
YANGA imewasili jijini Dar es Salaam jana ikitokea Arusha ilipoichapa Fountain Gate mabao 2-0 ikirudi juu ya msimamo, ilichofanya ikatoka na kugeuka upande mwingine wa uwanja wa ndege ikiwafuata Azam FC lakini kabla ya safari hiyo kocha wao akawazungumzia washambuliaji wake wawili akiwemo Laurindo Aurelio ‘Depu’.
Depu Alhamisi Juni 18, alifunga bao lake la saba msimu huu kwenye ligi akimaliza ukame wa muda mrefu na mshambuliaji huyo raia wa Angola, kabla ya bao hilo alifunga kwenye mechi dhidi ya Prisons Machi 12,2026, zikipita mechi nane bila kufunga huku tano akizikosa kutokana kuwa majeruhi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Abdihamid Moalin ambaye ni kocha wa muda wa Yanga, alisema hatua ya Depu kuanza kufunga ni habari njema kwa kikosi hicho na sasa mshambuliaji huyo atarudisha hali ya kujiamini na kuendelea kutupia wavuni.
Moalin alisema walijua ukame ambao alipitia Depu utapita na sasa wanaamini bao hilo litafungua mabao mengine kwenye mechi ambazo zimesalia kumalizia msimu huu,huku akisisitiza bado benchi lake lina imani na Muangola huyo.
“Bila shaka ni hatua nzuri kuona Depu akirudi kwenye rekodi za kufunga, wote tunafahamu huyu ni mchezaji mwenye kiwango kikubwa ndio maana yupo hapa timu kubwa, nadhani sasa bao hili litamjenga zaidi ajiamini na kufunga zaidi,” alisema Moalin.
Ukijua soka huwezi kupata shida na mchezaji wako akikutana na wakati mgumu, kuna mechi nane hapa zilipita bila Depu kufunga lakini tuliendelea kumpa muda wa kucheza, tulia mini hicho kipi ndi kigumu kitapita.
Aidha Moalin alisema baada ya Depu, wanaamini pia mshambuliaji wao mwingine Prince Dube atafunga muda sio mrefu kwa kuwa naye ana juhudi kubwa na uwezo mkubwa wa kufanya mambo makubwa.
“Dube pia wakati wowote atarudi kufunga, tunaamini hilo, ni mshambuliaji mwingine bora ambaye tunaye kwenye kikosi chetu, atamaliza wakati mgumu anaopitia kucheza mechi nyingi bila kufunga hii ni kawaida.
Hatuwezi kuwa kama mashabiki wachache ambao wanakata tamaa, tunawaamini sana ndio maana hata wakati hawafungi bado waliitwa timu za taifa na wakaenda kufanya vizuri, kinachozingatiwa hapa ni daraja la ubora wao.
“Jana (juzi) tulimpumzisha (Dube) ili aweze kurudisha utimamu wa mwili wake, usisahau ni mmoja kati ya wachezaji ambao wamecheza sana, sio kwamba alikuwa na tatizo, atarudi na atafanya yale ambayo watu wanatamani kuona anayafanya.”
Dube mpaka juzi dhidi ya Fountain Gate alipoingia kipindi cha pili amecheza jumla ya mechi saba bila kufunga bao ambapo mara ya mwisho kuifungia Yanga ilikuwa kwenye sare ya mabao 2-2 dhidi ya Simba, alipofunga bao la kwanza katika mechi hiyo iliyopigwa Mei 3,2026 kwa sasa akiwa na mabao tisa.