picha na Hellen Mdinda.
Kwa niaba ya madiwani, Diwani wa kata ya Didia, Sena Fredrick Sena amesema kuwa changamoto ya ukosefu wa umeme katika vitongoji bado ni kubwa unakuta kijiji kina vitongoji vinane na kati ya hivyo ni viwili tu vilivyo na umeme, hivyo ameiomba Serikali iliangalie hilo suala,
“Unakuta umeme umefika katika vijiji vyetu lakini ni vitongoji vichache tu vinavyonufaika, wengine bado wanateseka pia suala la maji unakuta yamefika shuleni tu lakini bado hayajasambazwa katika maeneo mengine,” amesema Sena.