
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vitendo vya Wazayuni kuvunjia heshima na kushambulia misikiti ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Esmail Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali vitendo vya jinai vya walowezi wa Kizayuni wanaosaidiwa na jeshi linalokalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina la utawala huo ghasibu, vya kushambulia misikiti miwili ya Ramallah katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na pia kushambulia nyumba, kuwapiga Wapalestina na kuharibu mali na mashamba yao.
Amesema jinai hizo ni muendelezo wa siasa za mauaji ya kikoloni za utawala wa Kizayuni katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Ameeleza masikitiko yake makubwa kutokana na kuendelea kukaa kimya mashirika ya kimataifa na ya kutetea haki za binadamu na kueleza kuwa, kuendelea kutochukua hatua Umoja wa Mataifa na Baraza lake la Usalama dhidi ya jinai za utawala ghasibu wa Kizayuni kumepelekea utawala huo kuendelea kukiuka sheria na kutekeleza jinai kubwa dhidi ya Wapalestina na nchi nyingine za eneo.
Baqhaei pia amekumbushia dhima ya kidini na kisheria ya madola ya Kiislamu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina katika kupigania haki zao za kujitawala na kusimamisha mauaji na jinai za utawala wa Kizayuni dhidi yao, na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za kivitendo na mifumo ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ili kuulinda Msikiti wa Al-Aqsa na maeneo mengine ya kidini dhidi ya uvamizi wa utawala ghasibu wa Kizayuni, na kuadhibiwa wahalifu na wachochezi wa jinai hizo.
Wakati huo huo Pakistan, na nchi nyingine saba za Kiarabu na Kiislamu, zimetoa taarifa ya pamoja ya kulaani vikali kuongezeka ghasia zinazofanywa na walowezi wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Pakistan, Misri, Uturuki, Indonesia, Jordan, Qatar, Saudi Arabia na Imarati wamelaani katika taarifa yao ya pamoja mashambulizi ya karibuni ya Wazayuni dhidi ya Msikiti Mkuu wa Ijumaa katika kijiji cha Jaljilia na Msikiti wa Al-Farooq katika kijiji cha Mazara Al-Nubani kaskazini mwa Ramallah, na kuyataja kuwa ukiukaji wa wazi wa matukufu ya maeneo matakatifu na sheria za kimataifa.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, mashambulizi ya walowezi wa Kizayuni na vitendo haramu vya Israel katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu vinachochea ukosefu wa amani, ghasia na misimamo mikali na kudhoofisha juhudi za kimataifa za kuleta amani.
Pakistan na nchi hizo za Kiislamu zimetoa wito kwa jamii ya kimataifa kutekeleza wajibu wake wa kisheria na kimaadili na kuilazimisha Israel iachane na sera zake haramu, kukomesha ghasia za walowezi na kuwawajibisha wahusika wa mashambulizi hayo.
Taarifa hiyo sambamba na kuonyesha mshikamano kamili na wananchi wa Palestina imesisitiza uungaji mkono wake kwa haki halali na zisizoweza kupokonywa za Wapalestina ikiwemo haki ya kujitawala na kuanzishwa nchi huru ya Palestina.
Nchi hizo za Kiislamu pia zimesisitiza uungaji mkono wao kwa juhudi zozote za kukomesha uvamizi huo na kufikia amani ya haki, ya kudumu na ya kina inayotokana na maazimio ya Umoja wa Mataifa na Mpango wa Amani wa Kiarabu.