Chanzo cha picha, Getty Images
Siku moja baada ya kutiwa saini kwa makubaliano kati ya Iran na Marekani, Rais wa Marekani Donald Trump amesema anatarajia usitishaji mapigano kuheshimiwa katika maeneo yote ya mzozo, ikiwemo Lebanon.
Wakati nchini Marekani mjadala mkubwa umejikita katika masharti ya kiuchumi na vipengele vinavyohusu mpango wa nyuklia wa Iran, mjini Tehran mjadala umeelekezwa zaidi kwenye hatma ya Mlango Bahari wa Hormuz na kuendelea kuwepo kwa majeshi ya Israel nchini Lebanon. Masuala hayo yamevutia kwa kiasi kikubwa viongozi wa Iran, hususan wahafidhina wenye msimamo mkali.
Alhamisi, katika ujumbe uliohusishwa na Mojtaba Khamenei, anayeelezwa kama kiongozi mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alisema alikuwa na mtazamo tofauti kuhusu makubaliano hayo, lakini alikubali yaendelee na sasa anasubiri kuona jinsi yatakavyotekelezwa.
Wakati huo huo nchini Uswisi, ambako mazungumzo zaidi yanatarajiwa kufanyika, usalama umeimarishwa katika eneo litakalowakutanisha Makamu wa Rais wa Marekani J.D. Vance na Spika wa Bunge la Iran Mohammad Baqer Qalibaf siku ya Ijumaa.