Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limeandika ukurasa mpya wa diplomasia katika michezo baada ya kukubali rasmi ombi la Saudi Arabia la kutoruhusu bendera yake ya taifa kulazwa chini na kugusa ardhi wakati wa mashindano ya Kombe la Dunia 2026.

Hatua hii ya kihistoria imeshuhudiwa kwa mara ya kwanza wakati wa sherehe za ufunguzi wa mechi yao ya Kundi H dhidi ya Uruguay, ambapo tofauti na desturi ya miaka mingi ya FIFA ya kulaza bendera za mataifa kama mabango makubwa kwenye nyasi, bendera ya Saudi Arabia ilibaki ikipeperushwa juu mikononi mwa vijana waliokuwa wameibeba.

Hata hivyo, ili kulinda usawa na mandhari ya uwanjani, FIFA ilichukua hatua ya kipekee kwa kuinyanyua na kuishikilia juu pia bendera ya wapinzani wao Uruguay.

Uamuzi huu umepongezwa duniani kote kama ishara ya ukomavu wa hali ya juu wa kitamaduni na heshima kwa misingi ya imani kwenye mashindano hayo makubwa yanayorindima nchini Marekani, Canada, na Mexico.

Sababu za Saudi Arabia kusimamia msimamo huo ni kuwepo kwa maandishi ya Kiarabu katikati ya bendera hiyo ya kijani yaliyofuma neno la Shahada (Kalimah Tayyibah), ambayo ndiyo nguzo ya kwanza na msingi mkuu wa imani ya dini ya Kiislamu.

Maandishi hayo yanasomeka:”Laa ilaaha illa-llaah, Muhammadur Rasuulullaah”.

Tafsiri yake ni “Hakuna Mungu anayestahili kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah, na Muhammad ni Mtume wa Allah.”

Hivyo, kutokana na utakatifu wa maneno haya yanayotaja majina ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, sheria za Saudi Arabia na kanuni za Kiislamu zinakataza vikali bendera hiyo kuwekwa chini au kugusa nyasi, ardhi, maji, au uso wowote ule wa chini.

Kuilaza chini bendera hiyo kunatafsiriwa kama ukosefu mkubwa wa adabu na kufuru dhidi ya utakatifu wa imani hiyo.

Pia, umuhimu wa bendera hii hauishii viwanjani pekee, bali unatawala itifaki zote za kidiplomasia duniani kote kupitia sheria kali za nchi hiyo

Tofauti na mataifa mengine ambayo hushusha bendera zao nusu mlingoti kama ishara ya maafa au msiba wa kitaifa, bendera ya Saudi Arabia haishushwi nusu mlingoti kamwe, hata mfalme anapofariki dunia.

Hii ni kwa sababu maneno matakatifu ya Mungu hayawezi kushushwa kwa ajili ya maombolezo ya kibinadamu.

Pia, Wizara ya Biashara ya Saudi Arabia inapiga marufuku matumizi ya bendera hiyo kwenye bidhaa za kibiashara kama fulana, viatu, kofia, au mifuko ili kuzuia uwezekano wa maneno hayo matakatifu kuchafuliwa, kukanyagwa, au kutupwa maeneo yasiyo na staha.

imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *