
Kamandi Kuu ya Majeshi ya Iran imetangaza rasmi kwamba Lango-Bahari la Hormuz limefungwa kwa vyombo vyote vya usafirishaji wa baharini, baada ya Marekani na Israel kukiuka makubaliano ya hati ya maelewano ya kusitisha vita kati ya Tehran na Washington.
Katika taarifa rasmi iliyotolewa mapema leo Jumamosi, Kamandi Kuu ya Majeshi ya Iran, Khatamul-Anbiya, imesema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na “ukiukwaji wa wazi wa kifungu cha kwanza cha mkataba wa hati ya maelewano wa baada ya vita na Marekani” na “ukiukwaji wa usitishaji mapigano kusini mwa Lebanon.”
Taarifa ya Kamandi Kuu ya Majeshi ya Iran imeanza kwa Aya ya Qur’ani Tukufu inayoelezea ulazima wa kupambana na makundi yanavyopinga dini yanayovunja na kukiuka ahadi zao inayosema:
Na wakivunja viapo vyao baada ya kuahidi kwao, na wakatukana dini yenu, basi piganeni na viongozi wa ukafiri. Hakika hao hawana viapo vya kweli, ili wapate kukoma. (Tauba:12)
Taarifa hiyo imesema, kufungwa Lango Bahari la Hormuz pia ni jibu kwa ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano unaoendelea kufanywa na utawala wa Israel kusini mwa Lebanon.
Kamandi Kuu ya Majeshi ya Iran imeongeza kuwa mashambulizi ya Israel huko Lebanon yamesababisha “mauaji ya kikatili na kulazimisha mamia ya maelfu ya watu kuhama makazi yao”, ikiongeza kuwa utawala wa Israel pia umeskataa kuondoa vikosi vyake katika kusini mwa Lebano.
Taarifa hiyo mesema kwamba kufungwa Lango-Bahari la Hormuz ni hatua ya kwanza katika kukabiliana na ukiukaji wa makubaliano hayo chini ya Hati ya Maelewano iliyosainiwa na marais wa Iran na Marekani, na kuongeza kwamba Iran itachukua hatua zaidi za kumlazimisha adui kutimiza majukumu yake.
Hati hiyo, iliyosainiwa na marais wa nchi hizo mbili mapema Jumatano, inalenga kukomesha kabisa vita vya uchokozi vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, ambavyo vilianza mwishoni mwa Februari.
Mkataba huo wenye vifungu 14 unaitaka Iran kufungua tena Lango-Bahari la Hormuz, njia muhimu kwa mtiririko wa nishati duniani, na inaita Marekani na washirika wake wakomeshe kabisa uchokozi na mashambulizi dhidi ya Iran na washirika wake wa kikanda.
Hata hivyo Israel imeendelea kukiuka makubaliano hayo kwa kushambulia maeneo ya kusini mwa Lebanon na kuua raia wasio na hatia.
Mapema leo Shirika la Ulinzi wa Raia la Lebanon limetangaza kuwa mashambulizi ya Israel katika wilaya ya Nabatieh kusini mwa Lebanon yamewaua watu wasiopungua 16 na kujeruhi wengine 12.
Mauaji hayo wanakuja siku moja baada ya watu wasiopungua 47 kuuawa na wengine 97 kujeruhiwa katika mashambulizi ya anga ya Israel kusini na mashariki mwa Lebanon, kama ilivyoripotiwa na Wizara ya Afya ya nchi hiyo.