Esnat Joseph na watoto wake

Chanzo cha picha, Thuthuka Zondi / BBC

Afrika Kusini imekuwa mahali penye mazingira magumu kwa wahamiaji wasio na nyaraka halali, huku tarehe ya mwisho iliyowekwa na waandamanaji kwao kuondoka nchini ikikaribia.

“Nina hofu kubwa na nimeathirika kisaikolojia,” alisema Esnat Joseph, mwanamke wa miaka 36 kutoka Malawi, alipokuwa akijaribu kuwabembeleza watoto wake watatu wa mwaka mmoja waliokuwa wakilia.

Alikimbia nyumba yake katika makazi yasiyo rasmi katika mji wa bandari wa Durban, katika jimbo la KwaZulu-Natal, na kutafuta hifadhi katika eneo la wazi ambapo hadi wageni 7,000, wengi wao wakiwa Wamalawi wamekusanyika na mali zao kwa wiki mbili zilizopita.

“Watu walikuja nyumbani kwangu na kuniambia: ‘Lazima uondoke. Hatutaki muendelee kuishi hapa, hivyo rudi nchini kwenu.’ Walikuwa 10 na walikuwa na silaha,” alisema, akielezea jinsi kundi hilo la wanaume wa Afrika Kusini lilivyokuwa na mapanga na viboko.

“Walimkata mume wangu kichwani na shingoni. Walimshika shingo kana kwamba walitaka kumuua. Kwa neema ya Mungu bado yuko hai, lakini amelazwa hospitalini.”

Watu wengi wengine walioko katika eneo hilo, ambapo mashirika ya misaada yamekuwa yakigawa mablanketi na chakula, wameripoti vitisho vya aina hiyo vya kwenda nyumba kwa nyumba.

Hali hiyo inafuatia maandamano kadhaa yaliyofanyika mwaka huu, mengi yakiwa ya amani, yaliyoongozwa na kundi la kupinga wahamiaji la March and March, chama cha upinzani ActionSA na makundi mengine, ambayo yameweka tarehe 30 Juni kuwa mwisho kwa wahamiaji wasio na nyaraka kuondoka nchini.

Wakiwa na fimbo mikononi, waandamanaji wamekuwa wakiimba “Mabahambe” , msemo wa Kizulu unaomaanisha “Waondoke.”

Wakati siku ya mwisho ikiendelea kukaribia, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, alionya siku ya Jumanne kwamba “kuwalaumu watu walio katika mazingira magumu” si suluhisho la changamoto ngumu za kiuchumi zinazoikabili nchi hiyo.

Waandamanaji

Esnat Joseph alifika Afrika Kusini miaka mitatu iliyopita na alikuwa akifanya kazi ya ndani kabla ya kupata watoto wake.

Hali yake ya kisheria haijulikani wazi. Anasema alipoteza pasipoti yake na nyaraka nyingine muhimu katika tukio la wizi. Ana mpango wa kurejea Malawi kupitia mojawapo ya mabasi ambayo ubalozi mdogo wa Malawi umekuwa ukiandaa, kwa msaada wa michango, ili kuwasaidia raia wake waliokata tamaa kuondoka Durban.

Nchi za Ghana, Msumbiji, Nigeria na Zimbabwe pia zimekuwa zikiandaa safari za kurejesha raia wao kwa ndege au mabasi katika wiki za hivi karibuni, huku takribani wageni 3,500 wakijitolea kuondoka hadi sasa.

Mamlaka za Afrika Kusini zilisema kwamba zaidi ya Wanigeria 500 waliorejeshwa hivi karibuni walikuwa wanaishi nchini humo kinyume cha sheria.

Akiwasili mjini Lagos wiki iliyopita baada ya karibu miaka tisa nchini Afrika Kusini, Benjamin, ambaye alitoa jina lake la kwanza tu, aliiambia BBC:

“Waafrika Kusini hawawapendi wageni, hasa Wanigeria. Afrika Kusini si mahali pa kuishi, ni mahali ambapo unaweza kupoteza maisha yako wakati wowote.”

Waandaaji wa maandamano wanakanusha kwamba vitendo vyao vina chuki dhidi ya wageni.

Wanasema wamechoshwa na kile wanachodai ni matumizi mabaya ya mfumo na wahamiaji kutoka mataifa mengine ya Afrika, na kama alivyoeleza kiongozi wa kundi la March and March, Jacinta Ngobese-Zuma, “kujifanya waathirika.”

“Ikiwa umeingia Afrika Kusini kwa pasipoti inayokuruhusu kukaa kwa siku 30, lakini ukabaki kwa siku 50, miaka miwili au hata miaka mitano, unajua kwamba unavunja sheria,” aliiambia BBC wakati wa maandamano huko Durban.

“Hatuwezi kuruhusu Afrika Kusini kugeuzwa kuwa kambi ya wakimbizi kwa mataifa yote ya Afrika yaliyoshindwa… Kila nchi huweka raia wake mbele, na tunataka serikali ya Afrika Kusini ifanye hivyo pia.”

Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa Afrika Kusini ina zaidi ya wageni milioni tatu, sawa na karibu asilimia 5 ya idadi ya watu wake, wengi wao wakitoka nchi jirani za kusini mwa Afrika.

Hata hivyo, takwimu hizo hazijumuishi wahamiaji wengi zaidi wanaoaminika kuishi nchini humo bila nyaraka halali, jambo ambalo limekuwa chanzo kikuu cha malalamiko ya waandamanaji.

Hasira yao inatokana na hali ngumu ya maisha inayoongezeka huku nchi ikikabiliwa na ukosefu mkubwa wa ajira kwa vijana na pengo kubwa la kiuchumi kati ya matajiri na maskini.

Afrika Kusini ina moja ya viwango vya juu zaidi vya ukosefu wa ajira duniani, ikiwa ni asilimia 32.7, kulingana na Statistics South Africa, ambayo iliripoti kupotea kwa ajira 350,000 katika robo ya kwanza ya mwaka 2026. Wengi wa waliopoteza ajira ni vijana.

Hata hivyo, uchumi wa Afrika Kusini, ambao ndio mkubwa na ulioendelea zaidi barani Afrika, unaendelea kuvutia raia wa nchi maskini zaidi wanaohatarisha maisha yao kwenda huko kutafuta kazi kama walinzi, wafanyakazi wa ndani na kazi nyingine za kipato.

Waandamanaji, kama Mecha Ramorola, pia wanaeleza wasiwasi wao kuhusu huduma za umma zilizolemewa, wakisema kwamba wananchi wa Afrika Kusini wanashindania rasilimali chache zilizopo.

“Tunahangaika kupata nafasi za shule kwa watoto wetu. Tunahangaika kuwapeleka wazee wetu hospitalini,” Ramorola aliiambia BBC wakati wa maandamano katika mji mkuu, Pretoria.

Hata hivyo, kuna hofu kwamba maandamano haya yanaweza kusababisha kurudiwa kwa ghasia za mwaka 2008, ambapo watu 62, wakiwemo Waafrika Kusini 21, waliuawa katika vurugu zilizowalazimisha maelfu kuhama makazi yao. Pia kulikuwa na milipuko ya vurugu dhidi ya wageni mwaka 2015, 2016 na 2019.

Mwezi uliopita, serikali ya Msumbiji ilisema kuwa raia wake watano waliuawa katika mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni katika jimbo la Western Cape. Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini alipinga madai hayo, akisema kuwa raia wawili wa Msumbiji ndio waliokufa na kwamba mazingira ya vifo hivyo bado yanachunguzwa.

Video zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zimeongeza uhasama dhidi ya wageni.

Katika video moja, mwanaume kutoka Ghana anaonekana akinyanyaswa na waandamanaji wanaomtaka arudi nyumbani, jambo lililoifanya Ghana kumwita balozi wa Afrika Kusini ili kudai ulinzi bora kwa raia wa kigeni.

Video nyingine iliyosambazwa sana inaonesha mwanaharakati maarufu wa maandamano, Nkosikhona Ndabandaba, anayejulikana kwa jina la Phakel’umthakathi na mwenye wafuasi milioni 1.4 kwenye Facebook, akimkaribia mwanaume aliyesimama kando ya barabara na kumuuliza uraia wake.

Baada ya mwanaume huyo kujibu kuwa ni raia wa DRC, Ndabandaba, akiwa amevaa vazi lake maarufu la kichwani la Kizulu, alimwambia kwa sauti ya upole lakini bila kuuliza kuhusu hali yake ya kisheria:

“Tarehe 30 Juni ndiyo mwisho, lakini si lazima usubiri hadi tarehe hiyo. Ondoka sasa.”

Wahamiaji

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Lakini wageni wanaoishi nchini Afrika Kusini kihalali wanasema nao pia wamekuwa wakilengwa. Baadhi yao wameweka kambi nje ya ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani mjini Durban wakitafuta ulinzi.

