
Dodoma. Ili kukabiliana na ugonjwa wa Ebola nchini, Serikali imepeleka maabara mbili Jongezi katika mikoa ya Kagera na Kigoma, kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika upimaji wa sampuli kwa wahisiwa wa Ebola hususani wanaoingia nchini kutoa mataifa jirani.
Hatua hiyo inajiri huku kukiwa na wahisiwa 64 wa ugonjwa wa Ebola nchini kutoka mikoa 21, ambapo kati yao wahisiwa 11 walikidhi vigezo na kulazimika kuchukuliwa sampuli zao kabla ya badaye kugundulika kuwa hawakuwa na ugonjwa huo.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa leo Alhamisi, Juni, 18 2026 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa tishio la ugonjwa wa Ebola na hatua zinazoendelea kuchukuliwa ili kuzuia na kuimarisha utayari.
Mchengerwa amesema, miongoni mwa wahisiwa waliogundulika ni wale walioingia nchini kutoka mataifa jirani kwa kupitia mipakani, bandari na viwanja vya ndege na tayari Serikali imeweka mipango ya kukabiliana na tatizo hili.
“Ili kubaini viashiria vya ugonjwa huu nchini, tumeongeza uchunguzi wa afya kwa wageni wanaoingia ndani ya Taifa letu kupitia mipaka, bandari na viwanja vya ndege ambapo mpaka kufikia sasa wahisiwa 64 wamegundulika kutoka mikoa 21,” amesema Mchengerwa.
Amesema uchunguzi huo unaambatana na usimikwaji wa maabara jongezi mbili katika mikoa ya Kigoma na Kagera ili kusogeza huduma ya upimaji sampuli za wahisiwa karibu na wananchi waliopo kwenye maeneo hayo.
Pamoja na kuimarisha uchunguzi kwenye maeneo ya kuingilia nchini kwa kukagua vyombo vya usafiri, ambapo 101,302 vimekaguliwa na wasafiri 164,652 wamechunguzwa katika mipaka ya nchi kavu, viwanja vya ndege na bandari.
“Tumefanikiwa kuchunguza wasafiri wa kimataifa 559 kutoka nchi zenye mlipuko na tutaendelea kufanya hivyo ili kuzuia ugonjwa huu kuingia nchini kwetu na tutapeleka wataalamu kwenye mataifa haya, ili kuongeza uwezo wa kukabiliana na Ebola,” amesema Mchengerwa.
Ameongeza kuwa mpaka kufikia sasa Serikali imetoa elimu kwa watoa huduma za afya kuhusu kinga, na namna ya kutoa huduma kwa wagonjwa wa Ebola ambapo jumla ya wataalamu 45,000 wamepatiwa elimu kwa njia ya mtandao na ana kwa ana.
Mchengerwa amesema, lengo la elimu hiyo ni kuhakikisha kuwa wataalamu wa afya wanapewa kipaumbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo ili kutoa nafasi kwa wataalamu hawa kusaidia waathirika ikiwa watagundulika.
Mbali na hayo Waziri pia ametoa wito kwa viongozi wa dini, jamii na jadi kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu kwa wananchi na kuhamasisha uchukuaji wa hatua madhubuti ili kuepuka hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo.