
Syed Mohsin Raza Naqvi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan amerejea tena Tehran kwa ajili ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa ngazi za juu wa Iran, kuhusu suala la kuendeleza mazungumzo kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani.
Naqvi amewasili leo Jumamosi mjini Tehran kwa madhumuni ya kujadili na kufuatilia maendeleo yaliyopatikana katika mazungumzo kati ya Iran na Marekani, na wakati huo huo kuondoa vikwazo vyovyote vinavyoweza kukwamisha mapatano ya kupatikana amani ya kudumu katika eneo.
Hii ni safari ya karibuni zaidi ya Naqvi mjini Tehran tangu Pakistan ilipochukua jukumu la kufanya juhudi za upatanishi kufuatia uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu mwishoni mwa mwezi Februari.
Katika safari yake ya awali tarehe 7 Juni, alikuwa na mikutano muhimu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi pamoja na Waziri mwenzake wa Mambo ya Ndani wa Iran Eskandar Momeni.
Pakistan ilipatanisha kwa mafanikio usitishaji vita kati ya Tehran na Washington, ambao ulianza kutekelezwa tarehe 8 Aprili. Tangu wakati huo, viongozi wa Pakistan wamekuwa wakifanya safari za mara kwa mara nchini Marekani na Iran kwa ajili ya kufanya makubaliano ya amani ya kudumu kati ya nchi hizi mbili.
Siku ya Jumatano, marais wa Iran na Marekani walitia saini rasmi Mkataba wa Maelewano wa Islamabad (MoU).
Shahbaz Sharif, Waziri Mkuu wa Pakistan alimpongeza Rais Masoud Pezeshkian wa Iran, uongozi wa Iran, pamoja na wananchi wa Iran kufuatia kusainiwa rasmi makubaliano hayo, akiangazia taathira zake chanya katika kuchangia utulivu na ushirikiano wa kikanda kati ya Iran na Pakistan.
Makubaliano hayo yenye vipengele 14, yaliyotiwa saini kielektroniki na Marais Masoud Pezeshkian wa Iran na Donald Trump wa Marekani, yanakusudia kusimamisha kabisa uhasama katika nyanja zote za mapigano, ikiwa ni pamoja na Lebanon, kuondolewa vikwazo vya kijeshi vya Marekani dhidi ya Iran ndani ya siku 30, na kurejeshwa safari za meli za kibiashara kupitia Lango-Bahari la Hormuz.
Rasimu ya makubaliano hayo pia inajumuisha mpango wa ujenzi mpya na maendeleo ya kiuchumi kwa Iran wenye thamani ya dola zisizopungua bilioni 300, kuondolewa kwa awamu vikwazo vya Marekani, kuachiliwa mali inayozuiwa ya Iran, na ahadi mpya ya Iran kutotengeneza silaha za nyuklia, wakati mazungumzo zaidi yanaendelea kuhusu hifadhi ya urani iliyorutubishwa na Tehran.