“Mimi nina nyaraka zinazotambua hadhi yangu ya ukimbizi nchini Afrika Kusini, lakini bado sisi sote tunafukuzwa,” mwanamke mmoja kutoka Burundi, aliyekuwa pamoja na watoto wake wanne, aliiambia BBC.

“Ninahofu na maisha yangu. Watoto wanaogopa. Hakuna heshima. Unapopita hapa unatukanwa. Watoto wanatukanwa hata shuleni,” alisema huku akijifunika blanketi kujikinga na baridi kali ya majira ya baridi.

Hata kwenda dukani siku hizi kunaweza kutisha, alisema mtaalamu wa urembo kutoka Malawi anayeishi Cape Town, ambaye ameishi Afrika Kusini kwa miaka 16 bila hadhi ya kisheria.

Yeye, mume wake na binti yao wa miaka tisa walikumbana na tukio la kutisha walipokuwa wakisafiri kwa Uber kwenda kwenye kituo cha biashara.

“Tulikuwa ndani ya Uber sisi watatu tu, na dereva alianza kutuuliza: ‘Nyaraka zenu ziko wapi? Mnatoka wapi? Lafudhi yenu ni tofauti.'”

Mtaalamu huyo wa urembo alisema anaelewa kwa nini Rais Cyril Ramaphosa hivi karibuni alitangaza mpango wa kushughulikia uhamiaji haramu, lakini alisisitiza kuwa kila binadamu, awe na hadhi ya kisheria au la, ana haki ya kuishi kwa usalama.

“Mtoto wangu hata haendi shule kwa sababu tunaogopa. Tuna hofu kubwa ya kile kinachoweza kutokea sasa.”

Katika hotuba maalumu kwa taifa mapema mwezi huu, Ramaphosa alionya kwamba hakuna mtu binafsi wala kundi lenye haki ya kuwataka watu waoneshe uthibitisho wa uraia wao katika maeneo ya umma, na akasema serikali itachukua hatua dhidi ya wanaofanya hivyo.

“Hakuna nafasi ya chuki dhidi ya wageni, ubaguzi wa rangi, ubaguzi wa kijinsia, chuki dhidi ya Waafrika, au aina yoyote ya kutovumiliana nchini Afrika Kusini,” alisema alipokuwa akieleza mkakati wa serikali yake ya muungano wa vyama mbalimbali wa kushughulikia mgogoro huo.

Hatua hizo zinajumuisha kukataa maombi ya hifadhi kutoka kwa watu waliopita katika nchi nyingine zinazochukuliwa kuwa salama, kuanzishwa kwa mfumo wa kiwango maalumu kwa ajili ya uraia wa wageni, na kupanua matumizi ya vitambulisho vya kidijitali kwa watu wasiokuwa raia wa Afrika Kusini.

Pia kutakuwa na vifungo vya jela kwa waajiri watakaowapa wahamiaji wasio na nyaraka kazi zenye mishahara midogo.

“Mara nyingi unakuta mhamiaji anaajiriwa katika kazi ambazo raia wa Afrika Kusini kwa kawaida hawatakubali kufanya, au kwa mshahara wa chini kuliko kiwango kinachotakiwa na serikali. Sababu ni kwamba wanakuwa na uhitaji mkubwa na wako tayari zaidi kwa kunyonywa,” alisema Shepherd Mpofu katika mahojiano na BBC.

Ramaphosa pia alisema juhudi zitaongezwa ili kupambana na rushwa ndani ya mfumo wa uhamiaji.

Mwanamke mmoja wa Malawi mwenye umri wa miaka 36 anayeishi Johannesburg, ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuhofia kulipiziwa kisasi, aliiambia BBC kuwa aliingia Afrika Kusini kwa visa ya utalii na alikuwa akiwapa rushwa maafisa wa mpakani ili wapige mihuri kwenye pasipoti yake kila baada ya miezi michache bila yeye kuvuka mpaka.

“Nimeamua kurudi nyumbani kwa muda na kufunga saluni yangu ya kusuka nywele kutokana na vitisho vinavyoendelea,” alisema, akieleza kwamba ana hofu kuhusu usalama wa watoto wake wadogo.

Operesheni ya serikali inayojulikana kama 'Operation New Broom' imeshuhudia vibanda vya biashara visivyo rasmi, ambavyo mara nyingi huendeshwa na wahamiaji wasio na nyaraka halali, vikibomolewa kwa kutumia mitambo ya kubomoa jijini Johannesburg.

Ongezeko la hivi karibuni la maandamano linakuja wakati vyama vya siasa vinatafuta kuungwa mkono na wapiga kura kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwezi Novemba.

Baadhi ya wanasiasa wasio waaminifu wamekuwa wakitumia taarifa za kupotosha kuchochea hofu na hasira kuhusu uhamiaji haramu, kwa kusambaza video za zamani na kuleta mkanganyiko kuhusu hali halisi.

Dai ambalo limekanushwa kwamba Afrika Kusini ina wahamiaji haramu milioni 15, lililoanza kusambazwa miaka mitano iliyopita na kiongozi wa ActionSA, Herman Mashaba, ambaye anawania kuwa meya wa Johannesburg, limeendelea kujitokeza mara kwa mara.

“Vyama vya siasa vinafanya kila wawezalo kuwadanganya watu kwamba matatizo yote ya Afrika Kusini yanasababishwa na wahamiaji, na kwamba tukiwafukuza wahamiaji basi matatizo yote yataisha,” alisema Sharon Ekambaram, mwanasheria wa haki za binadamu na mwanachama wa harakati za Kopanang Africa Against Xenophobia.

“Hili limekuwa jambo linaloendelea kwa muda mrefu nchini Afrika Kusini, na hivi karibuni limekuwa likihusishwa zaidi na vipindi vya uchaguzi.”

Serikali imeendelea kupinga madai hayo. Kikosi kazi kinachoshughulikia masuala ya uhamiaji kilisema wiki hii kwamba wahamiaji haramu 40,000 wamekamatwa tangu mwanzo wa mwaka huu kwa kukiuka Sheria ya Uhamiaji.

Hatua hizi zinaonekana wazi kupitia operesheni inayojulikana kama Operation New Broom, ambayo imekuwa ikitekelezwa katika maeneo ya katikati mwa jiji la Johannesburg.

Kwa miezi kadhaa iliyopita, mashine kubwa za kuchimba na kubomoa zimekuwa zikiharibu vibanda vya biashara vilivyojengwa kwa mabati kwenye njia za watembea kwa miguu.

Maafisa wa serikali wanaona maeneo hayo kuwa yanaweza kuwa vituo vya uhalifu na makazi ya wahamiaji haramu.

Siku niliyotembelea eneo hilo, wahamiaji kutoka Ethiopia walitazama kwa huzuni na mshtuko uharibifu huo ukiendelea, ingawa walikuwa wamepewa taarifa ya awali na mamlaka kuhusu hatua hiyo.

Baadhi ya Wanigeria walioomba kurejeshwa nchini mwao waliwasili nyumbani wiki iliyopita.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Hatua hizi pamoja na maandamano yanayoendelea zimewaacha wahamiaji wengi wakihisi kana kwamba wanazidi kukosa nafasi ya kuishi kwa amani nchini Afrika Kusini.

uMkhonto we Sizwe (MK), chama cha tatu kwa ukubwa nchini kinachoongozwa na Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, na chenye uungwaji mkono mkubwa eneo la KwaZulu-Natal, hakijaunga mkono rasmi muda wa mwisho uliowekwa kwa wahamiaji kuondoka nchini. Hata hivyo, kinaunga mkono hisia zilizo nyuma ya madai hayo.

“Sote tunakubaliana kwamba wahamiaji wasio na nyaraka wanavunja sheria… Wanapaswa kuondoka nchini mwetu kwa amani bila vurugu wala vitisho,” alisema mwanachama wa MK, Bonginkosi Khanyile, katika mahojiano na BBC.

Hata hivyo, hofu kubwa imeenea kote nchini kufuatia onyo kali kutoka kwa Nkosikhona Ndabandaba, mmoja wa viongozi wakuu wa maandamano.

“Mnamo tarehe 30 Juni sitaweza kuwazuia watu wa Afrika Kusini,” alisema.

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, misururu mirefu ya magari imeonekana katika kituo cha mpakani cha Msumbiji, huku wageni wengi wakiharakisha kuondoka kutokana na hofu na kutokuwa na uhakika kuhusu hali ya usalama.

Katika uwanja wa wazi huko Durban, Wamalawi wengi waliokumbwa na hofu, ambao kwa mujibu wa maafisa wengi hawana nyaraka halali wanasubiri kwa shauku kuondoka.

Basi la kwanza lilipowasili siku ya Jumapili kuwahamisha baadhi yao, umati ulianza kuimba kwa lugha ya Kizulu:

“Siyahamba”, yaani “Tunaondoka.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *